Hekima Na Mawaidha Mazuri Aya 125 -128



Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.

Aya hii inatupa mwongozo wa mambo yafuatayo:-
1. Mwito unapasa uwe wa haki usiokuwa na lengo jingine lolote. Mtu yeyote anayetoa mwito usiokuwa wa haki, basi mwito wake utakuwa ni ufisadi na upotofu. Kosa kubwa zaidi ni la yule anayeufanya mwito wa kumwendea Mungu na kwenye haki kuwa ni nyenzo za kufikia kwenye mambo yake na jaha yake; kama wafanyavyo viongozi na maraisi wa dini na dunia.
2. Mwito uwe kwa hekima na mawaidha mazuri. Ni wazi kuwa vitenda kazi vya hekima ni elimu na akili. Akili ndiyo itakayoweza kutofautisha anayetoa mwito wa haki na wa batili na wa heri na wa sahari. Hali za wahutubiaji hujulikana kulingana na ukali na upole.
3. Mawaidha mazuri zaidi ni kuhutubia yule anayemuongoza aliyekosea kwa mfumo unaotambulisha kuwa amekosea, sio kurukia kwa lawama. Walishasema wa kale: “Kubembeleza ni ufasaha zaidi kuliko kuweka wazi” Kwa maneno mengine ni kuwa mwaidha mazuri ndiyo yanayopelekea kufikia malengo; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Pinga kwa lililo zuri. Hapo yule ambaye baina yako na yeye pana uadui atakuwa kama rafiki mkubwa” (42: 34).
Kujadiliana kwa namna iliyo bora. Hilo litakuwa ikiwa lengo ni kuidhi- hirisha haki na kukinaisha, sio kwa lengo la ushindi na kuziba mdomo wa mwengine.
Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka.
Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamuru Mtume wake kufikisha (tabligh) kwa hekima na kujadiliana vizuri, sasa anamwambia kuwa hilo tu ndio lililo wajibu juu yake. Ama uwongofu hana jukumu nao. Hii ni kuonyesha kuwa hamasa katika mwito (da’wa) haifai katika mambo yote na hali zote. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Sema hii ni haki itokayo kwa Mola wenu, anayetaka na aiamini na anayetaka aikatae” (18: 29).
Na kama mkilipiza basi lipizeni kama mlivyofanyiwa.
Aya hii ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Basi wanaowachokoza, pia nanyi wachokozeni kwa kadiri walivyowachokoza.” Juz.2 (2:193).
Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Aya hii ilishuka Madina, iliyoingizwa kwenye Sura ya Makka na kwamba sababu ya kushuka kwake ni kuwa washirikina walizikatakata maiti za Waislamu katika vita vya Uhudi; hasa Hamza bin Abdul-Mutwalib, walimpasua tumbo lake, na Hind akachukua ini lake akalitafuna. Wakamakata pua na masikio na wakamkata mkono wake wa kuume. Waislamu wakasema: Tukiwapata, wachilia mbali waliokufa; hata walio hai tutawakatakata. Ndipo ikashuka Aya hii.
Na kama mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanaosubiri.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria kuwa kisasi kizidi mfano wake, sasa anasema kuwa kusamehe na kuvunja ghadhabu ni bora zaidi; kama alivyosema mahali pengine: “Na anayesubiri na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa” (42:43).
Na subiri na subira yako haikuwa ila kwa Mwenyezi Mungu.
Yaani kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na tawfiki yake. Maneno haya anaambiwa Muhammad (s.a.w.), lakini wanakusudiwa wote. Tumezungumzia kuhusu subira katika Juz. 2 (2:153–155).
Wala usihuzunike wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazozifanya.
Hakuna yeyote anayetoa mwito wa heri ila atapambana na maudhi na kero za watu wa shari. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuusia kila anayelingania kwenye njia yake kutohuzunika kwa kufanywa mwongo na upinzani wa mwenye kupinga mwito wake. Kwa sababu mwisho siku zote ni wa mwenye kumcha Mungu:
Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kucha yale aliyowayaharamisha kwa kumuogopa Yeye na wale ambao wanatenda mema kwa kuipiga vita batili na watu wake na kuwasamehe watu katika haki binafsi sio haki za umma.

Comments

Popular posts from this blog

NAMNA YA KUSWALI HATUA KWA HATUA

UTUKUFU WA MJI WA MAKKA NA MSIKITI MTUKUFU

Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1