Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1
UTANGULIZI
Ibraahiym عليه السلام alizaliwa Iraq, inavyosemekana Babylonia. Baba yake akiitwa Aazar na kauli nyingine inasema kuwa huyu ni ami yake aliyemlea tokea mdogo baada ya kufa baba yake. Allaah سبحانه وتعالى Anajua zaidi. Na huyu Aazar alikuwa akichonga masanamu.
Ibraahiym عليه السلام ni Khaliylul-Allaah yaani 'rafiki mwendani wa Allaah' Amemchagua kumpa ujumbe na Akamfadhilisha zaidi ya viumbe Vyake vingine.
Alikuwa akiishi na watu waliokuwa wakiabudu sayari (nyota, mwezi, jua na kadhalika), na wengine wakiabudu masanamu na wengine wakiabudu wafalme wao. Hakuridhika na ibada hizo zao, bali alihisi kuwa yupo Aliyeanzisha maumbile yote na kwamba kuna Mungu Mtukufu Anayestahiki kuabudiwa. Akawa anawaza na kutafuta uhakika hadi Allaah سبحانه وتعالى Akamhidi na kumchagua kumpa utume.
Akaanza Ibraahiym عليه السلام kuwaita watu wake katika Tawhiyd yaani ibada ya kumuabu Allaah Pekee, lakini hawakumuamini bali walimkanusha na wakajaribu kumuunguza katika moto lakini Allaah سبحانه وتعالى Alimuokoa mbele ya macho yao. Kisha Allaah سبحانه وتعالى Akamjaalia kupata watoto wawili ambao ni Ismaa'iyl عليه السلام na Is-haaq عليه السلام ambao ndio waliotoa vizazi vilivyotoa Mitume yote iliyobakia kama ifuatavyo:
Is-haaqعليه السلام alimzaa Ya'aquub ambaye ndiye aliyejaaliwa kutoa kizazi cha Mitume yote iliyobakia hadi 'Iysaعليه السلام . Baada ya hapo tena ikapita miaka takriban mia sita ndipo akatoka Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم kutoka kizazi cha mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام ambaye alimuacha Makkah pamoja na mama yake Haajar عليها السلام
Ibraahiym عليه السلام na mwanamwe Ismaa'iyl عليه السلام ndio waliojenga Ka'abah Makkah, mahali ambako ni patukufu kabisa na kama tunavyojua ndiko Ummah wote wa Kiislamu unapoelekea kutimiza fardhi ya Hajj ambayo ni nguzo ya tano ya Kiislamu.
FADHILA ZA IBRAAHIYM
Fadhila za Ibraahiym عليه السلام ni nyingi kabisa kutokana na mafundisho tunayopata katika Qur-aan na Hadiyth, na katika Qur-aan ametajwa mara nyingi katika sura nyingi mbali mbali.
Kwa kifupi zifuatazo ni baadhi ya fadhila zake:
1-Baba wa Manabii kwani kizazi chake ndicho kilichotoa Mitume yote iliyobaki.
2-Khaliyul-Allaah (rafiki mwendani) kama Alivyosema Allaah سبحانه وتعالى :
((وَمَنْ أَحْسَنُ دِينًا مِّمَّنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لله وَهُوَ مُحْسِنٌ واتَّبَعَ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَاتَّخَذَ الله إِبْرَاهِيمَ خَلِيلاً))
((Na nani aliye bora kwa dini kuliko yule aliyeusilimisha uso wake kwa Allaah, naye akawa mwema, na anafuata mila ya Ibraahiym (kuwa Muislam kweli kweli) Na Allaah Alimfanya Ibraahiym kuwa ni kipenzi chake)) [An-Nisaa:125]
3-Alikuwa ni Imaam na kiongozi kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى
((وَإِذِ ابْتَلَى إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ فَأَتَمَّهُنَّ قَالَ إِنِّي جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَامًا))
((Na Mola wake Alipomjaribu Ibraahiym kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza, akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe kiongozi wa watu)) [Al-Baqarah:124]
4-Ndiye aliyejenga Kaaba
5- Kizazi chake ndicho kilichotoa Mtume wa mwisho.
6-Ni miongoni mwa mitume watano walioitwa Ulul-'azm ni mitume waliopata tabu sana na watu. Wametajwa katika aya ifuatayo:
((وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَى وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ وَأَخَذْنَا
مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا))
((Na tulipochukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuwh na Ibraahiym na 'Iysaa mwana wa Maryam, na tulichukua kwao ahadi ngumu)) [Al-Ahzaab:7]
7-Allaah سبحانه وتعالى Amejaalia kuwa mila yake kuwa ni Tawhiyd khalisi isiyokuwa na aina yoyote ya shirk na Akajaalia walio na akili kufuata dini yake.
((إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِلّهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ))
((Hakika Ibraahiym alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu kwa Allaah, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina)) [An-Nahl:120]
8.-Mtu wa kwanza kuvalishwa nguo siku ya kufufuliwa kama ilivyokuja nasw katika Hadiyth:
عن ابن عباس رضي الله عنهما عن النبي صلى الله عليه وسلم قال:((إنكم محشورون حفاة
عراة غرلا ثم قرأ: ((كما بدأنا أول خلق نعيده)) وأول من يكسى يوم القيامة إبراهيم)) البخاري ومسلم
Imetoka kwa ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Mtafufuliwa bila ya viatu, uchi na bila ya kutahiriwa kisha akasoma ((Kama Tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena)) na wa kwanza kuvalishwa nguo siku ya Qiyaamah ni Ibraahiym)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Fadhila hii ni kwa sababu alipopelekwa na watu wake kuunguzwa moto bila ya kuwa na dhambi bali alikuwa na Tawhiyd.
UTOTO WAKE NA DA'WAH KWA WATU WAKE
Tokea utoto wake Ibraahiym عليه السلام alikuwa akiyachukia hayo masanamu kwani alishangaa kuwa vipi wanaabudu mawe ambayo wanayachonga wenyewe na ambayo hayakuweza kumdhuru au kumfaa mtu kwa chochote? Allaah سبحانه وتعالى Alimpa uongofu tokea mdogo:
((وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِه عَالِمِينَ))
((Na hakika Tulikwishampa Ibraahiym uongofu wake zamani, na Tulikuwa tunamjua)) [Al-Anbiyaa:51]
Akawa anajadiliana na watu wake ili awatoe katika upotofu:
((إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا هَذِهِ التَّمَاثِيلُ الَّتِي أَنتُمْ لَهَا عَاكِفُونَ))
((Alipomwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu?)) [Al-Anbiyaa:52 ]
Lakini kama kawaida ya watu, kila walivyokuwa wakiitwa katika Tawhyid, jibu kubwa lilikuwa kwamba wamekuta wazazi wao wanafanya hivyo. Lakini Ibraahiym عليه السلام hakuacha kuendelea kujadiliana nao:
(( قَالُوا وَجَدْنَا آبَاءنَا لَهَا عَابِدِينَ((
(( قَالَ لَقَدْ كُنتُمْ أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمْ فِي ضَلاَلٍ مُّبِينٍ))
(( قَالُوا أَجِئْتَنَا بِالْحَقِّ أَمْ أَنتَ مِنَ اللَّاعِبِينَ))
(( قَالَ بَل رَّبُّكُمْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الَّذِي فَطَرَهُنَّ وَأَنَا عَلَى ذَلِكُم مِّنَ الشَّاهِدِينَ))
((Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu))
((Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotofu ulio dhahiri))
((Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu?))
((Akasema: Bali Mola wenu ni Mola wa mbingu na ardhi Ambaye Ndiye Aliyeziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo)) [Al-Anbiyaa: 53-56]
Akaendelea kuwauliza vipi wanaabudu vitu visivyoona au kusikia wala kuwafaa au kuwadhuru? Na majibu yao yakawa ni hayo hayo tu:
((وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ إِبْرَاهِيم))
(( إِذْ قَالَ لأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا تَعْبُدُونَ))
((قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ ))
(( قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ))
((أَوْ يَنفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ))
(( قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آبَاءنَا كَذَلِكَ يَفْعَلُونَ))
((قَالَ أَفَرَأَيْتُم مَّا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ))
((أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمُ الأََقْدَمُونَ))
((Na wasomee khabari za Ibraahiym ))
((Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?))
((Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea))
((Akasema: Je! Yanakusikieni mnapoyaita?))
((Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?))
((Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo))
((Je! Mmewaona hawa mnaowaabudu))
((Nyinyi na baba zenu wa zamani?)) [Ash-Shu'araa :69-76]
TAWHIYD INAMDHIHIRIKIA IBRAAHIYM عليه السلام
Tufahamu kuwa Ibraahiym عليه السلام alihojiana na watu wake kwanza kuhusu upotofu wa kuabudu masanamu ambao waliwafanya kuwa ni wa kuwakuribisha (kuwaweka karibu) na Allaah سبحانه وتعالى. Watu wake walifikiri kuwa haikuleta maana au haikuwa na thamani kumuabudu Allaah سبحانه وتعالى Pekee bali kuweko kitu cha kuwakuribisha Naye. Na hii ndio shirk kwani Allaah سبحانه وتعالى Hahitaji kuombwa kwa kupitia mtu au kitu chochote, bali huombwa Mwenyewe moja kwa moja.
Aliendelea kuwaza kuhusu vitu wanavyoabudu zaidi ya masanamu, kama vile sayari, ikawa haimuingii akilini kabisa vitu hivi kuwa ndio mungu. Allaah سبحانه وتعالى Akataka kumdhihirishia Tawhyid kwake. Akawa anatoka kila siku kuangaza juu kuwaza maumbile ya Allaah سبحانه وتعالى.
Akataamali na kutambua kuwa vyote hivyo ni vitu vyenye kutoweka naye hakuona kama Mungu Anaweza kutoweka.
((وَكَذَلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ))
((فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَى كَوْكَبًا قَالَ هَذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لا أُحِبُّ الآفِلِينَ))
((فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمْ يَهْدِنِي رَبِّي لأكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ))
((فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَذَا رَبِّي هَذَآ أَكْبَرُ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ))
((Na kadhaalika Tulimwonyesha Ibraahiym ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini))
((Na ulipomuingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola wangu. Ilipotua akasema: Siwapendi wanaotua))
((Alipouona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola wangu Hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu waliopotea))
((Na alipoliona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipotua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayofanyia ushirikina)) [Al-An'aam: 75-78]
Akazidi kutambua kuwa ibada hiyo ni shirk na kwamba yuko Mungu Aliyeanzisha vitu vyote hivyo vinavyoelea katika mbingu, bali ndiye Muumba wa mbingu na ardhi na vyote viliomo ndani. Akataka kuwafahamisha watu wake upotofu wa kuabudu sayari
Na ndipo akasema:
((إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ حَنِيفًا وَمَا أَنَاْ مِنَ الْمُشْرِكِينَ))
((Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa Aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina)) [Al-An'aam:79]
Maana kwamba, mimi namuabudu Muumba wa vitu hivi Aliyevianzisha na Kuvikadiria na Anayemiliki shuhguli zake na Aliyevifanya vinyenyekee Kwake. Ni Yeye Ambaye Amemiliki kila kitu katika Mikono Yake, Ufalme wote ni Wake na ni Muumba Pekee wa kila kitu na Ndiye Anayepasa kuabudiwa Pekee.
Aayah hizi zinatufahamisha kuwa Ibraahiym عليه السلام alikuwa akihojiana na watu wake kuhusu shirki waliyokuwa wakiifanya,
((وَحَآجَّهُ قَوْمُهُ قَالَ أَتُحَاجُّونِّي فِي اللّهِ وَقَدْ هَدَانِ وَلاَ أَخَافُ مَا تُشْرِكُونَ بِهِ إِلاَّ أَن يَشَاء رَبِّي شَيْئًا وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا أَفَلاَ تَتَذَكَّرُونَ))
((Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Allaah, na hali Yeye Ameniongoa? Wala siogopi hao mnaowashirikisha Naye, ila Mola wangu Akipenda kitu. Mola wangu Amekusanya ilimu ya kila kitu. Basi je, hamkumbuki?)) [Al-An'aam:80]
Aya ina maana kwamba: Mnanihoji kuhusu Allaah Ambaye hakuna Apasaye kuabudiwa isipokuwa yeye? Naye Amenihidi mimi katika haki na Amenifanya nitambue hivyo. Kwa hiyo vipi nizingatie kauli zenu za upotofu na shaka iliyo batili? Na miongoni mwa dalili ya upotofu wa 'Aqiydah (Iymaan) yenu ni kwamba hiyo miungu ya uongo mnayoiabudu haileti athari yoyote na mimi siiogopi wala siijali. Kwa hiyo kama hiyo miungu inaweza kusababisha madhara basi itumilieni dhidi yangu inidhuru na wala msinipe muda wa kuomba msamaha, kwani nnayosema ni haki na pia hamtaweza kunidhuru ila Akipenda Allaah kwani Yeye Ndiye Mwenye kudhuru na Mwenye kunufaisha.
((وَكَيْفَ أَخَافُ مَا أَشْرَكْتُمْ وَلاَ تَخَافُونَ أَنَّكُمْ أَشْرَكْتُم بِاللّهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا فَأَيُّ الْفَرِيقَيْنِ أَحَقُّ بِالأَمْنِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ))
((Na vipi nivikhofu hivyo mnavyovishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Allaah na kitu ambacho Hakukiteremshia uthibitisho. Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua?)) [Al-An'aam:81]
Maana: Vipi nikhofu masanamu mnayoabudu badala ya Allaah? Na nyinyi hamna khofu ya kumshiriki Allaah kwa miungu mnayoiabudu mkaifanya dini Asiyoitolea Allaah ruhusa Yake? Basi nani miongoni mwetu sisi yuko katika haki? Wale wanaomuabudu Ambaye Ana uwezo wa kudhuru na kunufaisha au wanaoabudu ambao hawawezi kuleta madhara wala manufaa na bila ya ruhusa ya kuthibitisha kuabudu kwao? Nani miongoni mwa makundi haya mawili ana haki ya kuhifadhiwa na adhabu ya Allaah siku ya Qiyaamah?
MJADALA BAINA YA IBRAAHIYM عليه السلام NA MFALME NIMRUUD
Imenukuliwa kuwa Nimruud alikuwa mfalme na alitoka katika kizazi cha Nuuh عليه السلام . Jina lake lilikuwa Nimruud bin Canaan, bin Kush, bin Sam bin Nuuh. [Amenukuu Mujaahid - Tafsyir Ibn Kathiyr 2:35].
Mujaahid vile vile amesema: "Wafalme waliotawala pande za Mashariki na Magharibi za dunia walikuwa wanne, wawili walioamini; Sulaymaan bin Daawuud na Dhul-Qarnayn. Ama waliokuwa makafiri ni; Nimruud na Nebuchadnezzar" [At-Twabariy 5:433] Na Allaah Anajua zaidi.
Mfalme huyo alikanusha kuweko Allaah, na alijiona yeye ndiye mungu pekee kama vile alivyodai Fir'awn. Na kilichomfanya huyu Nimruud kuwa dhalimu na kukiri uungu wake ni kwa vile alitawala kwa muda mrefu.
Aliposikia kuwa Ibraahiym عليه السلام Anasema kuwa kuna Mungu Ambaye Ndiye Apasaye kuabudiwa na kwamba Yeye Ndiye mwenye kumiliki nafsi zetu kutuhuisha na kutufisha kama zinavyoelezea aya zifuatazo:
((فَإِنَّهُمْ عَدُوٌّ لِّي إِلأَّ رَبَّ الْعَالَمِينَ))
((الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ))
((وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ))
((وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ))
((وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ))
((وَالَّذِي أَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ))
((Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola wa walimwengu wote))
((Ambaye Ndiye Aliyeniumba, na Yeye Ndiye Ananiongoa))
((Na Ambaye Ndiye Ananilisha na Kuninywesha))
((Na ninapougua ni Yeye Ndiye Anayeniponesha))
((Na Ambaye Atanifisha, na kisha Atanihuisha))
((Na Ambaye Ndiye ninayemtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo)) [As-Shu'araa: 77-82]
Akamhoji Ibraahiym عليه السلام kuhusu Mungu wake na akataka dalili kama kweli Allaah Yupo. Naye akamjibu kuwa Allaah Ndiye Mwenye kuhuisha na kufisha. Naye Nimruud akasema kuwa yeye hali kadhalika anaweza kufanya hivyo.
Akaamrisha waletwe watu wawili ambao walikuwa wamehukumiwa kuuliwa mbele yake na akasema kuwa watakapoletwa ataweza kumuacha mmoja huru na mmoja ataamrisha auliwe. Na hivi ndio maana ya kuwa naye anao uwezo wa kuhuisha na kufisha. [At-Twabariy 5:433,436,437 imepokelewa na Qataadah, Muhammad bin Is-haaq na As-Suddi]
Ibraahiym عليه السلام akamuambia kuwa ikiwa yeye anadai hivyo, basi mwenye uwezo wa kufanya hivyo pia atakuwa na uwezo wa kudhibiti ulimwengu na viliomo ndani pamoja na kudhibiti sayari na mizunguko yake. Mfano jua linachomoza kila siku upande wa Mashariki kwa hiyo kama wewe Nimruud ni mungu kweli basi lifanye lichomoze upande wa Magharibi. Kwa vile Nimruud alitambua udhaifu wake wa kutokuwa na uwezo kama huu, alinyamaza kimya na hakuweza kujibu lolote bali alitahayarika. Allaah سبحانه وتعالى Ametuelezea katika Qur-aan haya:
((أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِي حَآجَّ إِبْرَاهِيمَ فِي رِبِّهِ أَنْ آتَاهُ اللّهُ الْمُلْكَ إِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللّهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ وَاللّهُ لاَ يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ))
((Hukumuona yule aliyehojiana na Ibraahiym juu ya Mola wake kwa sababu Allaah Alimpa ufalme? Ibraahiym aliposema: Mola wangu ni Yule Ambaye Huhuisha na Kufisha. Yeye akasema: Mimi pia nahuisha na kufisha. Ibraahiym akasema: Allaah Hulichomozesha jua mashariki, basi wewe lichomozeshe magharibi. Akafedheheka yule aliyekufuru; na Allaah Hawaongoi watu madhaalimu)) [Al-Baqarah:258]
ALLAAH سبحانه وتعالى AMEMUANGAMIZA NIMRUUD KWA MBU TU
Imesemekana kwamba kifo cha Nimruud kilisababishwa na mbu. Allaah سبحانه وتعالى Aliangamiza jeshi lake kwa kuwatumia mbu wengi, naye Nimruud almuingia mbu mmoja sikioni akafika kwenye ubongo wake. Mbu huyo akawa anamkera sana alipokuwa akizunguka katika ubongo wake. Ikawa nafuu yake ni kujipiga kichwa kila mara alipokuwa akimzunguka mbu huyo. Na mpigo mmoja wa nguvu ndio ulisababisha mauti yake. [Aysarut-tafaasiyr 1:248 - Abu-Bakr Al-Jazaairiy]
IBRAAHIYM عليه السلام ANAMUOMBA ALLAAH سبحانه وتعالى AMUONYESHE VIPI ANAHUISHA ALIYEKUFA
Maulamaa wamesema kwamba kuna sababu ya ombi hili la Ibraahiym عليه السلام kutaka kuonyeshwa vipi Allaah سبحانه وتعالى Anahuisha aliyekufa. Mfano Ibraahiym عليه السلام alipomuambia Nimruud kwamba "Mola wangu ni Yule Ambaye Huhuisha na Kufisha". Alitaka kuithibitisha elimu yake kuhusu kufufuliwa kwa kuona wazi mbele ya macho yake. Na ndipo alipomuomba Allaah سبحانه وتعالى:
((رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَى))
((Mola wangu ! Nionyeshe vipi unavyofufua wafu))
Allaah سبحانه وتعالى Akamjibu:
((أَوَلَمْ تُؤْمِن قَالَ بَلَى وَلَكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي))
((Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue)) [Al-Baqarah:260]
Hadiyth Swahiyh ifuatayo inatuonyesha kuwa sisi tunawajibika zaidi kutafuta uhakika.
عن أبي هريرة، رضي الله عنه، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((نحن أحق بالشك من إبراهيم، إذ قال:
((رب أرني كيف تحيى الموتى قال: أو لم تؤمن. قال: بلى، ولكن ليطمئن قلبي)))) البخاري
Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Sisi tunawajibika zaidi kuliko Ibraahiym aliposema: ((Mola wangu ! Nionyeshe vipi unavyofufua wafu. Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue)))) [Al-Bukhaariy]
Allaah سبحانه وتعالى Akamtakabalia Ibraahiym عليه السلام ombi lake na Akampa matumaini kwa kumtaka achukue ndege wanne. Maulamaa wa Tasfiyr wamekhtilafiana kuhusu aina ya ndege waliotajwa kwani haikuelezwa ndege aina gani. Allaah سبحانه وتعالى Akamtaka Ibraahiym عليه السلام awazoeshe kwake kwanza wamzoee, kisha awakate vipande vipande.
[Ibn 'Abbaas, Ikrimah, Sa'iyd bin Jubayr, Abu Malik, Abu Al-Aswad, Ad-Dili, Wahb bin Munabbih, Al Hassan na As-Sudi kutoka Ibn Haatim 3:109,1040]
Ibraahiym عليه السلام akawazoesha, kisha akawachinja na kuwatoa manyoa na kuwakata vipande vipande kisha akavichanganya vipande hivyo pamoja. Kisha akagawa vipande na kuviweka katika vilima vinne au saba. Ibn 'Abbaas amesema, "Ibraahiym عليه السلام aliweka vichwa vya ndege hao katika mikono yake". Kisha akafanya kama Allaah سبحانه وتعالى Alivyomuamrisha kuwaita hao ndege kwake. Akashuhudia kwa macho yake manyoya, damu na viungo vya hao ndege vikiruka kujiunga na kiungo cha mwili wake kila mmoja mpaka kila ndege akarudi kuwa hai na wakawa wanakuja mbele ya Ibraahiym عليه السلام wakitembea haraka kuelekea kwake, ili Ibraahiym عليه السلام ashuhudie kwa dhahiri kuhuishwa kwa ndege hao na apate na matumaini.
Kila ndege alikwenda kwa Ibraahiym عليه السلام kuchukua kichwa chake mikononi mwa Ibraahiym عليه السلام na alipojaribu kumpa ndege mmoja kichwa cha ndege mwingine, ndege alikataa kupokea au kujiunga. Subhana Allaah! Kwa hiyo kila kichwa cha ndege kilijunga na kile kile kiungo chake kwa uwezo wa Allaah سبحانه وتعالى. [Al-Qurtubi 3:300]
Anasema Allaah سبحانه وتعالى
وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِيۖ قَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِّنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِّنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا ۚ وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٢٦٠﴾
Na (taja) aliposema Ibraahiym: “Rabb (Mola) wangu nionyeshe vipi Unahuisha wafu?” (Allaah) Akasema: “Je kwani huamini?” Akasema: “La! (Naamini) lakini moyo wangu utumainike.” (Allaah) Akasema: “Basi chukua ndege wanne wazoeshe kwako, (kisha uwachinje), kisha weka juu ya kila jabali katika hao (ndege) sehemu yao; kisha waite watakujia mbio (ukiwaona wanavyoumbika); na jua kwamba hakika Allaah ni ‘Aziyzun-Hakiym(Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika - Mwenye hikmah wa yote).
Comments
Post a Comment