NAMNA YA KUSWALI
Nia: Nia ni sharti la swala kuwa sahihi, kwa maana ya mtu kukusudia kwa moyo wake kumuabudu Allah kwa kuswali, huku akijua kwamba swala anayoswali ni Magharibi kwa mfano au Isha. Haitakiwi na sheria kuitamka hii nia, bali makusudio ya moyoni na akilini ndio yanayotakiwa. Kuitamka Nia ni jambo ambalo hilo halikuthibiti kunukuliwa kwa Mtume,swallalahu alayhi wasalam, wala maswahaba wake watukufu. Atasimama wima kwa ajili ya swala na kusema: (Allahu Akbar). Atanyanyua mikono yake mpaka usawa wa mabega yake au juu yake huku matumbo ya viganja vya mikono akiyaelekeza upande wa Kibla. Takbira haiwi sahihi isipokuwa tu kwa tamko hili la (Allahu Akbar). Maana yake ni kumtukuza na kumuadhimisha Allah. Allah ni mkubwa zaidi kuliko kila kisichokuwa yeye. Ni mkubwa zaidi kuliko dunia pamoja na starehe zote na matamanio yote yaliyomo humo. Tunaziweka kando starehe zote hizo na tunaelekea kwa Allah mkubwa, mtukufu katika swala kwa nyoyo zetu na akili zetu huku tukiwa w...