Vazi La Hijabu La Kiislamu
Wanaume na wanawake, licha ya kwamba wanavyo vipengele vingi vinavyofanana, pia wanazo tabia za pekee. Mojawapo ya tabia hizi ni kwamba wanawake ni viumbe wa kuvutia, wazuri, na wanaopendwa. Ni wachangamfu, wanavutia na wanapendwa; ambapo wanaume huchangamshwa, huvutiwa na huwapenda wanawake kwa sifa zao.
Mwanaume anapomuoa mwanamke, hutamani uzuri wote na mapenzi yote ya mke wake visitiriwe kwa ajili yake tu.
Hutumaini kuwa ni yeye peke yake ndiye anayefaidi uchangamfu, mapenzi, kujishaua, uzuri, ukunjufu na kadhalika na kuwaepuka wanaume wengine kabisa. Mwanaume kimaumbile yu moto moto sana na hamvumilii mwanaume mwingine kumtazama mke wake au kuanzisha aina fulani ya uhusiano naye. Mwanaume ataona uhusiano wa karibu na mke wake na wanaume wengine kuwa ni kukiukwa kwa haki yake ya kisheria. Mume anatarajia mkewe kufuata kanuni ya vazi la kiislamu la Hijab na kwa kuwa mwepesi wa kubadilika kufuatana na tabia na maadili ya Kiislamu atashiriki katika kutunza haki yake ya kisheria.
Mwanaume yeyote aliye mwaminifu na hamasa lazima atakuwa na hamu hiyo. Tabia ya kijamii ya mwanamke ambayo imeegemezwa kwenye maadili ya Kiislamu, itaweka akili ya mume katika hali ya utulivu; kwa hiyo atafanya kazi kwa shauku kubwa ili aweze kutunza familia yake, na mapenzi kwa mke wake yataongezeka. Mwanaume wa namna hii hatavutiwa na wanawake wengine. Kinyume chake mwanaume ambaye mkewe havai Hijab ambayo ni vazi linalovaliwa na mwanamke Mwislamu na badala yake huonesha uzuri wake kwa wanaume wengine au anachanganyika nao, atatibuliwa sana. Atamuona mke wake kuwa anahusika na kukandamiza haki zake. Mume wa aina hiyo kila mara atapitia kwenye mateso na taabu na mapenzi kwa mkewe yatapungua pole pole.
Kwa hiyo, ni kwa manufaa ya jamii, na wanawake kwamba wanatakiwa kuvaa inavyostahiki na kuwa na tabia ya unyenyekevu, wanatakiwa kuonekana hadharani bila urembo na kuacha kuonesha uzuri wao kwa wengine.
Kuvaa Hijab ni wajibu wa Kiislamu. Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anasema kwenye Qur’ani Tukufu:
وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِنْ زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {31}
“Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho Yao, Na wazilinde tupu zao, na wala wasioneshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasioneshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyowamiki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanamume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yanayohusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikana mapambo waoliyoyafisha. Na tubuni vyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa. (Quran 24:31)
Kuchunga vazi la Kiislamu la Hijab na kuizingatiwa matumizi yake katika jamii kuna manufaa kwa wanawake katika vipengele vingi: Kwa kutumia vazi la Hijab, wanawake wanaweza kulinda uzuri wao wa kijamii na maadili ya ndani kwa ubora zaidi, na kujilinda dhidi ya kuwa tu kitu kilichopo kwenye maonesho.
Wanaweza kuthibitisha imani na mapenzi yao kwa waume zao, kwa ukamilifu zaidi na kwa hiyo kusaidia kutengeneza na kutunza familia yenye uchangamfu na kuzuia hisia mbaya na ugomvi wa kifamilia. Kwa ufupi, wanaweza kuvutia nyoyo za waume zao na kujiimarisha kwenye familia zao.
Kwa kuzingatia matumizi ya Hijab ya Kiislamu mitazamo isiyo ya kisheria yenye dokezo ya kutamani kutoka kwa watu wenye udhaifu huo, itakoma na kusaidia kupunguza idadi ya ugomvi, kuimarisha mizizi ya familia, na matokeo yake kutengeneza mazingira ya utulivu ndani ya familia.
Hijab ya Kiislamu ya wanawake pia itasaidia vijana wa kiume ambao hawajaoa, kutokana na kujiingiza kwenye vitendo viovu. Hivyo, kuwaepusha vijana dhidi ya mazingira yanayoamsha hisia za kutamaani mwanamke aliyevaa nguo isiyo sitiri umbo lake hali ambayo pia itawanufaisha wanawake katika jamii.
Kama wanawake wote wangefuata utaratibu wa Hijab ya Kiislamu basi, wanawake wote wangekuwa na uhakika kwamba waume zao wanapokuwa nje ya familia zao, hawangekutana na mwanamke asherati ambaye angewavutia na kumtoa nje ya familia yake.
Uislamu unatambua lengo mahususi ambalo limesababisha kuumbwa kwa mwanamke na humuona yeye kama msingi muhimu wa jamii na kupewa wajibu kwa jamii. Jamii humtaka mwanamke ajitolee katika kutekeleza wajibu wake wa kuvaa Hijab ya Kiislamu, ambayo ingeepusha uovu na upotofu wa jamii na kutengeneza uimara, usalama na kutukuza taifa lake. Lakini kwa wazi wazi thawabu kubwa zaidi ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mweza wa yote kwa kutekeleza wajibu wake kwa dini.
Mpendwa Bibi! Kama unapenda uimara na amani kuwepo kwenye familia yako, na mumeo aendelee kukuamini wewe siku zote, kama unajihusisha na haki za wanawake katika jamii; kama unavutiwa na afya ya vijana kiakili na unao wasi wasi kwamba wanaweza wakaacha maadili mema, kama unataka kuchukua hatua za uhakika za wanaume waovu kuacha kuwatongoza wanawake; na kama unatafuta radhi ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa Muislamu muaminifu na mwenye kujitolea, basi tumia vazi la Hijabu ya Kiislamu.
Usioneshe uzuri wako na urembo wako kwa wageni, ama uwe ndani nyumbani kwako ukiwa na ndugu zako wa karibu, au kwenye mikusanyiko mingine ya kijamii nje ya nyumbani kwako. Lazima uvae ushungi mbele ya shemeji zako na watoto wao, waume wa wifi zako, waume wa shangazi zako, na binamu zako.
Usipovaa Hijabu ya Kiislamu mbele ya watu waliotajwa ni dhambi na pia unaweza kusababisha mateso makubwa kwa mumeo, hata kama hatasema.
Mwanamke halazimiki kuvaa Hijabu kwa kiwango kile kile mbele ya baba mkwe, kaka yake, na watoto wa kiume wa kaka au dada yake, ingawa ni vema kwa kiwango fulani kuvaa Hijabu mbele ya watu hawa pia. Kwa usemi mwingine, wanawake wasionekane mbele ya watu hawa- ndugu zake- kama ambavyo anaweza kuvaa kwa kumvutia mumewe. Hii ni kwa sababu wanaume wengi sana hawapendi wake zao waonekane katika hali ya kuvutia kwa kuvaa nguo au urembo mbele ya wanaume wengine, na kama mambo yalivyo isisahaulike kwamba utulivu wa akili na imani ya mume kwa mke wake ni muhimu sana kwa kudumu na usalama wa familia yote.
Samehe Makosa Ya Mumeo
Kila mtu isipokuwa wale ambao Mwenyezi Mungu amewatangaza kuwa
‘Maasum’
hufanya makosa. Watu wawili wanaopendana na wanashirikiana pamoja, hufanya makosa, lazima wawe wasemehevu. Kama hawatasameheana, basi ndoa yao itavunjika.
Wafanya biashara wawili ambao ni wabia, na jirani wawili, marafiki wawili na hususan mume na mke wanahitaji kusameheana.
Kama watu wa familia hawasameheani na kufuatilia makosa ya kila mmoja wao, basi ama familia itafarakana au wataishi maisha yasiyovumilika.
Mpendwa Bibi! Pengine mumeo hufanya makosa. Anaweza akakutukana, akakufedhehesha, akasema uwongo, anaweza hata kukupiga. Matendo kama hayo yanaweza kufanywa na mwanamume yeyote.
Baada ya kufanya kosa, kama mumeo hujuta kwa kosa hilo au wewe unahisi anajuta kwa kosa lake hilo, basi msamehe na usilifuatilie jambo hilo. Kama anajuta lakini hayupo tayari kuomba msamaha, basi usijaribu kuthibitisha kosa lake. Vinginevyo, anaweza kuhisi anadhalilishwa na anaweza kulipiza kisasi kwa kukumbuka makosa yako na kwa hiyo, ikawa chanzo cha ugomvi mkubwa kwa hali hiyo, ni bora wewe unyamaze kimya hadi hapo atakapo jilaani mwenyewe kutoka kwenye dhamira yake na akaanza kuhisi majuto kuhusu kosa hilo. Hapo atakuona wewe kuwa ni mtu mwenye busara na mke wa kujitoa kwa mambo mema ambaye anavutiwa na mume wake, na familia yake.
Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: Mwanamke mbaya hatoi msamaha kwa makosa ya mumewe na hakubali hata kuomba msamaha.”
Je, si ni jambo la kusikitisha kwamba mkataba wa ndoa takatifu unavunjwa kwa sababu mwanamke hayupo tayari kusamehe makosa fulani ya muewe?
Kuweza Kuishi Na Ndugu Wa Mumeo
Mojawapo ya matatizo ya kifamilia husababishwa na ndugu wa mume na mke wake.
Baadhi ya wanawake hawana uhusiano mzuri na mama wa mumewe, dada au kaka zake mumewe.
Kwa upande moja mke anaweza kujaribu kumtawala mume wake ili asiweze kumsikiliza hata mama yake au ndugu yake yeyote na anaweza kujaribu kuwafitinisha ili wasielewane wao kwa wao. Kwa upande mwingine, mama wa mume anajiona kuwa yeye ni mmiliki wa mwanae na mke wa mwanae.
Mama hujaribu sana kuwa karibu sana na mwanae na kutahadhari kwamba mke wa mwanae asiweze kummiliki mumewe kwa ukamilifu. Anaweza kusingizia uwongo kuhusu mke wa mwanae au kumuona anayo makosa.
Msimamo wa aina hii unaweza kufuatwa na mabishano mengi na hata chuki ya mara kwa mara. Hali inakuwa mbaya zaidi endapo watu hawa huishi kwenye nyumba moja. Hata kama ugomvi unaweza kutokea baina ya wanawake wawili, uchungu wa kiakili na dhiki hasa zaidi humpata mume aliyoko kati yao.
Mume ananaswa katikati ya mabishano ambapo hawezi kuegemea upande wowote. Kwa upande moja yupo mke wake ambaye angependa kuendesha maisha ya kujitegemea bila kuingiliwa na mtu yeyote. Kwa kawaida mume huhisi lazima amsaidie mke wake na amfurahishe. Lakini kwa upande mwingine, anafikiria wazazi wake ambao wamemsaidia kuingia katika maisha, wamemsomesha na wametumia muda mwingi wa maisha yao kumlea.
Anahisi kwamba wazazi wake wanatarajia awasaidie wakati wanahitaji msaada na kwamba haitakuwa busara kuwasahau. Zaidi ya hayo, kama yeye mwenyewe anayo haja ya kupata kitu fulani, hatakwenda kwingineko isipokuwa kwa wazazi wake, ambao watamsaidia yeye na familia yake. Matokeo yake ni kwamba anatambua kwamba marafiki zake wakuaminika ni wazazi wake na ndugu zake. Kwa hiyo, mtanziko kwa mtu mwenye busara ni ama kuwa upande wa mke na kuwaacha wazazi au kinyume chake, lakini hapana lolote kati ya haya mambo mawili yanawezekana.
Matokeo yake, atalazimika kwenda na pande zote mbili na kuziweza pande hizi katika hali ya kuridhika ambayo ni kazi ngumu. Njia moja tu inayoweza kurahisisha hali ni kwamba mwanamke lazima awe mwaminifu na mwenye hekima. Katika hali kama hii, mume anatarajia mkewe amsaidie katika kutatua tatizo.
Kama mke anamheshimu mama mkwe wake, humtaka ampe ushauri wake, na anakuwa mtiifu na kufanya urafiki naye basi, mama mkwe wake atakuwa msaidizi wake mkubwa sana.
Je, si jambo la kusikitisha kuona mtu ambaye anaweza kuwavutia watu wengi kwa sababu ya wema wake na tabia zake, halafu awafukuze kwa ajili ya ukaidi na ubinafsi wake? Hutambui kwamba katika mazuri na mabaya ya maisha, mtu anaweza akahitaji msada wa wengine, na hususan ule wa ndugu ambao wanaweza kukusaidia ambapo kila mtu akiwa amekukimbia? Je, si ni jambo zuri zaidi kufurahia uhusiano mzuri na ndugu wa mtu kwa kutumia busara na tabia njema? Je, hivi kweli ni busara na haki kufanya urafiki na watu wengine ambapo unavunja uhusiano na ndugu zako?
Uzoefu unaonesha kwamba mtu anapotaka msaada kutoka kwa wengine, marafiki humkimbia lakini ndugu aliwo watupa huja kumsaidia. Hii ni kwa sababu mshikamano wa kifamilia unao asili na hauwezi kuvunjika kwa urahisi. Kuna methali isemayo: “Hata kama nyama ya mtu ingeliwa na ndugu zake, wasingeitupa mifupa yake”
Imam Ali (a.s) alisema: “Mtu hawezi kamwe kuishi bila kuwa na ndugu zake, hata kama ni tayari na anao watoto.”
Mtu atataka heshima na wema wa ndugu zake. Ni wao ndio watakao msaidia kimwili na kiakili. Ni ndugu ndio wanasaidia mara nyingi. Wakati wa shida ndugu huweza kusaidia haraka zaidi kuliko wengine. Yeyote anaye watupa ndugu zake hupoteza mikono mingi, ya kumsaidia.
Mpendwa Bibi! Kwa ajili ya mume wako na faraja yako mwenyewe na pia kutafuta marafiki wengi na wanao kuunga mkono, vumilia kuwa nao ndugu wa mumeo. Usiwe mbinafsi na mjinga; uwe na busara na usisababishe usumbufu wowote kwa mumeo. Uwe mke mzuri na mwenye kujitolea ili uweze kukubalika kwa Mwenyezi Mungu na watu.
Kuvumilia Kazi Ya Mume Wako
Kila mtu anayo kazi na kazi hutofautiana; mathalan, dereva ambaye muda mwingi zaidi yupo barabarani na anashindwa kurudi nyumbani kila siku usiku; polisi ambaye anatakiwa kuwa kwenye zamu baadhi ya muda wa usiku; daktari wa tiba ambaye ana muda mfupi wa kuwa na familia yake, mkufunzi au mwanasayansi ambaye husoma sana muda wa usiku; makanika ambaye nguo zake ni chafu na hunuka mafuta, mfanyakazi kiwandani ambaye hufanya kazi usiku. Kwa hiyo ni mara chache sana mtu kuwa na kazi ambazo hazisumbui kwa namna moja au nyingine na kusababisha kero kwa familia.
Hakuna njia nyingine yeyote ya kupata riziki kihalali isipokuwa kufanya kazi. Ni muhimu kwa wanaume kuvumulia matatizo ya kazi zao. Hata hivyo, kuna tatizo lingine ambalo ni malalamiko ya familia.
Kwa kawaida wanawake hupenda waume zao kuwa karibu nao na hupendelea wawepo nyumbani giza liingiapo. Wanawake hutaka waume zao kuwa na kazi nzuri yenye mshahara mnono. Wanapenda kuwa na muda wa kutosha wa kwenda matembezi ya jioni. Lakini bahati mbaya kazi za waume walio wengi, hazikidhi matamanio ya wake zao, na hii kwa baadhi ya familia ni chanzo cha ugomvi na mabishano.
Dereva ambaye amekuwa kazini kwa mausiku kadhaa, ambaye hajalala usingizi wa kutosha na amekuwa hapati chakula kwa wakati unaostahili, anaingia nyumbani kwake apumzike na apate amani na faraja akiwa na familia yake. Halafu mke wake, bila kumpa nafasi ya kupumzika hata kidogo, anaanza kupiga kite na kugumia: “maisha gani haya? Kwa nini unaniacha mimi na watoto hawa na ulikuwa wapi? Ninafanya kazi zote kwa sababu wewe haupo ambapo ungenisaidia. Nimechoshwa na hawa watoto watundu! Na kwa kweli udereva si kazi nzuri. Ama lazima ubadili kazi au tulizana na mimi hapa nyumbani. Siwezi kuishi namna hii zaidi ya hapa!”
Masikini dereva huyu ambaye anaye mke wa aina hii hawezi kutegemewa kufanya vizuri kazi yake na anaweza kuhatarisha maisha yake; na maisha ya hao anao wasafirisha.
Daktari ambaye tangu asubuhi hadi usiku, huwatembelea wagonjwa makumi kadhaa hawezi kuvumilia malalamiko ya mke wake. Daktari huyu ataweza kuendelea na kazi yake? Mfanya kazi ambaye hufanya kazi ya zamu ya usiku hawezi kufuatilia kazi yake kwa hamasa endapo mke wake ni mwanamke mjanja.
Mwanasayansi ataweza kufuzu katika eneo la taaluma yake ya utafiti endapo mke wake anamsumbua kila wakati?
Hii ni mitihani inayo wabainisha wanawake wenye busara na wale walio wajinga.
Mpendwa Bibi! Hatuwezi kuitengeneza dunia iwe vile tunavyotaka sisi, na mazingira yaliyopo. Mume wako anahitaji kazi ili aweze kupata riziki halali kwa ajili ya familia yake. Kazi yake inayo masharti ambayo yatakufanya ubadilike ili uendane nayo. Lazima upange utaratibu wa maisha ya familia yako kufuatana na kazi yake. Kwa nini ulalamike na umuone anayo makosa kwa sababu ya kazi yake? Mkaribishe nyumbani kwa uso wenye furaha na uwe mwema kwake. Uwe na hekima na uivumilie kazi yake.
Kama mume wako ni dereva ambaye muda mwingi yupo barabarani, basi, tambua kwamba anajaribu kuleta fedha nyumbani kwa ajili yako na watoto. Kazi yake si tatizo. Yeye ni sehemu ya jamii na anaihudumia kwa namna nzuri kadiri awezavyo. Ingekuwa bora kama angekuwa mvivu au kama angekuwa anafanya kazi isiyoendana na masharti ya dini? Kwa hiyo, yeye hana ubaya wowote. Kasoro ipo kwako, unatarajia awepo nyumbani kila siku usiku na wewe unashindwa au hutaki kubadilika kufuatana na hali iliyipo sasa.
Hivi si busara kuzoea hali ya wakati uliopo na kuishi kwa raha zaidi? Si ingekuwa bora zaidi kumkaribisha mumeo kwa uso wenye tabasamu na kumshawishi aendelee na kazi yake kwa kumpa ‘kwa heri’ ya kuchangamsha anapoondoka nyumbani kwenda kwenye kazi yake? Kama ukimfanyia wema, atazidi kuvutiwa na familia yake na anaweza kuzidisha bidii kwenye kazi yake.
Hata farakana na wewe; atarudi nyumbani mapema kadiri iwezekanavyo; atajitahidi asifanye ajali na atakuwa imara kushikilia maadili mema.
Kama mume wako anafanya kazi ya zamu ya usiku, anakosa usingizi mzuri wa usiku ili aweze kumudu matumizi ya familia yake. Jaribu kuzoea hali hii na usioneshe kutokuridhika kwako. Kama unachoshwa na upweke, unaweza kufanya baadhi ya kazi za nyumbani, kushona na kusoma wakati wa usiku. Asubuhi tayarisha kifungua kinywa, mume wako anaporudi kutoka kwenye kazi, halafu tandika kitanda mahali penye kimya. Wanyamazishe watoto wawe kimya na uwafundishe wasimsumbue baba yao wakati anapumzika. Unaweza hata kulala nusu usingizi ili uweze kupumzika na mume wako wakati wa mchana. Lakini usisahau kwamba amekuwa macho usiku kucha na usingizi wake wa mchana ni sawa na usingizi wako wa usiku. Wanawake waliopo kwenye hali kama hii wanatakiwa kuwa na mipango ya aina mbili, moja wa kwao na mwingine wa waume zao.
Kama mume wako ni dereva, dakitari, mfanya kazi au bingwa wa sayansi na kadhalika, basi lazima ujivune na sababu ya kuwa naye. Mume wako si mvivu, mzururaji au hafanyi kazi isiyo afikiana na mafundisho ya dini. Kwa hiyo, umthamini na kumshukuru.
Usimtarajie yeye au kumuambia aache kazi yake, lakini jaribu kuafikiana na kazi aliyonayo. Kama anasoma au anatafiti katika eneo fulani, basi usimsumbue. Wewe unaweza kufanya kazi ya nyumbani soma kitabu au kwa ruhusa yake, nenda uwatembelee marafiki au ndugu.
Lakini, wakati anapumzika, jaribu kuwepo nyumbani. Tayarisha chakula chake na mahitaji mengine. Mpokee mume wako kwa tabasamu na tabia njema. Kwa kuonesha wema wako na kwa kumfurahisha, unaweza kumfanya asahau uchovu wake. Kama wewe ni mke mzuri, basi si tu kwamba utaharakisha kupandishwa kwake cheo, lakini unatoa mchango kwa huduma zake kwa jamii.
Si wanawake wote wanastahiki wanamume wenye bidii kama hao. Kwa hiyo, kwa kuwa na tabia njema na mwenye kujitolea, thibitisha kwamba na wewe unastahiki kuwa naye.
Kama kazi ya mume wako inamtaka avae nguo rasmi ambazo huchafuka, basi zifue nguo hizo mara kwa mara.
Usilalamike na usimwambie mambo yasiyofaa kwa sababu ya kazi yake. Usimwambie abadili kazi. Kuna ubaya gani kuwa makenika? Kwa vyovyote vile, hili si jambo la umuhimu na familia zisivunjike kwa sababu hii.
“Mwanamke alimwambia jaji mahakamani kwamba kazi ya mume wake, ilikuwa kuuza mafuta ya taa na kwa hiyo kila mara alikuwa ananuka vibaya na kwa hiyo alichoshwa na hali hiyo.”

Comments
Post a Comment