Seneta wa upinzani ajitangaza kuwa Rais Bolivia
Seneta wa chama cha upinzani nchini Bolivia, Jeanine Áñez amejitangaza kuwa Rais wa taifa hilo kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais, Evo Morales.
Hata hivyo, amepata upinzani mkali kwa hatua aliyoichukua. Wabunge kutoka katika chama cha Morales walisusia bunge na rais huyo wa zamani alitangaza alichokifanya Anez kama mapinduzi ya Serikali.
Morales amekimbilia nchini Mexico ambako amedai aliomba hifadhi kwakuwa maisha yake yalikuwa hatarini.
Rais huyo wa zamani alijiuzulu nafasi ya Urais Jumapili iliyopita ikiwa ni wiki kadhaa tangu yazuke maandamano makubwa ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu. Alisema kuwa aliamua kujiuzulu mwenyewe ili kuepusha damu kumwagika.
Jana, upande wa Anez ulidhibiti bunge na kumpitisha kuchukua nafasi ya urais kwa kipindi cha mpito. Hatua hiyo ilipingwa vikali na wabunge wanaomuunga mkono Morales ambao hadi leo wamekuwa wakipinga.

Comments
Post a Comment