Wanawake Wenye Dhana
Si vibaya mwanamke kuwa na tahadhari kuhusu mume wake, lakini ni pale tu ambapo haitavuka kiwango cha dhana na kutokuaminiana. Dhana ni maradhi yenye uharibifu na yasiotibika. Bahati mbaya baadhi ya wanawake huathiriwa na ugonjwa huu (wa dhana).
Mwanamke mwenye dhana hudhania kwamba mume wake, hawi mwaminifu kwake kihalali au isivyo halali. Anadhani kwamba ameoa mke mwingine au anataka kuoa mke mwingine. Mke anatuhumu kwamba mume wake anao uhusiano wa kimapenzi na katibu mukhtasi wake au mwanamke mwingine. Hupoteza imani kwake kwa sababu huchelewa kurudi nyumbani au alionekana anaongea na mwanamke.
Endapo atamsaidia mjane na watoto wake, mke anaweza kufikiria kwamba mume wake anavutiwa na mwanamke huyo, na si tendo la msaada.
Kama mwanamke yeyote anampongeza mume wake, kwa kumwambia kwamba sura yake inapendeza au tabia yake ni njema, anamalizia kwa kusema kwamba yeye anavutiwa na mwanamke huyo. Kwa kuona unywele wa mwanamke ndani ya gari yake, mke anadhani yupo mwanamke mwingine katika maisha yake. Wanawake wa aina hii wenye fikira kama hizi na uthibitisho usio kamili, polepole kimakosa hupata uhakika kuhusu waume zao kutokuwa na uaminifu.
Huwaza kuhusu suala hili usiku na mchana.
Pia huwaambia wengine, marafiki, na maaadui kuhusu suala hili; ambao kwa jina la huruma, wanaongezea nguvu shutuma zao na kuanza kuwaambia wanawake wahusika habari za wanaume wengine wasio waaminifu.
Ubishi na ugomvi huanza kutokeza. Mwanamke huanza kudharau mambo ya nyumbani na watoto na anaweza hata kwenda kwa wazazi wake.
Atamfuatilia na kupekua mifuko yake. Atasoma barua zake na ataelezea kila jambo dogo kuwa ni kwa sababu ya yeye kutokuwa mwaminifu.
Kwa msimamo huu, atayafanya maisha ya familia kuwa magumu na kuigeuza nyumba kuwa jahanamu iwakayo moto na ambamo yeye pia atateseka. Kama mume wake angeleta uthibitisho wa yeye kutokuwa na hatia au kuapa kwamba hajafanya jambo lolote baya, au alie, bado hataridhika.
Msomaji bila shaka amekwisha waona wanawake wa aina hii, lakini inafaa kujua mifano ifuatayo:
“Mwanamke alisema kwenye mahakama: “msishangae kwa nini nimeamua kutengana na mume wangu baada ya maisha ya ndoa ya miaka kumi na mbili na watoto wadogo watatu. Sasa ninao uhakika kwamba mume wangu si mwaminifu kwangu. Siku chache zilizopita nilimwona anatembea mtaani na mwanamke wa kuvutia. Nikasoma gazeti la kila wiki lenye ukurasa wa utabiri wa nyota.
Kila wiki, utabiri wa nyota ya mume wangu unasema kwamba angefurahia maisha na watu waliozaliwa mwezi wa juni. Mimi nimezaliwa mwezi wa Februari; Kwa hiyo mimi si mmojawapo wa watu waliotajwa kwenye utabiri. Zaidi ya hayo ninahisi mume wangu hanipendi kama alivyokuwa ananipenda zamani.”
Mume wa mwanamke huyu akasema: “Tafadhali niambie nifanye nini. Ningependa magazeti haya yangewafikiria wasomaji kama mke wangu, na hayangesema uwongo mwingi sana. Naomba kuaminiwa ninaposema kwamba huu utabiri wa nyota umeyafanya maisha yangu na yale ya watoto wangu kuharibika. Kama mojawapo ya utabiri huu unasema kwamba wiki hii nitapata kiasi kikubwa cha fedha halafu mke wangu huja kwangu na kuniuliza fedha nilizopata nimezifanyia nini? Au endapo utabiri wa nyota unasema kwamba ningepokea barua, basi Mwenyezi Mungu na anikoe! nadhani labda ni vizuri zaidi tutengane kwa sababu mke wangu hataki kukabiliana na ukweli.”
Mwanaume alisema mahakamani: “Ilikuwa mwezi uliopita nilipokuwa narudi kutoka kwenye karamu, mfanya kazi mwenzangu aliniomba nimpe lifti yeye na mke wake hadi nyumbani kwao. Siku moja mke wangu aliniomba nimnpeleke kwa wazazi wake. Wakati tupo njiani, mke wangu alipotazama nyumba ya gari akaona unywele wa mwanamke kwenye kiti cha nyuma. Akauliza unywele huo ulikuwa wa nani. Nilihangaika na sikuweza kumpa maelezo yanayo faa. Nilimfikisha nyumbani kwa wazazi wake na mimi nilikwenda kwenye kazi yangu. Nilipokwenda kumchukua usiku huo akakataa kuondoka na mimi. Nilimuuliza kwa nini? Aliniambia kwamba afadhali niendelee kuishi na mwenye huo unywele.”
Mwanamke mwenye umri mdogo alilalamika mahakamani na akasema: “mume wangu huchelewa kurudi nyumbani kila siku usiku kwa sababu ya kufanya kazi saa za ziada.
Nina wasi wasi kuhusu hili na tuhuma yangu imeongezeka kwa sababu ya hayo yanayo semwa na majirani zetu. Wanasema kwamba mume wangu anadanganya na hafanyi kazi usiku na kwamba huenda kwenye starehe zake.
Matokeo yake ni kwamba sipo tayari kuishi na mwongo.”
Katika nukta hii, mume alichukua barua chache kutoka mfukoni mwake na akaziweka kwenye kaunta mbele ya jaji na akamwomba azisome ili athibitishe kwamba yeye hana hatia na kumsitisha mkewe asiendelee na msimamo usiofaa.
“Jaji alianza kusoma barua kwa sauti. Mojawapo ya barua hizo ilionesha kwamba yeye hufanya kazi saa za ziada kuanzia saa 10 hadi 2 usiku. Barua nyingine pia zilihusiana na kazi yake ambapo aliombwa kuhudhuria semina fulani.
Mke wake alikuja mbele na baada ya kuona barua hizo alisema; “Nilikuwa nikipekua mifuko yake lakini zikuziona barua hizi.”
Jaji alisema; “Inawezekana aliziacha ofisini kwake.”
Mume akasema: “Tuhuma ya mke wangu kwangu imekuwa kubwa mno hivyo kwamba ninamtuhumu yeye. Kila siku usiku ninapatwa na majinamizi, ninadhani kwamba mke wangu anaye bwana mwingine na anataka tutengane ili akaolewe na bwana huyo.”
Kufikia hapo, mke alimkimbilia mume wake kwa haraka huku analia kwa furaha, alimwomba msamaha na wote wakaondoka mahakamani.
Mtaalamu wa meno alilalamika mahakamani na kusema: “Mke wangu ana wivu kupita kiasi. Mimi ni mtaalamu wa tiba ya meno na wapo wagonjwa wanawake ambao huja ofisini kwangu kwa ajili ya matibabu. Hali hii imeamsha wivu wa mke wangu na kila siku tunabishana kuhusu jambo hili. Mke wangu anaamini kwamba nisingewatibu wagonjwa wanawake. Lakini haiwezekani mimi nipoteze wateja wangu na yeye ananipenda mimi, lakini matumani yake yasio na maana yanaharibu maisha yetu.
Siku chache zilizopita alikuja kwenye chumba changu cha upasuaji na akanilazimisha tuondoke.
Tulikwenda na tukagombana. Aliniambia: ‘Nilikwenda kwenye chumba chako cha upasuaji na nikaketi karibu na msichana mdogo kwenye chumba cha wanaosubiri. Mimi na msichana huyu tukazungumza kuhusu wewe bila kujua kwamba mimi ni mke wake, alisema; Huyu bwana mganga wa meno ana sura nzuri na anatabia njema.” ’
Mganga wa meno aliendelea kusema: “Kwa sababu ya maoni ya msichana, mke wangu aliniburuza nje ya sehemu yangu ya kazi kwa njia ya kunivunjia heshima.”
Mwanamke alilalamika mahakamani na alisema: “Mmojawapo wa marafiki zangu aliniambia kwamba mume wangu huenda kwenye nyumba ya wageni wanawake. Siku moja nilimfuata na kugundua kwamba ilikuwa kweli. Sasa nataka mahakama imwadhibu.” Mume katika kukubali yale yaliyosemwa na mke wake, aliiambia mahakama: “Siku moja nilikwenda kwenye duka la dawa kununua dawa. Nilimuona mwanamke humo kwenye duka la madawa ananunua maziwa ya unga. hakuwa na fedha ya kutosha kununua maziwa, kwa hiyo nikajitolea kumsaidia. Baadaye nilitambua kwamba ni mjane ambaye alikuwa masikini. Kwa hiyo niliamua kuendeleza msaada wangu.” Majaji walitambua ukweli baada ya kuchunguza jambo hili na wakawasuluhisha wanandoa.”
Matukio kama haya hutokea kwenye familia nyingi. Hali ya familia hubadilika na huwa na mazingira ya kutazamia taabu tuhuma na uadui.
Watoto watapata mateso na athari za kisaikolojia ni mbaya sana.
Kama wanandoa wanaendelea katika hali hii, basi wote watateseka na wakioneshana kiburi, hakika wataelekea kutalikiana.
Inapotokea kutalikiana, wote wawili mume na mke watahasarika, kwa sababu kwa upande moja mume hatawaza kupata mke mwingine ambaye atakuwa bora zaidi kuliko wa kwanza. Kwa upande mwingine, watoto watateseka na hawatafurahia maisha mazuri. Watoto wanaweza hata kupata matatizo mapya kwa sababu ya baba wa kambo au mama wa kambo.
Mwanamume anaweza kudhani kwamba kwa kumtaliki mke wake, anaweza akamuoa mke, ‘bora’ ambaye ataishi naye kwa amani. Lakini hii ni ndoto tu na kuitambua ni vigumu sana. Kwa kumtaliki mke wake, anaweza akakutana na matatizo mapya kutoka kwa mke mpya.
Kutalikiana si njia ya kuielekea kwenye faraja na furaha kwa mwanamke. Licha ya kwamba anaweza kuhisi kwamba amelipiza kisasi, kuolewa tena haitakuwa rahisi kwake. Anaweza kuishi peke yake katika maisha yake yote na labda hatafurahia hata kuwa nao watoto wake. Hata kama ataolewa tena, hakuna uhakika kwamba mume wake mpya atakubaliana na matarajio yake. Anaweza hata akajikuta analea watoto wa mume wa mke aliyefariki. kwa hiyo wala si talaka ama ubishi na ugomvi vinaweza kuwaokoa wanandoa. Lakini ipo njia inayoweza kuwakomboa.
Msimamo mzuri kushinda yote ni kwamba mwanamume na mke wake wanaacha kubishana na kujaribu kuwa na mantiki. Wanamume wanayo wajibu mkubwa zaidi katika jambo hili na kwa kweli ufunguo wa suluhu upo mikononi mwao. Kwa kufuatia uvumilivu na usamehevu, wanaume wanaweza kujiokoa kutoka kwenye matatizo na pia kusaidia kuondoa kabisa dalili za tuhuma kwa wake zao.
Sasa maneno machache kwa wanaume:
Kwanza, mpendwa bwana! Lazima ukumbuke kwamba mkeo hata kama anakutuhumu, anakupenda. Anavutiwa sana na watoto wako na nyumba yenye familia.
Anaogopa kutengana. Kwa hakika atateseka kwa sababu ya hali yako ya maisha ya kusikitisha. Kama angekuwa hakupendi, hangekuonea wivu. Kwa hiyo mkeo hapendezwi na hali ya sasa, lakini atafanya nini endapo yeye ni mgonjwa? Wagonjwa wengine wanayo maradhi ya baridi yabisi na wengine wanaugua saratani. Mke wako anaumwa maradhi ya kuvurugikiwa na akili na kama huamini, basi mpeleke kwa mtaalamu wa maradhi ya akili. Unatakiwa kuwa na huruma na mpole. Usimkasirikie au kubishana na mkeo. Hapana mtu anayeweza kugombana na mtu mgonjwa. Usiwe mkali kwa ajili ya matendo yake yasio na adabu au madai. Usiishie kupigana naye.
Usimpeleke kwenye mahakama yoyote. Usimdharau. Usizungumze habari ya talaka au kutengana. Baina ya matendo haya, hakuna mojawapo linaweza kutibu maradhi yake, kwa kweli maradhi hayo yanaweza kuwa mabaya zaidi. Kutokuwa mwema kwake inaweza kuwa chanzo cha tuhuma yake.
Lazima uwe mwema kwa mkeo kadiri iwezekanavyo. Unaweza kumkasirikia mkeo sana kwa sababu ya msimamo wake, lakini hakuna njia nyingine yoyote. Lazima umtendee kwa namna hivyo kwamba anakuwa na uhakika wa wewe kutokuwa na hatia.
Pili, unatakiwa kujaribu kutengeneza uelewano baina yenu. Usimfiche kitu chochote. Mruhusu asome barua zako hata kabla wewe hujasoma. Usifiche funguo za meza yako ya faragha au sefu, Mruhusu apekue mabegi na mifuko yako. Mruhusu akufuatilie. Usioneshe kutokufurahishwa na mambo yaliyotajwa hapo juu, lakini yafikirie kama utaratibu wa kawaida katika maisha ya familia iliyo imara na kuelewana.
Baada ya kazi, kama hauna shughuli nyingine, rudi nyumbani haraka iwezekanavyo. kama jambo la haraka linajitokeza ambalo linahitaji kushughulukiwa, basi mwambie mkeo na mjulishe unakokwenda na wakati ambao atakutarajia kurudi nyumbani. Halafu jaribu kurudi muda huo. Endapo unachelewa kurudi nyumbani, basi haraka mwambioe mkeo sababu ya kukuchelewesha.
Uwe mwangalifu, usidanganye, vinginevyo ataanza kukutuhumu. Omba ushauri wake kuhusu mambo yako. Usimfiche kitu chochote. Mpe uhuru wa kukuuliza kuhusu suala lolote lisiloeleweka na kumtatiza yeye.
Tatu, wewe unaweza kuwa huna hatia ya jambo ambalo anakutuhumu, lakini pia tuhuma za wanawake zilizo nyingi si kwamba hazina uthibitisho. Labda, kwa kutokuwa mwangalifu umefanya jambo ambalo limemwathiri kiakili na kumfanya akutuhumu. Lazima utafakari kwa uangalifu kuhusu matendo yako ya nyuma. Inawezekana ukatambua sababu ya tuhuma yake. Kwa njia hii unaweza kutatua tatizo vizuri zaidi. Mathalani, kama wewe unataniana sana na wanawake wengine, jaribu kusitisha tabia hiyo kabisa.
Kuna umuhimu gani wewe kusifiwa kuwa unayo sura nzuri na tabia njema kwa hasara ya kutuhumiwa na mkeo na kutokukuamini? Kwa nini uchokoze tuhuma ya mke wako kwa kutaniana na katibu muhtasi wako au mfanyakazi mwenzako mwanamke? Kwa nini umwajiri mwanamke? Usitaniane na wanawake wengine, kwenye karamu.
Kama unataka kumsaidia mwanamke mjane, kwa nini usimjulieshe mke wako? Unaweza hata kumsaidia mjane kupitia kwa mke wako. Usijifikirie kwamba wewe ni mtumwa, au mtu aliyefungwa minyororo. Hutakiwi kuwa mtumwa, lakini mwanamume mwenye busara baada ya kufanya mkataba na mke wake, ana mtunza. Unatakiwa umsaidie aondokane na tatizo hili. Kwa uvumilivu na busara, unatakiwa uondoe hatari zinazo tishia msingi wa maisha safi ya familia yenu. Hapo utakuwa umetibu maradhi ya mke wako na kuwaokoa watoto wenu kutoka kwenye huzuni. Utakuwa umetoa huduma kubwa kwako kiakili na kimwili. Zaidi ya haya, Mwenyezi Mungu huwapa thawabu wanamume ambao wapo tayari kujitoa mhanga kwa nyakati muhimu kama hizi.
Imamu Ali (a.s) alisema: “Kila wakati wafanyieni wanawake wastani katika mambo yenu. Semeni nao kwa wema ili matendo yao yawe mazuri”
Imamu Sajjad (a.s) alisema: “Mojawapo ya haki za mwanamke kwa mume wake ni kwamba mume anatakiwa kusamehe ujinga na upumbavu wa mkewe (na kinyme chake).”
Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: “Mwanamume yeyote anayeweza kuvumilia upungufu wa mkewe, kwa uvumilivu wake (kwa mke wake) wa kila mara, Mwenyezi Mungu Mweza wa yote, atampa thawabu za uvumilivu wa Hadhrat Ayub (a.s)”
Sasa wanawake wanakumbushwa kuhusu mambo machache:
Kwanza: Mpendwa Bibi! Suala la mume wako kutokuwa mwaminifu, kama masuala mengine yoyote, linahitaji kuthibitishwa.
Almuradi hajathibutishwa kuwa anahatia, huna haki ya kumtia hatiani. Wala si sheria ama dhamira ya mtu humruhusu mtu kumshtaki mtu kwa sababu ya welekeo wa uhalifu kufanyika. Wewe hungehisi uchungu kama mtu angekushtaki kuhusu kitu fulani bila ya uthibitisho wowote? Inawezekana kufikiria nadharia zako za kipumbavu na zisizo na msingi kama ndio uthibitisho wa uhalifu mkubwa kama zinaa?
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ {12}
“Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani baadhi ya dhana ni dhambi…” (Quran 49:12).
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Uzito wa kumshitaki mtu asiye na hatia kwa kumsingizia ni mzito zaidi ya milima mirefu.”
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Uzito wa kumshitaki mtu asiye na hatia kwa kumsingizia ni mzito zaidi ya milima mirefu.”
Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Mtu yeyote anayemshitaki muumini kwa kumsingizia, Mwenyezi Mungu, siku ya Ufufuo atamweka kwenye lundo la moto ili apate adhabu anayostahili.”
Mpendwa Bibi! Usiwe mpumbavu na usifanye haraka kuamua mambo. Unapokuwa na wakati, keti na andika uthibitisho wote na hoja kuhusu mumeo kuvunja uaminifu kwako. Halafu mbele ya kila jambo, andika vipengele vingine kwenye tatizo hilo na uwezekano wa mambo hayo kujitokeza tena. Kitakachofuata, jiweke wewe katika nafsi ya jaji na utafakari kwa undani sana kuhusu mambo yaliyoandikwa. Kama hazikushawishi kwamba ana hatia, basi ama unaweza kusahau jambo hilo au ufanye uchunguzi zaidi.
Mathalani kuwepo kwa unywele wa mwanamke kwenye gari ya mume wako ni jambo ambalo linaweza kuelezeka kwa urahisi kwa mojawapo ya haya yafuatayo: Unywele huo unaweza kuwa ni wa mmojawapo wa ndugu za mumeo kama vile dada yake, mama yake, changazi yake au watoto wao.
Unywele huo unaweza kuwa ni wako.
Inawezekana alimpa lifti rafiki au ndugu yake akiwa na mke wake na unywele huo ukawa ni wake.
Inawezekana alimpa lifti mwanamke ambaye alikuwa hajiwezi.
Inawezekana mmojawapo wa maadui zake ameangusha unywele huo kwenye gari lake kwa makusudi ili kukufanya wewe uwe na wasiwasi na mumeo.
Inawezekana aliyempa lifti ni mmojawapo wa wafanyakazi wanawake kwenye gari lake.
Pia uwezekano upo kwamba alitoka nje kimatembezi na hawara yake. Lakini mfano huo upo mbali mno kuliko ile iliyo tangulia kwa hiyo si wa kuzingatiwa sana. Si lazima mtu aufikirie kama ushahidi madhubuti wa kumtia mtu hatiani wakati ambapo anasahau uwezekano mwingine katika orodha hiyo hapo juu.
Kama mumeo anachelewa anarudi nyumbani, inawezekana alikuwa anafanya kazi za ziada; au labda alikuwa nyumbani kwa rafiki yake; au alikuwa anahudhuria semina au mkutano wa kidini; au inawezekana alitembea kwa miguu kurudi nyumbani.
Kama mwanamke anamuona mumeo kuwa ana sura ya kuvutia, hilo si kosa la mumeo. Kuwa na tabia njema si uthibitiosho wa kuwa na hatia!
Je, ungependa mumeo kuwa mtu mkali na kukimbiwa na kila mtu?
Kama mume wako anamhudumia mjane na watoto wake, mfikirie kuwa ni mtu mwenye kupenda kusaidia ambaye anafanya hili kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Kama mume wako anayo meza ya faragha au sefu nyumbani; na kama hakuruhusu kusoma barua zake usimfikirie kuwa anaye kimada. Kwa kawaida wanamume wanayo tabia ya usiri na wastani. Hawapendi watu wengine wajue mambo yao, labda wanayo mambo ya siri yahusuyo kazi zao. Labda hakuona wewe kama mtu unayeweza kuweka siri. Kwa vyovyote vile, uwezekano ni huo tu na usifikirie kuwa uthibitisho madhubuti.
Pili: Wakati wowote unapodhania jambo lolote ni lazima ulizungumze na mume wako kwa namna ambayo utapata ukweli wa jambo lenyewe, na si kwa njia ya ugomvi. Uwe muwazi kwake na muombe akueleze kuhusu suala la dhana yako ili usafishe moyo wako na utulie katika amani. Halafu msikilize kwa uangalifu. Tafakari kuhusu maelezo yake. Kama unaridhika nayo basi jambo hilo liishe.
Lakini kama bado una wasi wasi, basi chunguza jambo hilo wewe mwenyewe hadi ukweli ujulikane. Kama wakati wa kupeleleza unapata kipengele ambacho mumeo alidanganya, basi usikifikirie kama ndio uthibitisho wa kuwa na hatia. Hii ni kwa sababu licha ya kuwa hana hatia, inawezekana kwa makusudi alikuwa hasemi kweli ili usije ukawa na wasi wasi zaidi. Tena ni bora zaidi kumwendea na kumhoji kwa nini hakusema kweli yote. Kama mambo yalivyo, si vema mtu kudanganya, lakini mumeo alifanya kosa hili, basi wewe usifanye upumbavu. Muulize kwa ushupavu akwambie ukweli.
Kushindwa kwake kukueleza kuhusu suala la tuhuma yako si dalili ya yeye kuwa na hatia. Inawezekana kwamba kwa hakika anaweza kusahau jambo au anaweza kuwa amehangaika. Wakati huu, usiendelee kufuatilia jambo hili tena na liache hadi wakati mwingine unaofaa. Akikwambia kwamba amesahau kitu fulani, kubali. Hata hivyo, kama bado unayo mashaka, fanya upelelezi kupitia njia nyingine.
Tatu: Usimwambie kila mtu unayemuona dhana yako kwa mumeo, kwani wanaweza kuwa maadui zako. Maadui mara nyingi huthibitisha madai yako na wanaweza hata kuongeza uwongo juu yako ili waharibu maisha yako.
Wanaweza kuwa si maadui, lakini kundi la watu wapumbavu wenye kuvutiwa kiakili kwa rahisi na watu wasiokuwa na uzoefu ambao wataimarisha madai yako kwa namna ya kukuhurumia. Watu hawa wanaweza kuwa ni ndugu zako au marafiki zako wa karibu. Ushauri unaofaa unatakiwa kutolewa na watu wenye busara, werevu na wenye huruma halisi. kama unataka kupata ushauri, basi waendee watu wanao stahiki na uwazungumzie jambo hili.
Nne: Kama ushahidi wa hatia ya mume wako si madhubuti; kama marafiki zako na ndugu zako wanadhani kwamba ushahidi huo hautoshi, endapo mume wako anajihisi kwamba hana hatia na hatimaye kama bado unamtuhumu, basi uwe na uhakika wewe unayo maradhi. Maradhi hayo ni kuvurugika kwa akili ambamo dalili za tuhuma zimeongezeka na kushindwa kuzidhibiti. Ni muhimu uende umuone mtaalamu wa magonjwa ya akili ambaye atakutibu ipasavyo.
Tano: Kwa hiyo, si busara wewe kubishana na mume wako au kupeleka malalamiko mahakamani. Usizungumze kuhusu talaka na usimshushe hadhi yake. Msimamo wa aina hiyo unaweza tu kuongeza hasira zaidi na ugomvi ambao unaweza kusababisha kuachana. Uwe mwangalifu usifanye mambo kipumbavu au kuamua kujiua. Kujiua mwenyewe si tu kwamba utapoteza maisha, lakini pia utaadhibiwa huko akhera.
Je, si jambo la kusikitisha kupoteza maisha yako kwa sababu ya fikra isiyo na msingi? Je, si vema kutatua matatizo yako kwa uvumilivu na busara?
Sita: Kama bado unamdhania mume wako au una hitimisha kwamba kwa hakika anaye mpenzi nje ya ndoa, bado wewe unalaumiwa, kwa sababu hujajaribu vya kutosha kuvuta moyo wake. Unaweka ufa katika maisha yake ambapo wanawake wengine wanaweza kuona ni mahali pa wazi na wakakaa hapo. Lakini, usikate tamaa; bado muda upo. Angalia upya msimamo wako na fanya mambo yako kwa namna ya kumvuta mume kwako.
Usisikileze mazungumzo ya uwongo
Mojawapo ya tabia hasi ya watu wengine ni kuwasema wengine kwa ubaya. Tabia hii si tu ni mbaya kwa jinsi ilivyo, lakini pia ni chanzo cha fitina. Husababisha dhana, kukosa rajua (kushutumu kila kitu), kutotangamana na migongano miongoni mwa watu. Huharibu mazingira ya kirafiki na kupanda mbegu ya kutokuelewana miongoni mwa familia. Huwatenganisha wanamume kutoka kwa wake zao na inaweza kusababisha mauaji.
Kwa bahati mbaya tabia hii imeenea miongoni mwa watu hivyo kwamba haionekani kuwa ni mbaya tena. Kwenye mkutano utawaona watu wanateta na kusengenya. Hususan kwenye mkutano wa wanawake, ishara za kuteta huwa zimejazana. Wanawake wawili wakikutana, huanza kuteta. Wanawasengenya wenzao kama vile ni mashindano. Wakati mwingine huwasema waume zao. Mathalani wanawasema jinsi waonekanavyo au kazi zao, na kuona dosari za mume wa nwanamke mwingine. Mwanamke mmoja anaweza kumlaumu mwenzake kwa kuolewa na makenika au fundi viatu. Kama mume ni dereva atasema; “Mumeo kila mara yupo safarini, unawezaje kuvumilia hali hiyo? Kama mume anauza nyama, atasema mumeo kila mara hunuka mafuta.”
Kama mume hana kipato cha kutosha, atasema; “Unaishi vipi kwa fedha ndogo kiasi hicho? Kwanini uliolewa naye? Si inasikitisha kwamba wewe na uzuri wote huo umeolewa na mtu mfupi na dhalili kama huyo? Wazazi wako walikuruhusu vipi kufanya hivi? Walichoka kuishi na wewe? Ungeweza kuolewa na mwanamume yeyote ambaye ungemtaka. Kwa nini ulimchagua mwanammume huyu? Hakupeleki mahali popote, hakupeleki sinema, popote.
Pamoja na hayo mumeo ni mtu mwenye uso wa kuotisha. Unawezaje kuishi naye? Ni vipi wewe, na elimu yako, ulikubali kuolewa na mkulima?”
Mazungumzo ya aina hii yanaweza kusikika katika asiliamia kubwa miongoni mwa vichimbakazi wa kike katika jamii yoyote. Wanawake wenye mazoea ya namna ya kuzungumza, kwa kweli, hawafikirii kuhusu matokeo mabaya sana yanayofuata baadaye. Hawafikiri kwamba kuteta kwao na kutafuta na kuona makosa ya watu ni tabia inayoweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa au hata mauaji.
Wanawake wa aina hii kwa kweli ni mashetani katika umbo la binadamu. Wao ni maadui wa familia. Hutengeneza migongano miongoni mwa familia na kuzibadili nyumba zao kuwa gereza la chini ya ardhi lenye giza na kutisha. Mtu anaweza kufanya nini? Hii ni sehemu ya jamii zetu. Licha ya kwamba Uislamu umetukataza kabisa kufanya vitendo kama hivi, hatupo tayari kuacha.
Mtume (s.a.w.w) alisema: “Enyi watu mnaodai kuwa ni Waislamu, lakini mlishindwa kuiruhusu imani iingie kwenye nyoyo zenu, msiwaseme Waislamu kwa ubaya na msitafute dosari zao.
Yeyote anayetafuta mapungufu ya watu, basi Mwenyezi Mungu Mweza wa yote atakuwa anafanya kama anavyofanya mtu huyo kwa wengine; na katika hali ile watafedheheshwa miongoni mwa watu, licha ya kuwa watakuwa majumbani mwao.”
Wanawake wenye tabia mbovu wanaweza kuwa wanafuatilia lengo moja au mengi. Wanateta kwa ajili ya kulipiza kisasi ili wavunje familia. Wanaweza wakafanya hivyo kwa sababu ya husuda au kujifaharisha wenyewe. Pengine walitaka kuficha upungufu wao wenyewe au kuwadanganya wanawake walio wepesi kudanganywa. Wanaweza kujifanya kuwa wanahuruma. Wakati mwingine wanateta kwa sababu ya kujifurahisha na hawafuatilii lengo lolote zaidi ya kuridhisha matamanio yao ya kuchukiza. Lakini mtu anachoweza kuwa na uhakika nacho ni kwamba matendo ya aina hii hayafanywi kwa lengo la kuwasaidia wengine na kwamba matendo kama haya yanaweza kusababisha athari za maangamizi.
Wasomaji kwa hakika wamekutana na matuko fulani ambayo yametokea kutokana na utesi. Ufuatao ni mfano wa matukio hayo: “Mwanamke alisema mahakamani: “Bwana… alikuwa na tabia ya kumteta mume wangu kwa lengo la kusababisha ugomvi baina yangu na mume wangu. Alikuwa akiniambia kwamba mume wangu hakuwa mtu mzuri vya kutosha na kwamba hakunielewa mimi au sikuwa na mshtuko wowote. Kila mara alitaka mimi nipewe talaka na niolewe na yeye…. matokeo ya ushauri wake wa udanganyifu nilipotoshwa na siku moja mimi na yeye tulimuua mume wangu.”
Bibi mpendwa! Sasa umetambua nia mbaya zilizojificha kwenye usengenyaji na kama unampenda mume na watoto wako, basi usije ukavutiwa na ndimi za mashetani yenye umbo la binadamu. Usikubali urafiki wao wa udanganyifu. Hakikisha wao si marafiki zako, ila ni maadui zako ambao wanataka kukuona wewe unatengana na familia yako. Usiwe mwepesi kudanganywa na usiwaamini.
Jaribu kupata malengo yao maovu kwa kutumia akili. Waambie waache haraka sana wanapoanza kumshutumu mume wako. Usione aibu kuwaambia: “kama mnataka muwe marafiki, basi acheni kuzungumza habari zinazohusu mume wangu. Si haki yenu nyinyi kumshutumu mume wangu. Ninampenda na hana dosari yoyote.”
Mara watakapo tambua kwamba unampenda mume wako na watoto wako kwa kutumia uimara wa ulimi wako, basi wanaweza wakatahayari kwa kukupotosha na hutasumbuliwa tena. Usidhani kwamba watakasirika, au kwamba utapoteza marafiki zako. Kama wao ni marafiki zako wa kweli, basi hawatakudhuru na sana watakushukuru. Kama ni maadui zako, basi, ni kipi kizuri zaidi cha kufanya kama sio kuwaepuka. Kama ukikutana na wale ambao wanang’ang’ania matendo yao maovu, vunja uhusiano wako nao.
Comments
Post a Comment