Uwe Mtu Wa Kuonesha Shukrani

Kama mtu ni mwema na mpaji wa utajiri wake ambao ameupata kutokana na kazi ngumu, shukrani na kuoenasha kufurahia kwako kwa matendo kama hayo ni hali ambayo itachangamsha hisia zake za ndani na kumfanya ahisi amefanikiwa.
Matendo ya ukarimu yanaweza kuwa kawaida ya mtu ambapo hujenga mazoea kutumia na kugawana utajiri wake na wale wanao hitaji. Hata hivyo, kama matendo ya ukarimu yanapuuzwa na hayafurahikiwi, mhusika anaweza akapoteza utashi na msukumo wa kufanya wema. Itakuwa ni kawaida kwa mtu kuhitimisha kwamba ilikuwa ni kutumia vibaya kutoa fedha yake aliyoipata kwa jasho ambapo hakuna shukrani inayotolewa.
Shukrani na kufurahishwa ni tabia za kuvutia akiwa nazo mtu na ni siri ambayo kwayo mtu anaweza kuvuta matendo ya msaada.
Hata Mwenyezi Mungu ametaja kwamba shukrani kwa neema Zake ni sharti ambalo husababisha neema Zake kuendelea kutolewa kwa wanadamu:
وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِنْ شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِنْ كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ {7}
“Na alipotangaza Mola wenu : Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.” (Qur’ani 14:7).

Mpendwa Bibi! Mumeo naye pia ni binadamu. Kama mtu mwingine yeyote yule. Yupo tayari kusaidia familia yake na anaiona kama wajibu wa uadilifu na kisheria. Anapopewa shukrani na kufurahikiwa kwa kutekeleza kazi yake, kazi hizo haziwi tena mzigo kwake.
Wakati wowote anaponunua vitu vya nyumbani au kitu kama nguo na viatu kwa ajili yako na watoto, furahi na umshukuru yeye. Onesha shukrani zako kwa vitu vidogo anavyofanya kama kununua bidhaa za vyakula, kusafiri na familia na kukupa wewe fedha. Unapoonesha shukrani, unamfanya mumeo ajihisi kuwa mwema na kuzawadiwa kwa usumbufu uliompata. Uwe mwangalifu kwamba usizipuuze kazi zake na kuwa mtu asiyejali mchango wake kuhusu ustawi wa familia.
Anaweza akaanza kutumia fedha yake kwingineko au kwake yeye mwenyewe.
Ikiwa tu rafiki au ndugu amekupa zawadi ya jozi ya soksi au shada la maua, unatakiwa kumshukuru mara nyingi, hivyo, ni kawaida tu na ni haki kumfurahia mumeo kwa kukupendelea na kukufikiria. Usidhani kwamba utakuwa unajidhalilisha kwa kuonesha shukrani zako. Kinyume chake, utapendwa na kujaliwa kwa vitu vingi zaidi kwa sababu unafurahia juhudi ya mumeo ambapo dharau na ubinafsi ni tabia ambazo zinaweza kuipeleka familia kwenye mabalaa.
Zifuatazo ni Hadith zinazozungumzia tabia za shukrani: Imam Sadiq (a.s) alisema: “Wanawake bora zaidi miongoni mwa wanawake wenu ni hao ambao huonesha furaha wakati waume zao huleta kitu nyumbani na hawaoneshi kutokuridhika kama hakuna kilicho letwa nyumbani.”
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwanamke yeyote ambaye husema kwa mumewe kwamba hajaona vitu vyovyote vizuri kutoka kwake basi anakuwa amekosa uaminifu na anavuruga ibada yake.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Yeyote asiye washukuru watu wanaomsaidia, kwa kweli, haoneshi shukrani zake kwa Mwenyezi Mungu kwa neema Zake.”

Usitafute Dosari Za Mwenzio

Hakuna mtu aliyekamilika. Watu wengine ni warefu sana au wafupi sana au wanene sana au wembamba sana, wanapua kubwa au pua ndogo, wanasema sana au wakimya sana, wana hasira zana au wanaelewana na watu haraka sana weusi sana rangi ya wastani au wanakula sana au wanakula kidogo na orodha inaweza kuendelea. Wanaume na wanawake wengi sana wanazo dosari hizi. Ni matumaini ya kila mwanaume na kila mwanamke kutafuta mwenzi aliyekamilika, lakini matumaini ya aina hiyo si sahihi. Hakuna uwezekano wa kumpata mwanamke anaye muona mumewe kama mtu aliye kamilika.
Wanawake hao ambao hutafuta makosa ya waume zao bila shaka watayapata.
Wanaweza wakaona dosari ndogo na kuzikuza kwa kushughulikia jambo hilo hadi kiwango cha kuwa kipingamizi kisichovumilika. Dosari hii huchukua nafasi ya sifa zingine zote za mume. Kila mara huwalinganisha waume zao na wanaume wengine. Wameanzisha kitu kinachoitwa mwanaume anayefaa katika dhana yao kiwango ambacho hakiafikiani na waume zao. Kwa hiyo, kila mara wanalalamika kuhusu dosari ndani ya ndoa zao. Wanawake hao hujifikiria kuwa na bahati mbaya na kushindwa na maisha na pole pole huwageuza kuwa wanawake |wenye chuki.
Tabia ya aina hiyo ya mwanamke humfanya nini mumewe? Anaweza kuwa ni mtu mvumilivu sana ambaye anaweza kustahamili ujeuri lakini upo uwezekano mkubwa atafedheheshwa na atakuwa na kinyongo kwa mkewe.
Hali hii inawezekana ikawatumbukiza wanandoa husika kwenye mabishano na kuelezana dosari za kila mwanandoa. Wote wawili watadharauliana na maisha yao yatageuka kuwa na mlolongo wa ugomvi na mabishano. Hivyo, ama wataishi katika mateso wakiwa pamoja au wataamua kutalikiana. Katika hoja zote mbili, wote watahasarika, hususan ambapo hakuna uhakikisho kwamba ndoa nyingine inaweza kuthibitisha vinginevyo.
Inasikitisha kwamba wapo wanawake wasiojua na wanakaidi katika huo ujinga wao. Inawezekana kwamba wanaweza kuharibu maisha ya familia zao kwa jambo dogo. Ifuatayo ni mifano ya wanawake wa aina hiyo: “Mwanamke alimwacha mume wake na akaenda nyumbani kwa baba yake kwa sababu mume wake alikuwa ananuka mdomo. Mwanamke huyo hakuwa tayari kurudi kwa mumewe hadi atatue tatizo lake. Kufuatana na malalamiko ya mume, mahakama iliwasuluhisha wana ndoa hao na mke akarudi kwa mumewe. Walipokwenda nyumbani, mke aligundua kwamba pumzi ya mumewe ilikua bado inanuka, kwa hiyo alihamia chumba kingine.”
“Daktari wa meno mwanamke alimtaliki mume wake kwa sababu hakuwa katika kiwango kinacholingana na cha kwake; mwanaume alifuzu na kupata taaluma hiyo miaka mitatu baada ya mke wake.”
“Mwanamke aliomba kumtaliki mume wake kwa sababu alikuwa na desturi ya kuketi chini na kula kwa kutumia vodole vyake, alikuwa hanyoi kila siku na hakujua jinsi ya kuishi na watu.”
Kama mambo yalivyo, si kwamba wanawake wote wapo hivi. Wapo wanawake wenye akili, wa kweli, na wanao utambuzi wa kutosha kwamba hawa hatarishi ndoa na furaha kwa kukuza dosari za waume zao. Mpendwa Bibi! Mumeo ni binadamu kama wewe. Hakukamilika, lakini anaweza kuwa na sifa nyingi. Kama unapendezwa na ndoa yenu na familia yenu basi usitafute udhaifu wake.
Usifikirie dosari zake ndogo kuwa muhimu. Usimlinganishe na mwanaume huyo ambaye umembuni akilini mwako. Inawezekana mumeo awe na udhaifu fulani ambao haupo kwa wengine. Lakini kumbuka kwamba wanaume wengine wanaweza kuwa na kasoro ambazo hazipo kwa mumeo. Ridhika na sifa zake. Hatimaye, utaona kwamba sifa zake zinazidi dosari zake. Zaidi ya hayo kwa nini utarajie kumpata mume mkamilifu ambapo wewe mwenyewe si mkamilifu. Kama wewe unajivuna kiasi cha kutosha kujiona wewe ni mkamilifu, basi waulize watu wengine:
Mtume (s.a.w.w) alisema: “Hakuna kitu kibaya zaidi kwa binadamu kuliko kutafuta dosari za watu wengine, ambapo hawajali mapungufu yao.”
Kwa nini ukuze dosari ndogo? Kwa nini uharibu maisha yako kwa kitu kisichokuwa maanani?
Uwe na busara, acha upuuzi! Puuza dosari za mumeo na usizitaje mbele yake au nyuma yake. Jaribu kutengeneza hali ya hewa ya uchangamshi katika familia yako na ufurahie neema za Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo, inawezekana pawepo dosari katika tabia ya mumeo ambazo unaweza kuzirekebisha. Kama ni hivyo, unaweza kufaulu kufanya hivyo hapo tu ambapo utakuwa na busara na uvumilivu. Hutakiwi umlaumu au kuanza kumgombeza, lakini mwendee kwa njia ya kirafiki.

Comments

Popular posts from this blog

NAMNA YA KUSWALI HATUA KWA HATUA

UTUKUFU WA MJI WA MAKKA NA MSIKITI MTUKUFU

Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1