Uganda LGBT: Kwa nini taifa hilo linawakamata na kuwashtaki wapenzi wa Jinsia moja
GETTY IMAGES
Maafisa wa polisi nchini Uganda wanasema kwamba watu 16 waliokamatwa siku ya Jumatatu katika kijiji kimoja kilichopo jirani na mji mkuu wa kampala watashtakiwa kwa kushiriki ngono kwa njia ilio kinyume na maumbile.
Siku ya Jumatatu usiku, umati wa watu ulizingira makazi ya vijana 16 yalio kwenye mtaa wa Kyengera, nje kidogo mwa Mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Vijana hao waliwapigia simu polisi na kuomba usaidizi wa dharura. Polisi ilipofika kwenye eneo hilo, ilitawanya umati huo wa watu na kuwatia mbaroni watu hao na kuwapeleka maeneo salama.
Na kufikia siku ya Jumatano, polisi ilikataa kuwaachilia washukiwa hao na kusema itawafungulia mashtaka ya kuwa wapenzi wa jinsia moja.

Polisi inasema kwamba ukaguzi wa kimatibabu umeonesha kwamba walikuwa wakishiriki ngono kinyume na maumbile.
Frank Mugisha ambaye ni mtetezi wa haki za wapenzi wa jinsia moja anasema, wanajaribu kuwatowa vijana hao kwasababu walikamatwa wakiomba usaidizi kutoka kwa polisi.
Sheria ya adhabu ya Uganda inamruhusu jaji kumfungia maisha mtu yeyote anayehukumiwa kwa hatia ya kuwa mpenzi wa jinsia moja
Ingawa polisi imekuwa ikikamata washukiwa kadhaa wa mapenzi ya jinsia moja, lakini ni wachache tu wamefanyiwa mashtaka mahakamani
Hatua hiyo inajiri karibia wiki mbili baada ya serikali ya Ugandan kusema kwamba haikuwa na mipango kurudisha upya muswada wa wapenzi wa jinsia moja ambao unaweza kutoa adhabu kali ikiwemo kunyongwa kwa watu wanaoshiriki mapenzi hayo.
Chini ya sheria iliowekwa wakati wa ukoloni, mtu yeyote atakayepatikana na hatia anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifungo cha maisha jela.
- Ndoa za mapema marufuku Tanzania, uamuzi wapokewaje?
- Ni nani anayeuzia Uturuki silaha za kijeshi?
- Putin ana mpango gani na Afrika?
Sheria inaelezea kitendo cha ngono kinyume na maumbile kama mwanamume kushiriki ngono na mwanamume mwengine au mwanamke kwa mwanamke.
Miezi miwili iliopita waziri wa maadili nchini Uganda amesema kuwa shughuli zote za wapenzi wa jinsia moja ni haramu na kinyume na tamaduni za watu wa Uganda.
Simon Lokodo aliuambia mkutano wa waandishi habari kuwa shughuli za wapenzi wa jinsia moja haziruhusiwi kamwe Uganda.
Katika jamii yetu maswala ya ngono huwa ni ya siri mno, itakuwaje kuwa sasa maswala ya ngono yanawekewa gwaride ?, aliuliza Simon Lokodo , Waziri wa maadili Uganda
Waziri huyo alikuwa akitoa sababu iliyosababisa polisi kupiga marufuku mkutano wa wapenzi wa jinsi moja katika klabu moja ya usiku mjini Kampala.
Mwanaharakati wa kupigania haki za wapenzi ya jinsia moja nchini Uganda anasema kuwa watu wenye wapenzi wa jinsia moja wanastahili kuendelea na shughuli zao ikiwa watahitaji kufanya hivyo.
Kupitia mtandao wake wa kijamii Frank Mugisha anasema kuwa ''jamii ya LGBT itaendelea kufanya mikutano yao kama inavyoruhusiwa kikatiba bila pingamizi lolote''
Lakini Waziri wa maadili nchini Uganda amesema kuwa serikali yake haitawafumbia macho wale wanaoshabikia wapenzi wa jinsia moja na kujaribu kusambaza harakati zao alizoita haramu nchini humo.
''Tutapambana na mtu yeyote atakayejaribu kuchochea ama hata kufadhili na kupigia debe swala la wapenzi wa jinsia moja''
Fahamu mataifa yaliohalilisha na kupinga mapenzi ya jinisia moja Afrika
Angola ni nchi ya hivi karibuni Afrika iliofuta sheria ambayo ilikuwa inatafsiriwa kama inapinga mapenzi kwa watu wa jinsia moja.
Serikali ya nchi hiyo tayari imekataza ubaguzi wa watu kulingana na hali zao za mahusiano; yeyote anayemnyima mtu kazi au huduma kutokana na uhusiano wao wa kimapenzi anahatarisha kufungwa jela kwa kipindi cha mpaka miaka miwili.
Angola ni koloni la zamani la tatu la Ureno barani Afrika kufuta sheria zinazokataza mahusiano ya watu wa jinsia moja, Visiwa vya Sao Tome na Cape Verde.
Hata hivyo hakuna mtu yeyote anayefahamika ambaye alishawahi kufungwa ama kukamatwa kama sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo iliyofutwa. Angola inatazamwa kama nchi ambayo watu wake wengi hawana mtazamo hasi na matendo ya mapenzi ya jinsia moja.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamua la Amnesty International linaeleza kwamba haki za kisheria zinapungua kwa wapenzi wa jinsia moja barani Afrika.
Nchi nyingi za Afrika zina sheria kali zinazopingana mahusiano ya watu wa jinsia moja.
CLARE SPENCERUganda:
Mapenzi ya watu wa jinsia moja iliharamishwa nchini Uganda chini ya sheria za ukoloni katika kifungu kinachokataza mtu kufanya ngono kinyume na kawaida.
Waziri wa maadili nchini Uganda Simon Lokodo, mwezi uliopita alisema shughuli zote za wapenzi wa jinsia moja ni haramu na kinyume na tamaduni za watu wa Uganda.
Wanaharakati wa kupigania haki za wapenzi ya jinsia moja nchini Uganda wanasema kuwa watu walio wapenzi wa jinsia moja wanastahili kuendelea na shughuli zao ikiwa watahitaji kufanya hivyo.
Serikali hatahivyo kupitia wizara ya maadili nchini humo inasema kuwa haitawafumbia macho wale wanaoshabikia mapenzi ya jinsia moja na kujaribu kusambaza harakati hizo zinazotazamwa kuwa za haramu nchini.
Iwapo utapatikana katika uhusiano wa aina hii, unaweza kufungwa miaka 7 gerezani.
GETTY IMAGESKenya:
Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume na sheria Kenya na mtu anaweza kuadhibiwa kwa hadi miaka 14 gerezani.
Mnamo 2016, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu limegundua kwamba wapenzi wengi wa jinsia moja wanaoishi nchini Kenya wanakabiliwa na 'wasiwasi wa usalama kila siku'.
Chini ya sheria za Kenya zilizoandikwa enzi za ukoloni, mapenzi ya jinsia moja yametambuliwa kama kitendo kisicho cha kawaida, na kuwekwa katika kitengo kimoja na hatia ya kufanya mapenzi na Wanyama.
Wanaharakati wanasema kwamba kuwepo kwa sheria hii kumezidisha ubaguzi, huku watu wakifurushwa kutoka nyumba walizokodisha, kunyimwa nafasi za kupata matibabu na pia kuhangaishwa na polisi, yote kwa sababu ya jinsia zao.
Wanaharakati wamewasilisha kesi mahakamani kutaka kubainishwa uamuzi kuhusu uhalali wa sheria inayoharamisha mapenzi kwa watu wa jinsia moja.
Katiba ya Kenya inaonya dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote, ikiwemo ubaguzi wa kijinsia.
Afrika kusini:
Mwaka 2006 Afrika ya Kusini ilikuwa nchi ya kwanza Afrika na ya tano duniani kuruhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja. Hata hivyo, si wote wanaokabiliana na hatua hiyo, na nje ya miji mikubwa wapenzi wengi wa jinsia moja wanakumbana na mashambulizi na kutengwa na jamii zao.
Jiji la Cape Town ndiyo sehemu pekee nchini humo ambao wapenzi wa jinsia moja wapo salama zaidi na wamekuwa wakifanya tamasha la kila mwaka la kuionesha na kujitangaza uwepo wao.
Tanzania:

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kufanya mapenzi 'kinyume na maumbile' ni kosa la jinai ambalo mtu akikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 au maisha jela.
Hatahivyo wadadisi wanaona taifa hilo kwa kiasi fulani limelegeza kamba juu ya mahusiano hayo ya mapenzi ya jinsia moja kufuatia hatua ya serikali kujitenga na kampeni ya kuwakamata na kushtaki wapenzi wa jinsia moja iliyoidhinishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Makonda aliidhinisha kamati maalum aliyoieleza kuwa ni ya kuhakikisha kuwa watu wanaofanya biashara chafu za ngono wanachukuliwa hatua za kisheria.
Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Tanzania imevifunga vituo kadhaa visivyo vya kiserikali kwa madai ya kuchochea ushoga kwa kutoa elimu ya mahusiano ya jinsia moja.
Nigeria:
Kwa mujibu wa Amnesty International, Nigeria tayari imepinga mapenzi ya jinsia moja.
lakini kumeshuhudiwa visa vingi vya watu kukamatwana kuwekwa gerezani, na adhabu zimezidi kuwa kali wakati rais wa taifa hilo alipopitisha marekebisho kwa sheria zilizopo mnamo Januari 2014.
Zambia:
Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, ni haramu nchini Zambia.
Wadadisi wanasema kuwa watu wengi, wanaamini kuwa ni kinyume na imani zao
Vitendo kama ulawiti na uhusiano wa mapenzi kati ya wanawake, vina adhabu ya miaka 15 au kufungwa maisha jela.
Msumbiji:
Msumbiji imehalalisha mapenzi ya jinsia moja, na kuwa moja wapo wa nchi chache Afrika zinazohalalisha mapenzi ya jinsia moja.
Sheria hiyo iliyowekwa na wakoloni wa nchi hiyo Ureno iliondolewa na bunge la nchi. Watetezi wa haki za wapenzi wa jinsia moja, wametaja hatua hiyo kama ushindi mkubwa.
Sheria ya awali ilitupiliwa nje na mahakama ya kikatiba.
Hatahivyo, wanaharakatia wanasema, hiyo ni hatua ya kwanza tu katika jitihada za usawa wakikamilifu nchini humo.
Shirika lililopigania haki na mageuzi hayo, Lambda, bado halitambuliwi kikamilifu kama shirika lisilo la kiserikali, Amnesty International linasema.
source;BBC
Comments
Post a Comment