Uchumi Wa Familia

Kufanya mpango wa sadaka ya mke ni wajibu wa mume. Ni kwamba mwanaume anawajibika kulipa gharama za mke wake kama chakula, nguo, nyumba, daktari na dawa. Atakuwa anakosea kama hata mgharimia mke wake na anaweza kushitakiwa kisheria.
Mtu hawezi kutarajia familia iishi bila matumizi yeyote ya fedha. Watu wa familia wote wanahitaji chakula, nguo, dawa na mahali pa kuishi. Hata hivyo, wanaweza wakaomba vitu visivyo muhimu ambavyo mwanaume anaweza kukataa kuvinunua na asikubaliane na matakwa yao mbali mbali.
Mtu mwenye busara atatumia fedha kufuatana na uwezo wa kipato chake. Lazima abainishe bidhaa muhimu na avinunue katika mpango wa kipaumbele wakati wowote anapoweza. Lazima pia aweke akiba ya fedha kwa matumizi ya siku za shida. Kiasi fulani cha fedha lazima kitengwe kwa ajili ya kodi ya nyumba au kununua mahali pengine. Lazima mume asisahahu umeme, maji, nishati na simu. Kodi na ada za shule lazima zikumbukwe. Lazima kabisa aepukane na kutumia zaidi ya bajeti na kulipa vitu visivyo muhimu. Mpango mzuri wa matumizi ya fedha utamwepusha mtu asifilisike au kuwa na madeni.
Mwenyezi Mungu huona matumizi yaliyopangwa vizuri ni ishara ya imani na anasema ndani ya Qurani:

وَالَّذِينَ إِذَا أَنْفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامًا

{67}
“Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili bali wanakuwa katikati baina ya hayo”. ( Quran 25:67).
Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Yapo makundi manne ya watu ambao sala zao hazitafika kiwango cha kukubaliwa; Kundi moja ni la watu ambao hutumia vibaya utajiri halafu humwomba Mwenyezi Mungu Mweza, ‘Ee Mwenyezi Mungu naomba riziki. Halafu Mwenyezi Mungu hujibu, si nilikuagiza uwe mwangalifu katika matumizi yako. ’ ”
Abdullah bin Aban anasema: “Nilimuuliza Musa bin Jafar (a.s) kuhusu utunzaji wa familia ya mtu na akasema: ‘Ubadhilifu na uchoyo vyote ni sifa mbaya. Mtu lazima awe na kiasi.”
Mtu mwenye busara ataepuka kukopa fedha na hawezi kuchukua mkopo kwa matumizi mabaya. Uchumi unaotegemea mikopo (na riba), inayopokewa kutoka kwenye mabenki na taasisi zingine si sahihi kiislamu na kimantiki haufai.
Kununua vitu kwa mkopo, ingawa hufanya nyumba yako ionekane nzuri, lakini faraja na utulivu wa akili hutoweka.
Kwa nini mtu ananunua vitu visivyo muhimu kwa bei ya juu zaidi na kujaza mifuko ya wenye mabenki kwa malipo kidogo? Ni maisha ya aina gani hayo ambapo kila kitu hupatikana kwa bei ya mkopo? Kwani si vema zaidi kwa mtu kungoja na kuweka akiba ili anunue bidhaa kwa bei nafuu?
Ni kweli kwamba kupata fedha ni vigumu na huathiri sana maisha ya mtu. Hata hivyo, la muhimu zaidi ni jinsi mtu anavyotumia fedha yake. Zipo familia zenye vipato vizuri ambazo kila mara ni wadeni wa wengine. Zipo pia familia nyingi zenye vipato vya chini ambao huishi kwa raha. Tofauti baina ya makundi haya mawili ni jinsi ya fedha inavyo tumiwa. Kwa hiyo, inafaa zaidi ama mwanaume aendeshe udhibiti wa matumizi au awe msimamizi wa mtu ambaye anawajibika nayo.
Mwisho, inakumbushwa kwamba ubakhili ni mbaya kama ufujaji, kama mwanaume anacho kipato zaidi lazima aifurahishe familia yake zaidi na kuwapa mahitaji yao muhimu kadiri iwezekanavyo.
Utajiri na fedha vyote ni vya kutumia na kuwezesha upatikanaji wa vitu muhimu vya maisha, na si vya kulundika na kuviacha hapa duniani.
Ishara za utajiri lazima zionekane wazi kwenye familia ya mtu na nyumba. Kuna manufaa gani kufanya kazi kwa bidii halafu kinachopatikana kisitumike?
Mtu mzima atumie utajiri kuhusu familia yake na starehe yake mwenyewe. Inachukiza kuona mtu ambaye anao uwezo wa kifedha lakini watoto wake wanatamaani chakula kizuri na nguo nzuri. Watoto wa mtu bakhili kungoja kifo chake ili wagawane utajiri wake. Kama Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anampa mtu neema zake, neema hizi lazima zidhihiri katika maisha ya mtu huyo.
Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema: “Si mwenzetu (si mfuasi wa Mtume s.a.w.w) ambaye anazo fedha lakini huiweka familia yake mbali na utajiri wake.”
Musa bin Jafar (a.s) alisema: Jamaa ya mtu ni watu wanaomtegemea. Hivyo, yeyote anayepewa neema za Mwenyezi Mungu, lazima azisambaze kwa wale wanao mtegemea ili wafarijike, au vinginevyo neema hizo zitaondoshwa kwake.”
Imamu Rida (a.s) alisema: “Ni jambo la manufaa kwa mtu kuwapa watu wa familia yake starehe itokanayo na matumizi yake, ili wasingoje hadi hapo atakapofikwa na mauti.”
Imamu Ali (a.s) alisema: “Tayarisha matunda kwa ajili ya watu wanaokutegemea kila siku ya Ijumaa ili kwamba watafurahia kuja kwa Ijumaa.”

Saidia Kufanya Kazi Za Nyumbani

Licha ya kwamba utunzaji wa nyumba ni wajibu wa wanawake, lazima ieleweke kwamba kuendesha mambo ya nyumbani si kazi rahisi.
Mke ambaye ni mama wa nyumbani hata akitumia muda kiasi chochote kile kwa utunzaji wa nyumba, hatoweza kumaliza kazi hiyo yote kwa wakati moja. Hii ni kweli hasa zaidi pale ambapo anatakiwa kuwakirimu wageni au anapougua na kadhalika. Kazi ya kutunza nyumba humchosha mke wa nyumbani na hivyo wanaume wanatarajiwa kuwasaidia wake zao katika suala hili.
Si haki kwamba mwanamume awe amekaa nyumbani bila ya shughuli yoyote ambapo mke wake anashughulika na kazi nyingi mbali mbali. Inafaa tu mume kumsaidia mke wake kadiri iwezekanavyo na wakati wowote awezapo. Msaada huu ni ishara ya huba ambayo humvutia mke kwa mume wake na familia yake.
Si ujasiri wa kiume hata kidogo kwamba mwanaume hapaswi kugusa kitu chochote ndani ya nyumba, bali kutoa amri tu kumpa mkewe. Nyumba ya familia si makao makuu ya kutoa amri, isipokuwa hapo ni mahali pa upendo, wema na ushirikiano.
Bwana mpendwa! Usidhani kwamba wewe ukifanya kazi za nyumbani ni kushusha hadhi yako. Kinyume chake ni kwamba, mke wako atapendezwa sana na kitendo chake cha kumsaidia.
Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu ambaye ni mtu anaye heshimiwa sana katika historia, alikuwa na desturi ya kusaidia kazi za nyumbani.
Ayisha, mke wa Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wakati wowote Mtume
(s.a.w.w) anapokuwa hana kazi, alikuwa na desturi ya kushona nguo zake, kutengeneza viatu vyake na alikuwa anafanya kazi nyumbani kama wanaume wengine.”

Rudi Nyumbani Mapema

Mwanaume asiye na mke anao uhuru wa kutumia muda wake, lakini pindi anapooa, lazima abadilishe mpango wake. Hawezi kukaa nje kwa muda wowote anaotaka. Anatakiwa kumtaarifu mke wake mahali alipo na kadhalika. Lazima asisahau kwamba mke wake huwepo nyumbani siku nzima, husafisha nyumba, huosha vyombo na hupika. Humngoja arudi nyumbani mara tu anapomaliza kazi zake, ili amuone, azungumze naye na kufurahia kuwa naye.
Watoto pia huwa na matumaini ya kumuona baba yao. Si haki kwamba mwanaume aache familia yake nyumbani na yeye afuate starehe zake mahali pengine.
Ndoa si tu kulisha chakula na kuimvisha nguo familia yako. Mwanamke ni mwenza wa mume wake na si mtumishi. Mke hayupo pale kwa ajili ya kufanya kazi mchana kutwa na kulishwa chakula lakini hasa zaidi anayo matarajio ya kuwa na rafiki wa kudumu na mwenza.
Baadhi ya wanaume kwa kweli hawafanyi sawa, hawana haki na wapumbavu. Huwaacha wake zao na watoto wao nyumbani na kutumia muda wa usiku kucha mahali pengine. Fedha ambayo wangetumia na familia nyumbani, anaipoteza mahali pengine.
Wanaume wa aina hii bado hawajaelewa maana ya mapenzi na huba na huona starehe zao zisizo na thamani na chafu kama ndio njia ya maisha mazuri. Hawatilii manani ukweli kwamba vitendo kama hivyo huwadhalilisha. Wengine hutambua vitendo kama hivyo kuwa vya kipumbavu na kijeuri.
Wanaume wa aina hii ni sababu ya huzuni kwa wenyewe na familia zao. Matendo yao huwashawishi wake zao kudai talaka kutoka kwao.
Mwanaume ambaye alimtaliki mke wake, alisema mahakamani: “Mwanzoni mwa ndoa yangu, nilikuwa na marafiki fulani ambao nilikuwa nikitoka nao kwa matambezi, ambapo humwacha mke wangu nyumbani… na nilikuwa na desturi ya kurudi nyumbani kesho yake alfajiri. Mke wangu ambaye alichoshwa na hali hii, alipewa talaka.
Tulikuwa na watoto kumi, ambao nilitaka kukutana nao mara mbili kwa mwezi. Kipindi fulani kilipita tukitekeleza mpango huu. Lakini sasa ni muda mrefu tangu watoto wangu wajifiche na ninayo shauku kubwa kuwaona watoto wangu.”
Mwanamke alisema; “Nimekata tamaa kwa upweke. Mume wangu hajali kabisa kuhusu mimi. Kwa ajili ya starehe zake huwa nje hadi asubuhi sana.”
Bwana mpendwa! Sasa umeoa. Usiendekeze tabia ya kikapera. Wewe unawajibika kwa mke wako na watoto wako, acha kushirikiana na marafiki wasiofaa rudi nyumbani mara unapomaliza kazi yako. Furahia maisha ya familia na mke wako na watoto wako. Hata kama starehe zako za kila siku usiku si zenye uovu, hata hivyo, zinaweza kusababisha madhara kwako na maisha yako ya ndoa.

Uwe Mwaminifu

Baada ya mapatano ya ndoa maisha binafsi ya watu wawili yanalingana na kuwa maisha ya ushirika moja wa kijamii. Kiapo kitukufu cha ndoa kinamaanisha kwamba mwanaume na mwanamkie wanapeana ahadi kila moja kuwa pamoja katika maisha yao yote, kusaidiana wao kwa wao, kuwa mwema na mwelewa wakati wote, wakati wa neema na wakati wa shida, wakati wa ugonjwa na afya njema na huzuni na kadhalika.
Utu unadai kwamba mwanandoa anatakiwa kuwa mwaminifu kwa ahadi yake. Wanandoa hawatakiwi kusahau mkataba wao hata kwenye hali ngumu. Msichana mdogo ambaye huchagua mwanamume mmoja kuishi naye katika maisha yake yote hatarajii kuwa amekuwa mwanamke wa makamo ya utu uzima. Si haki kwamba mwanaume atafute starehe na mwingine na kumwacha mke wake.
Mwanamke ambaye hutoa mchango mkubwa katika kujenga familia madhubuti katika mazingira mazuri ya maendeleo ya uchumi, hatarajii mume wake kumpenda mwanamke mwingine.
Mwanamke anayefanya bidii nyumbani kwa kawaida anayo matumaini kwamba mume wake hatamnyima mapenzi na huba yake wakati wa ugonjwa na kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi. Jambo la mwisho kabisa hatarajii mume wake kutafuta starehe ya kwake peke yake.
Baadhi ya wanaume kwa kweli hawashituki. Wakati wake zao ni vijana na maumbo ya kuvutia wanafurahia kuwa nao, lakini huwaacha wanapo zeeka.
Mwanaume alimtaliki mke wake kwa sababu ya kuwa na kisirani, kwani tangu walipooana baba yake alikufa na mjomba wake akafilisika.
Mwanaume aliye muoa mwanamke kijana kwa kumpenda, alimtaliki baadaye kwa sababu hakumpenda tena.
Mwanamke… alilalamika mahakamani: “Nimeishi na mume wangu kwa miaka mingi, lakini sasa nimepata maradhi anasema kwamba hataki mke mgonjwa!”
Bwana mpendwa! Wewe si hayawani ambaye maisha yake yote ni kula na kukidhi matamanio ya kimwili. Wewe ni binadamu mwenye mchomo wa moyo, dhamira na tabia ya kujitolea. Hivi ni haki kweli kwamba wewe unafuatilia starehe zako nje ya nyumba yako?
Kama ndio, basi wewe ni muonevu na kwa hali hiyo wewe utaadhibiwa hapa hapa duniani. Ukitumia muda wako na mwanamke mwingine, basi, kwa ajili ya starehe utulivu wa akili yako na utapata maradhi ya kuharibikiwa akili. Watoto wako hawatakubali na watajibu kwa kukukashifu.
Kama mke wako anaugua, chukua hatua muhimu za kumtibu, na kama anayo maradhi yasiotibika, basi endelea kuishi naye, jitolee kumsaidia na usioe mke mwingine akingali hai.
Usimuudhi wakati huo mgumu. Ungetarajia nini endapo wewe ungekuwa katika hali hiyo? Ni haki kabisa kwamba yeye angetegemea hivyo hivyo kutoka kwako.
Ni sahihi kwamba wewe unapo ugua mke wako atataka umtaliki? Je hujafedheheka mbele ya marafiki na ndugu? Kwa hiyo kama unakubali kwamba uaminifu na unyofu ni sifa nzuri, basi jaribu kuwa mwaminifu.

Elimu Na Mafundisho

Mwanamke kijana ambaye ndio kwanza kaolewa anao wajibu wa kuendesha mambo ya mume wake na katika hali hiyo atahitaji ujuzi wa kupika, usafi, kunyosha nguo, kushona, kupanga fenicha, kukaribisha wageni wake, kushirikiana na watu wengine, kumtunza mtoto wake na kadhalika.
Mume wake atatarajia mke wake kujua yote haya. Hata hivyo, mategemeo yake yanaweza yasifanikiwe takriban muda wote kwa sababu ujuzi wa mke wake kijana kuhusu utunzaji wa nyumba ama haupo kabisa au upo kidogo sana.
Mtu afanyeje? Hili ni tatizo katika jamii zetu. Wazazi hawajali, wala mfumo wa elimu hauna mipango ya kutosha kukidhi haja hii. Hata hivyo, mtu anatakiwa kupata ufumbuzi wa tatizo hili.
Kwa vile mwanaume anakusudia kuishi na mke wake kwa maisha yake yote lazima amsaidie kumuelimisha, kwa sababu kwa kawaida wanaume huwa na umri mkubwa kuzidi wa wake zao na hivyo wanao uzoefu zaidi.
Mwanaume kwa uvumilivu anaweza kumuelemisha mke wake na kumfundisha vitu ambavyo anavijua. Anweza hata kumuuliza mama yake, dada au shangazi zake kuhusu mambo ambayo hayajui, au anaweza hata kununua vitabu vinavyohusu masomo kama ya kupika, ushonsji, utunzaji wa nyumba na kadhalika.
Mwanaume vile vile lazima amhimize mke wake kusoma vitabu ambavyo vitaonesha kimaadili kuwa ni vyenye manufaa. Lazima asahihishe upungfu wake wa maadili kwa adabu nzuri na sio kwa upinzani, au vinginevyo atageuka dhidi yake.
Mwanaume, kwa kutumia uvumilivu wake, anaweza kumwelimisha mke wake kwa mujibu wa njia yake ya maisha katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo wa ndoa yao. Inawezekana asifaulu asili mia kwa mia lakini bila shaka atakaribia kutosheleza mahitaji.
Elimu ya aina hii inahitaji uvumilivu, muda na busara, lakini mwanaume lazima ajaribu kuipata. Hii ni kwa sababu mwenza mzuri ni mama mzuri kwa watoto wake ni neema kwa mwanaume.
Mojawapo ya mambo muhimu ambayo mwanaume Mwislam aliyeoa anatakiwa kukumbuka ni ukweli kwamba mke wake pia ni Mwislam, na inawezekana awe hatambui utaratibu wa maisha ya Kiislamu na sheria zake. Inawezekana asijue hata kuhusu wudhu, kusali na kadhalika.
Kwa kweli ni wajibu wa wazazi kuwafundisha watoto wao mambo yote muhimu ya Kislamu na maadili. Kwa bahati mbaya, hata hivyo, wazazi hawajui kabisa kuhusu ukweli huu, na bila kuwafundisha mabinti wao kitu chochote kuhusu Uislamu, wanawaozesha. Hivyo wajibu wao huangukia kwenye mabega ya waume wanaowaoa.
Bwana mpendwa! Ni wajibu wako kumzoeza mke wako maadili ya Kiislamu na kumfundisha mambo yaliyohalalishwa na yale yaliyo haramishwa katika dini. Mfanye ajifunze kuhusu tabia za Kiislam. Kama huwezi kufanya hivi, basi tafuta msaada kutoka kwa wengine au fanya mpango wa vitabu na makala zenye elimu ya Uislamu na mwambie asome na kufanya kwa vitendo. Unaweza hata kufanya mpango wa elimu na maelekezo yake kupitia kwa mtu mwaminifu na aliyeelimika.
Kwa ufupi, ni wajibu wa mwanaume kumtia moyo mke wake kumuamrisha kufanya mema na kumkataza kufanya mabaya. Kama mwanamume atafuata wajibu wake huu, basi atafurahia kuwa na mwenza mwenye tabia njema, mwema, muaduilifu na mke mwenye busara.
Hata hivyo, kama mwanamume anaamua kutojali wajibu wake atateseka kwa kuwa na mke mjinga ambaye imani yake ni dhaifu na ambaye hana kinga dhidi ya uovu. Pia mume ataulizwa na Mwenyezi Mungu huko akhera kuhusu uzembe wake huu.
Mwenyezi Mungu anasema kwenye Qurani Tukufu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ

{6}
“Enyi mlioamini jiokoeni nafsi zenu na watu wenu (wa nyumbani – wake zenu watoto wenu nk.,) kutokana na moto ambao kuni zake ni watu na mawe…” (Quran 66:6)
Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Aya hiyo hapo juu ilipoteremshwa mmoja wapo wa Waislamu alikuwa analia na kusema; ‘Mimi siwezi kujinusuru hata mimi mwenyewe kutoka kwenye moto wa Jahanamu na ninatakiwa kuwajibika kuinusuru pia familia yangu kutoka kwenye Jahanamu!’ Mtume (s.a.w.) alimwambia mtu huyu: “Ingetosha kama tu ungewaagiza kufanya mambo hayo ambayo wewe unayafanya na uwakataze wasifanye yale ambayo wewe mwenyewe unajizuia kuyafanya.”
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wanaume wameumbwa kuwa viongozi na kuwajibika kwa familia zao, na kwa namna hiyo wanawajibu kwa watu wanaowategemea.”

Mtukufu Mtume (s.a.w.) pia amewakumbusha wanawake: “Waambieni waume zenu wafanye matendo mema kabla hawajawashawishi nyinyi kufanya mabaya.”

Comments

Popular posts from this blog

NAMNA YA KUSWALI HATUA KWA HATUA

UTUKUFU WA MJI WA MAKKA NA MSIKITI MTUKUFU

Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1