SWALA

Swala ndio nguzo kubwa ya dini na ni mafungamano ya mja na Mola wake. Kwa sababu hiyo, swala imekuwa ibada kubwa sana na yenye hadhi tukufu mno. Allah amemuamrisha Muislamu kudumu kuswali katika mazingira yake yote; awapo mjini mwake, safarini, wakati wa afya njema na wakati wa ugonjwa. Maana ya swala Nafasi ya swala na fadhila zake Swala tano zilizofaradhishwa na nyakati zake Mahali pa kuswali Namna ya kuswali Je, ninaswali vipi? Nguzo za swala na mambo yake ya wajibu Swala ya jamaa Adhana Swala ya Ijumaa Swala ya msafiri Swala ya mgonjwa

Maana ya swala

Maana ya swala kilugha ni maombi. Swala ni mafungamano ya mja na Mola na Muumba wake. Swala inajumuisha maana ya juu sana ya unyenyekevu na kumtegemea Allah na kumuomba msaada. Mja anamuomba Mola wake, anasemezana naye na kumtaja, na kwa sababu hiyo nafsi yake inatakasika, anakumbuka jinsi alivyo na jinsi dunia anayoishi ilivyo, anahisi utukufu wa Mola wake na huruma zake kwake. Hapo, swala hii inamuongoza awe na msimamo imara katika sheria za Allah na kukaa mbali na udhalimu, uasi na mambo machafu, kama Allah alivyosema kuwa: «Kwa yakini, swala inakataza mambo machafu na maovu». (Sura Al-ankabuut, aya 45).
«Kwa yakini, Swala inakataza machafu na maovu». Sura Al-ankabuut, aya 45.

Nafasi ya swala na fadhila zake

Swala ni ibada kubwa sana miongoni mwa ibada zinazofanywa na mwili, na yenye hadhi tukufu sana. Ni ibada inayohusisha moyo, akili na mdomo. Umuhimu wa swala unakuwa wazi katika mambo mengi. Miongoni mwa mambo hayo ni haya: 

Swala ina daraja za juu sana:

  1. Swala ni nguzo ya pili katika nguzo za Uislamu. Mtumeswallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: Kukiri kuwa hakuna anayestahiki kuabudiwa  kwa haqi isipokuwa Allah tu na kwamba Muhammad ni Mtume  wa Allah, na kusimamisha za swala…». (Bukhari, Hadithi Na. 8. Muslim, Hadithi Na. 16). Nguzo ya jengo ndio msingi ambao linautegemea na haliwezi kusimama bila ya msingi huo.
  2. Hoja za kisheria zimeweka tofauti baina ya Waislamu na Makafiri ni kusimamisha swala kama Mtume, swallalahu alayhi wasalam, alivyosema kuwa: «Kwa yakini, baina ya mtu na baina ya Shirki na ukafiri ni kuacha swala». (Muslim, Hadithi Na. 82). Pia amesema kuwa: «Ahadi ambayo ipo baina yetu na baina yao ni swala. Kwa hiyo, mwenye kuiacha amekuwa kafiri». (Tirmidhi, Hadithi Na. 2621. Annasai, Hadithi Na. 463).
  3. Allah Mtukufu ameamrisha kudumu kuswali katika mazingira yote; safarini, katika ukaazi, katika amani, katika vita, katika hali ya afya njema na katika ugonjwa. Swala inatekelezwa kwa kadiri ya uwezo, kama Allah alivyosema kuwa: «Dumuni katika swala». (Sura Albaqara, aya 238). Pia amewasifu waja wake waumini kwa kauli yake kwamba: «Na ambao wao wanadumu katika swala zao». (Sura Almuuminun, aya 9).

Fadhila za swala

Zimekuja hoja nyingi katika Qur’ani na katika Sunna kuhusu fadhila za swala. Miongoni mwa hoja hizo ni hizi:
  1. Swala inafuta dhambi, kama Mtume,swallalahu alayhi wasalam, alivyosema kuwa: «Swala tano na Ijumaa mpaka Ijumaa zinafuta (madhambi) yatokeayo baina yao, madamu hayajafanywa madhambi makubwa». (Muslim, Hadithi Na. 233. Tirmidhiy, Hadithi Na. 214).
  2. Swala ni nuru inayomuangazia Muislamu katika maisha yake yote. Inamuimarisha kwenye kheri na kumuepusha na shari, kama Allah Mtukufu alivyosema kuwa: «Kwa yakini, swala inakataza mambo machafu na maovu». (Sura Al-ankabuut, aya 45). Na Mtume,swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Swala ni nuru». (Muslim, Hadithi Na. 223).
  3. Swala ni jambo la kwanza kabisa atakalohojiwa mja Siku ya Kiama. Swala ikiwa imetengemaa na kukubaliwa, matendo mengine yatakubaliwa. Swala ikikataliwa, matendo mengine nayo yatakataliwa, kama Mtume, swallalahu alayhi wasalam, alivyosema kuwa: «Jambo la mwanzo kabisa atakalohojiwa mja Siku ya Kiama ni swala. Swala ikitengemaa, matendo mengine yatatengemaa, na swala ikiwa mbaya, matendo mengine nayo yatakuwa mabaya». (Tabaraaniy, Hadithi Na. 1859).
Swala ni kipindi kitamu sana cha muumini pale anapozungumza na Mola wake, na kwa hiyo, anahisi burudani, utulivu na kuliwazika kwa kuwa na mahusiano na Allah Mtukufu.
  • Swala ni ladha adhimu sana kwa Mtume, swallalahu alayhi wasalam  kama yeye mwenyewe alivyosema kuwa: «Na faraja yangu imewekwa katika swala». (Annasaai, Hadithi Na.3940).
  • Mtume alikuwa akimwambia Muadhini wake Bilali, Allah amuwiye radhi, ili aadhini kwa ajili ya swala kwamba: «Tuburudishe kwayo ewe Bilali». (Abudaud, Hadithi Na. 4985).
  • Mtume,swallalahu alayhi wasalam, akikerwa na jambo au kumshughulisha alikuwa akikimbilia kuswali. (Abudaud, Hadithi Na. 1319).

Comments

Popular posts from this blog

NAMNA YA KUSWALI HATUA KWA HATUA

Maana ya kufunga Maana ya kufunga katika Uislamu: Ni kufanya ibada kwa ajili ya Allah kwa kujizuia na kuacha kula, kunywa, kujamiiana, pamoja na vitu vyote vyenye kufunguza, kuanzia kuchomoza kwa alfajiri –ambao ni muda wa adhana ya Alfajiri- mpaka kuzama kwa jua – ambao ni muda wa adhana ya Magharibi-. «...Basi atakayekuwa katika mji (hayuko safarini) miongoni mwenu katika mwezi (wa Ramadhani) aufunge». Sura Albaqara, aya 185. Ubora wa mwezi wa Ramadhani Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa tisa katika miezi ya mwezi muandamo katika kalenda ya Kiislamu. Ni mwezi bora zaidi katika mwaka. Allah ameuhusisha peke yake kuliko miezi mingine kwa sifa nyingi bora na za kipekee, na miongoni sifa hizo bora ni hizi: Kwamba Ramadhan ni mwezi ambao Allah ameuhusisha na kushuka kwa Qur’ani kitabu kitukufu na bora kuliko vitabu vyote. Allah Mtukufu amesema kuwa: «Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani ikiwa ni muongozo kwa watu, na hoja zilizo wazi za muongozo na upambanuzi. Basi atakayekuwa mjini miongoni mwenu katika mwezi huu, basi afunge». (Sura Albaqara, aya 185) Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Utakapoingia mwezi wa Ramadhani milango ya pepo hufunguliwa, na milango ya Jahanamu hufungwa, na mashetani hufungwa minyororo». (Bukhari, Hadithi Na. 3103, Muslim, Hadithi Na. 1079). Hakika Allah ameuandaa mwezi huu kwa waja wake ili waelekee kwake kwa kufanya ibada na kuacha maovu. Kwamba mwenye kufunga mchana wa Ramadhani na akasimama usiku wake (kwa kuswali), Allah humsamehe madhambi yake yaliyopita. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Mwenye kufunga Ramadhani kwa kuamini na kutaraji kupata malipo ya Allah, husamehewa madhambi yake yaliyopita». (Bukhari, Hadithi Na. 1910, Muslim, Hadithi Na. 760). Pia Mtume amesema kuwa: «Mwenye kusimama (kwa kuswali) katika Ramadhani kwa kuamini na kutaraji kupata malipo ya Allah, husamehewa madhambi yake yaliyopita». (Bukhari, hadithi na. 1905, Muslim, Hadithi Na. 759). Kwamba ndani ya mwezi wa Ramadhani kuna usiku wenye hadhi kubwa (Lailatul Qadri), usiku ambao ni bora sana kuliko nyakati nyingine za usiku za mwaka mzima. Allah ameeleza katika kitabu chake kwamba kufanya jambo jema ndani ya usiku huo ni bora zaidi kiliko kulifanya jema hilo siku nyingi nyingine. Allah amesema kuwa: «Lailatulqadri ni bora zaidi kuliko miezi elfu moja». (Sura Alqadri, aya 3). Mwenye kusimama katika usiku huo kwa kuamini na kutaraji kupata malipo ya Allah husamehewa madhambi yake. Huo ni usiku uliopo katika siku kumi za mwisho katika mwezi wa Ramadhani, na hakuna yeyote anayejua tarehe yake kwa uhakika. Ubora wa kufunga «Ambaye hakuacha kusema uzushi na kuutumia hakuna haja kwa Allah katika kuacha chakula chake na kinywaji chake». Kufunga kuna fadhila nyingi ambazo zimeelezwa katika sheria. Miongoni mwazo ni hizi zifuatazo: Kwamba mwenye kufunga mwezi wa Ramadhani kwa kumuamini Allah, kutii amri zake, kuamini fadhila zake zilizotajwa na sheria na kuwa na matarajio ya kupata thawabu kwa Allah, atasamehewa madhambi yake yaliyopita. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Mwenye kufunga Ramadhan kwa kuamini kutaraji kupata malipo ya Allah, husamehewa madhambi yake yaliyopita». (Bukhari, Hadithi Na. 1910, Muslim, Hadithi Na. 760). Pia mwenye kufunga atafurahia malipo atakayoyapata wakati wa kukutana na Mola wake kwa sababu ya funga yake. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Mwenye kufunga ana furaha mbili: furaha wakati wa kufungua kwake na furaha wakati wa kukutana na Mola wake». (Bukhari, Hadithi Na. 1805, Muslim, Hadithi Na.1151) Peponi kuna mlango unaoitwa Arrayaan. Haingii yeyote kupitia mlango huo isipokuwa tu wenye kufunga. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Hakika, peponi kuna mlango unaoitwa Arrayyaan. Wenye kufunga wataingia kupitia mlango huo Siku ya Kiama. Haingii yeyote kupitia mlango huo ila wao tu. Patatolewa tangazo kwamba: Wako wapi wenye kufunga? Watasimama. Hataingia yeyote kupitia mlango huo isipokuwa wao tu. Wakishaingia, utafungwa na hataingia yeyote kupitia hapo». (Bukhari, hadithi Na. 1797, Muslim, Hadithi na. 1152) Pia Allah ameyahusisha kwake yeye tu malipo na thawabu za mfungaji. Ikiwa malipo ya mtu yanatoka kwa Mkarimu, Mtukufu, Mtoaji sana na Rahimu sana, anatakiwa ayafurahie yale ambayo Allah amemuandalia. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, katika Hadithi Qudsiy amesema kuwa: «Matendo yote ya mwanadamu ni yake yeye isipokuwa funga. Funga ni yangu, na mimi ndiye nitakaye itolea malipo». (Bukhari, Hadithi Na. 1805, Muslim, Hadithi Na.1151) Hekima ya funga Allah amefaradhisha kufunga Ramadhani kwa hekima nyingi na faida mbali mbali katika dini na dunia, na miongonimwazo ni hizi: Kuthibitisha kumtii Allah na kumuogopa. Hiyo kutokana na kuwa funga ni ibada ambayo mja anajiweka karibu ya Allah kupitia ibada hiyo kwa kuacha anavyo vipenda, na kuyazuia mataminio yake. Anaidhibti nafsi yake kwa kumcha Allah na kumuogopa kila sehemu na kila wakati, katika siri na katika dhahiri. Kwa sababu hii, Allah Mtukufu anasema kuwa: «Enyi mlio amini, mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa waliokuwepo kabla yenu ili mpate kuwa wenye kumuogopa Allah». (Sura Albaqara, aya 183) Mazoezi ya kuacha maasi na madhambi Mwenye kufunga ajizuiapo kufanya mambo yaliyo halali kwa kufuata amri ya Allah atakuwa na uwezo zaidi wa kuyadhibiti mataminio yake ya kutaka kufanya maasi na madhambi, atachunga mipaka ya Allah na hatajiachia katika kufanya maovu. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Mtu ambaye haachi kusema uzushi na kuufanyia kazi, basi Allah hana haja ya kuacha chakula chake na kinywaji chake». (Bukhari, Hadithi Na. 1804). Maana ni kwamba: Mtu ambaye haachi uongo na kufanya uchafu katika kauli na vitendo, huyo hajayafikia makusudio ya funga. Kuwakumbuka wenye shida na kuwasaidia Hiyo inatokana na kwamba katika funga kuna mazoezi ya kupambana na ukata, njaa, na kuwakumbuka maskini ambao wanapambana na hali ya kutokuwa na pato la kutosha siku zote. Kwa kufunga, mja huwakumbuka ndugu zake masikini na namna wanavyoteseka na mambo mawili machungu; njaa na kiu, na kwa sababu hiyo, atafanya juhudi ya kuwasaidia na kuwafariji.

Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1