Ni ipi hali ya watu wa fatrah (kipindi baina ya mitume miwili) ambao hawakujua kuhusu Uislamu? Jee watakwenda motoni kwa vile walikufa bila ya Imani?
Fatrah maana yake ni kusimama na kupitiwa na muda ndani ya kipindi fulani. Kama neno la kidini, linamaanisha kipindi (muda) baina ya mitume wawili.
Katika hadithi iliyosimuliwa na Bukhari, fatrah maana yake ni kipindi (muda) baina ya mtume Issa na mtume Muhammad (rehma na Amani ziwe juu yao). (1)
Inafahamika katika baadhi ya aya kwamba Waarabu kabla ya Uislamu walikuwa na ufahamu mdogo juu ya mitume waliotumwa kwa watu. Katika Qur’an, imetajwa kwamba Waarabu waabudu masanamu walisema: “…Lau angelitaka Mola wetu mlezi (Kututumia mitume kutuonya) bila ya shaka angeli wateremsha malaika”. (2) na hivyo basi inaelezwa jinsi gani walivyokuwa na uelewa mdogo kuhusu Utume na pia kuhusu dini za haki.
Ingawa Waarabu walijua kuwa Mtume Ibarahim alikuwa ni mtume, walijua kuwa utume wake uliishia katika wakati wake, Kutokana na kipindi kirefu cha miaka elfu tatu (3000) baina ya Mtume Ibrahim na Mtume Muhammad (rehma na Amani ziwe juu yao), si wengi waliojua usafi (Hanif) wa dini aliyokuja nayo Mtume Ibrahim.
Wasomi wa Kiislamu wanawajadili watu wa fatrah (wale walioishi kwenye nyakati baina ya mitume wawili) kwa kuwagawa kwenye makundi matatu:
1. Wale waliojiridhisha na kukubali uwepo na umoja wa Allah kwa msaada wa hoja na uwezo wa akili zao kama vile Qus bin Saida na Zayd bin Amr, baba wa Said bin Zayd ambaye alibashiriwa pepo, n.k.
2. Wale walioingilia kwa kuiharibu na wakaibadili Imani ya Mungu mmoja, wakakubali ibada za masanamu pamoja na wale waliovumbua dini kwa matashi yao na wakawakusanya watu waliowazunguka kuwashawishi: akiwemo Amr bin Luhay, ambaye alianzisha ibada za masanamu kwa Waarabu na waabudu masanamu wengine, n.k.
3. Wale ambao hawakujiingiza ima kwenye Imani sahihi au Imani potofu, ambao hawakuwa waumini wala hawakuwa waabudu masanamu, na ambao waliyapitisha maisha yao kwenye ujinga, na ambao hawakuwahi kufikiri kuhusu mambo haya. Kwenye kipindi cha ujinga (kipindi cha ujinga kabla ya ujio wa Mtume) kulikuwa na watu wa aina hiyo pia.
Katika makundi haya matatu, kundi la pili litakwenda motoni kwasababu walikuwa waabudu masanamu. Wale wanaoangukia katika kundi la tatu hawatoingia motoni kwasababu ndio hasa watu wa kipindi cha fatrah. Hii ni kwasababu mtume ambaye angewalingania kwenye dini sahihi na ya kweli hakuwafikia na hawakuonesha ishara za kutokuamini; na kwa hiyo walikuwa miongoni mwa waliosalimika. Wanazuoni wote wa sunnah (Ahl As-Sunnah - kundi lenye wafuasi wengi) wamekubaliana kwenye hili. (3)
Qus bin Saida na Zayd bin Amr waliotajwa kwenye kundi la kwanza, kwa upande mwengine, watafufuliwa na Allah siku ya Kiama kama ni ummah tofauti (jamii), kwa vile wao waliamini uwepo na umoja wa Allah kati ya maelfu ya watu waliokuwepo kipindi hicho, na hawakuwa watu wa mtume yoyote kwasababu hakukuwa na mtume aliyetumwa kwao, na hawakufika kipindi cha Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake). Wao ni watu walionusurukia na wakaokoa maisha yao ya milele kwasababu ya Imani zao. Watakapofufuliwa, watakuwepo uwanja wa makusanyo siku ya hukumu kama “jamii ya mtu mmoja”. Watu hawa ni “wa kipekee” watafunikwa na rehma na huruma za Allah.
Ni Dhahiri kwamba watu wa fatrah hawahusiki na ibada pamoja na amri za kidini. Ingawa, kuna mgongano kati ya madhehebu mawili ya watu wa Sunnah (Ahl as-Sunnah), Maturidi na Ash’ari, kwamba jee walipaswa kuamini au laa. Kwa mujibu wa Imani ya dhehebu la Maturidi, watu hao walipaswa kutumia hoja na uwezo wa akili walioruzukiwa na Allah ili uwafikishe katika kufahamu uwepo wa Allah kwa kutathmini umbile la mbingu na ardhi na kila kilichomo. Kwa mujibu wa Ash’ari, kwa upande mwengine, watu wa fatrah hawalazimishwi kumuamini Allah. Na hii ni kutokana na hali ya kutokuletewa mtume. Allah anasema katika Qur’an: “…Wala Sisi hatuadhibu (mtu au jamii kwa makosa waliyofanya) mpaka tumpeleke Mtume.” (4) Hivyo basi, hawastahili kuadhibiwa kwasababu hawakupelekewa mtume.
Badiuzzaman, mwanachuoni wa Kiislamu ambaye aliishi na kuchapisha kazi kadhaa karne ya ishirini (20), anaileta aya iliyotajwa kama ushahidi na anasema:
“Watu walioishi kipindi baina ya mitume wawili ni miongoni mwa waliosalimika. Imetajwa kwamba hawatoadhibiwa kwa makosa yao kwenye mambo ambayo si ya msingi. Kwa mujibu wa Imam Shafi'i na Imam Ash'ari, wanasema kwamba hata kama si waumini na hawakuamini misingi ya Imani, bado watakuwa ni wenye kusalimika. Wajibu mbele ya Allah huwepo pale anapopeleka mitume, na mitume wakishaletwa, kuwajibika huanza kupitia elimu ya ujumbe wao. Kwavile kutokujali na kupita kwa muda mrefu kuliwafanya wasijue misingi ya dini ya mitume waliotangulia hawakuweza kutoa ushahidi kwa watu wa kipindi hicho. Kama watatii mfumo wa maisha uliotangulia, watapata malipo; na kama hawakufuata, hawatoadhibiwa. Na kwa msingi huo basi, kwa vile mfumo wa maisha ulifichika, hauwezi kuwa uthibitisho.” (5)
Imam Ghazali, Mwanachuoni wa Kiislamu muhimu, anawagawa watu baada u utume wa Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) katika makundi matatu makubwa:
1. Wale ambao hawakusikia kuhusu ujumbe wa Mtume na hawakupata taarifa kuhusu Mtume. Wale watakaoangukia kwenye kundi hili ni watu waliosalimika na wataingia peopni.
2. Wale ambao walisikia kuhusu ujumbe wa Mtume, na miujiza aliyokuja nayo, tabia zake zilizotukuka, lakini hawakumuamini Mtume. Kundi hili bila shaka yoyote litaangamia na litapata adhabu iumizayo.
3. Wale ambao walilisikia jina la Mtume, lakini hawakusikia chochote zaidi ya propaganda chafu, na hakuna yoyote aliyewaeleza ukweli na kuwatia moyo kwenye Imani thabiti; kwa sababu hizi, wanabaki katikati. Na natumai kwamba nao watakuwa miongoni mwa watu waliosalimika na hivyo basi wataingia peponi.
Mwanachuoni Badiuzzaman, ambaye anaeleza kwamba mwisho wa zama, watatokea pia watu wa fatrah, na anaelezea kwamba aina hiyo ya watu wasio na hatia ambao hufa katika vita vya dunia nao pia watakuwa watu waliosalimika. Badiuzzaman anasema:
“Katika zama za mwisho (akhir zaman), kutaibuka dini na dini ya Muhammad (rehma na Amani ziwe juu yake) itakuwa kama joho fulani tofauti litakalo akisi aina fulani ya fatrah, na katika zama za mwisho kabisa dini sahihi ya Nabii Issa (Yesu) itatawala na kuwa bega kwa bega na Uislamu. Kwa sababu zote hizi, bila shaka majanga waliyoyapata Wakristo ambao walimfuata Nabii Issa (Yesu) ni aina ya mateso kwao.” (6)
Marejeleo
1. Bukhari, Manaqibu'l-Ansar: 53.
2. Qur’an, Fussilat , 14.
3. Tajrid-i Sarih trns, 4:544.
4. Qur’an, Isra, 15.
5. Barua za (Mektubat), 360-361.
6. Kastamonu Lahikası, p. 77.
2. Qur’an, Fussilat , 14.
3. Tajrid-i Sarih trns, 4:544.
4. Qur’an, Isra, 15.
5. Barua za (Mektubat), 360-361.
6. Kastamonu Lahikası, p. 77.

Comments
Post a Comment