Mtunze Mke Wako KATIKA hili
Mtunze Mke Wako
Mume na mke kila mara huhitaji ushirikiano wa kila mmoja wao na kuonesha mapenzi kwa kila mmoja. Hata hivyo, haja hili huwa kubwa zaidi wakati wa ugonjwa na matukio mengine yanayo fanana na hilo. Mtu mgonjwa, kama vile anavyohitaji daktari na dawa, huhitaji matunzo na uangalizi wenye mapenzi. Muuguzi mzuri humsaidia mgonjwa kupona vizuri na haraka.
Mwanamke pia hutegemea mume wake kumtunza yeye wakati anaugua na kulala kitandani. Mke anatarajia mume kumtunza yeye zaidi ya wazazi wake.
Mwanamke anaye fanya kazi nyumbani kama mtumishi wa nyumbani anastahili uangalizi ulio na mapenzi kutoka kwa mume wake. Anatarajia kwamba ni haki yake mume wake amuuguze.
Malipo ya tiba na dawa ni mojawapo ya matumizi ya kawaida ya maisha na mwanaume anao wajibu wa kumpa fedha hizo muhimu. Mwanamke anayefanya kazi nyumbani bila mshahara wowote, hakika anayo haki ya kumtarajia mume wake kulipa gharama ya tiba yake.
Wapo wanaume ambao hawana aibu kufanya isivyo haki. Huwatumia wake zao wakati wana afya njema na wenye uwezo, lakini hukataa kulipa fedha wanapo ugua. Fedha yoyote ndogo wanayotumia kwa ajili ya tiba ya wake zao huilalamikia sana. Baadhi ya wanaume, wakiona gharama ya tiba ni kubwa wanaweza hata kuwaacha wake zao. Tabia hii ni sawa kweli? Mwanamke mmoja alikuwa analalamika kuhusu mume wake. Alisema: “Nilikuwa nafanya kazi kwa bidii nyumbani na nilipita kwenye nyakati nyingi za furaha na shida na mume wangu. Hata hivyo, sasa nimeugua, mume wangu anataka kuniacha!”
Bwana mpendwa! Kama unapenda kuwa na furaha na maendeleo ya familia yako, lazima umpeleke mkeo kwa daktari anapougua. Lazima ulipe gharama ya matibabu yake. Zaidi ya hapo, lazima umuuguze kwa wema. Sasa amewaacha wazazi wake ili aishi na wewe, anatarajia wewe kuwa na mapenzi zaidi kwake kuliko wazazi wake. Yeye ni mwenzako na mama wa watoto wako! Mhurumie na mpe matumaini ya kupona haraka. Mpikie chakula. Tayarisha chakula kinachofaa na nunua vifaa vilivyoelekezwa. Mlishe chakula. Yote haya yatamfanya mke wako afurahi.
Wanyamazishe watoto. Uwe mwangalifu wakati wa usiku. Wakati wowote akiamka muulize hali yake anavyojisikia. Kama hawezi kulala kwa sababu ya maumivu, basi na wewe uwe macho. Unaweza hata kuwaambia watoto wenu wakusaidie kumwangalia mama yao. Usimwache hata kidogo mke wako bila huduma, hasa zaidi anapokuwa anaumwa. Wakati kama huo, mke wako ataona mapenzi yako na yeye atakupenda zaidi. Atajivuna kwa sababu hiyo na atakuwa tayari kukuhudumia wewe na watoto zaidi, mara atakapo pona.
Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mtu mzuri zaidi miongoni mwenu ni yule ambaye ni mwema zaidi kwa familia yake, na mimi ni mwema kuliko wote kwa familia yangu.”
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu pia alisema: “Yeyote anayefanya jitihada kutambua haja ya mgonjwa, dhambi zake zitasamehewa, na atakuwa kama siku aliyozaliwa.” Mmoja wa maansari (wenyeji wa Madina) aliuliza: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wazazi wangu na watolewe muhanga kwa ajili yako, ni vipi endapo mgonjwa anatoka miongoni mwa familia yako- Ahlul –bait? Hakuna thawabu nyingi zaidi katika mfano huu?”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alijibu: “Ndio.”
Uchumi Wa Familia
Kufanya mpango wa sadaka ya mke ni wajibu wa mume. Ni kwamba mwanaume anawajibika kulipa gharama za mke wake kama chakula, nguo, nyumba, daktari na dawa. Atakuwa anakosea kama hata mgharimia mke wake na anaweza kushitakiwa kisheria.
Mtu hawezi kutarajia familia iishi bila matumizi yeyote ya fedha. Watu wa familia wote wanahitaji chakula, nguo, dawa na mahali pa kuishi. Hata hivyo, wanaweza wakaomba vitu visivyo muhimu ambavyo mwanaume anaweza kukataa kuvinunua na asikubaliane na matakwa yao mbali mbali.
Mtu mwenye busara atatumia fedha kufuatana na uwezo wa kipato chake. Lazima abainishe bidhaa muhimu na avinunue katika mpango wa kipaumbele wakati wowote anapoweza. Lazima pia aweke akiba ya fedha kwa matumizi ya siku za shida. Kiasi fulani cha fedha lazima kitengwe kwa ajili ya kodi ya nyumba au kununua mahali pengine. Lazima mume asisahahu umeme, maji, nishati na simu. Kodi na ada za shule lazima zikumbukwe. Lazima kabisa aepukane na kutumia zaidi ya bajeti na kulipa vitu visivyo muhimu. Mpango mzuri wa matumizi ya fedha utamwepusha mtu asifilisike au kuwa na madeni.
Mwenyezi Mungu huona matumizi yaliyopangwa vizuri ni ishara ya imani na anasema ndani ya Qurani:
وَالَّذِينَ إِذَا أَنْفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامًا
{67}
“Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili bali wanakuwa katikati baina ya hayo”. ( Quran 25:67).
Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Yapo makundi manne ya watu ambao sala zao hazitafika kiwango cha kukubaliwa; Kundi moja ni la watu ambao hutumia vibaya utajiri halafu humwomba Mwenyezi Mungu Mweza, ‘Ee Mwenyezi Mungu naomba riziki. Halafu Mwenyezi Mungu hujibu, si nilikuagiza uwe mwangalifu katika matumizi yako. ’ ”
Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Yapo makundi manne ya watu ambao sala zao hazitafika kiwango cha kukubaliwa; Kundi moja ni la watu ambao hutumia vibaya utajiri halafu humwomba Mwenyezi Mungu Mweza, ‘Ee Mwenyezi Mungu naomba riziki. Halafu Mwenyezi Mungu hujibu, si nilikuagiza uwe mwangalifu katika matumizi yako. ’ ”
Abdullah bin Aban anasema: “Nilimuuliza Musa bin Jafar (a.s) kuhusu utunzaji wa familia ya mtu na akasema: ‘Ubadhilifu na uchoyo vyote ni sifa mbaya. Mtu lazima awe na kiasi.”
Mtu mwenye busara ataepuka kukopa fedha na hawezi kuchukua mkopo kwa matumizi mabaya. Uchumi unaotegemea mikopo (na riba), inayopokewa kutoka kwenye mabenki na taasisi zingine si sahihi kiislamu na kimantiki haufai.
Kununua vitu kwa mkopo, ingawa hufanya nyumba yako ionekane nzuri, lakini faraja na utulivu wa akili hutoweka.
Kwa nini mtu ananunua vitu visivyo muhimu kwa bei ya juu zaidi na kujaza mifuko ya wenye mabenki kwa malipo kidogo? Ni maisha ya aina gani hayo ambapo kila kitu hupatikana kwa bei ya mkopo? Kwani si vema zaidi kwa mtu kungoja na kuweka akiba ili anunue bidhaa kwa bei nafuu?
Ni kweli kwamba kupata fedha ni vigumu na huathiri sana maisha ya mtu. Hata hivyo, la muhimu zaidi ni jinsi mtu anavyotumia fedha yake. Zipo familia zenye vipato vizuri ambazo kila mara ni wadeni wa wengine. Zipo pia familia nyingi zenye vipato vya chini ambao huishi kwa raha. Tofauti baina ya makundi haya mawili ni jinsi ya fedha inavyo tumiwa. Kwa hiyo, inafaa zaidi ama mwanaume aendeshe udhibiti wa matumizi au awe msimamizi wa mtu ambaye anawajibika nayo.
Mwisho, inakumbushwa kwamba ubakhili ni mbaya kama ufujaji, kama mwanaume anacho kipato zaidi lazima aifurahishe familia yake zaidi na kuwapa mahitaji yao muhimu kadiri iwezekanavyo.
Utajiri na fedha vyote ni vya kutumia na kuwezesha upatikanaji wa vitu muhimu vya maisha, na si vya kulundika na kuviacha hapa duniani.
Ishara za utajiri lazima zionekane wazi kwenye familia ya mtu na nyumba. Kuna manufaa gani kufanya kazi kwa bidii halafu kinachopatikana kisitumike?
Mtu mzima atumie utajiri kuhusu familia yake na starehe yake mwenyewe. Inachukiza kuona mtu ambaye anao uwezo wa kifedha lakini watoto wake wanatamaani chakula kizuri na nguo nzuri. Watoto wa mtu bakhili kungoja kifo chake ili wagawane utajiri wake. Kama Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anampa mtu neema zake, neema hizi lazima zidhihiri katika maisha ya mtu huyo.
Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema: “Si mwenzetu (si mfuasi wa Mtume s.a.w.w) ambaye anazo fedha lakini huiweka familia yake mbali na utajiri wake.”
Musa bin Jafar (a.s) alisema: Jamaa ya mtu ni watu wanaomtegemea. Hivyo, yeyote anayepewa neema za Mwenyezi Mungu, lazima azisambaze kwa wale wanao mtegemea ili wafarijike, au vinginevyo neema hizo zitaondoshwa kwake.”
Imamu Rida (a.s) alisema: “Ni jambo la manufaa kwa mtu kuwapa watu wa familia yake starehe itokanayo na matumizi yake, ili wasingoje hadi hapo atakapofikwa na mauti.”
Imamu Ali (a.s) alisema: “Tayarisha matunda kwa ajili ya watu wanaokutegemea kila siku ya Ijumaa ili kwamba watafurahia kuja kwa Ijumaa.”
Saidia Kufanya Kazi Za Nyumbani
Licha ya kwamba utunzaji wa nyumba ni wajibu wa wanawake, lazima ieleweke kwamba kuendesha mambo ya nyumbani si kazi rahisi.
Mke ambaye ni mama wa nyumbani hata akitumia muda kiasi chochote kile kwa utunzaji wa nyumba, hatoweza kumaliza kazi hiyo yote kwa wakati moja. Hii ni kweli hasa zaidi pale ambapo anatakiwa kuwakirimu wageni au anapougua na kadhalika. Kazi ya kutunza nyumba humchosha mke wa nyumbani na hivyo wanaume wanatarajiwa kuwasaidia wake zao katika suala hili.
Si haki kwamba mwanamume awe amekaa nyumbani bila ya shughuli yoyote ambapo mke wake anashughulika na kazi nyingi mbali mbali. Inafaa tu mume kumsaidia mke wake kadiri iwezekanavyo na wakati wowote awezapo. Msaada huu ni ishara ya huba ambayo humvutia mke kwa mume wake na familia yake.
Si ujasiri wa kiume hata kidogo kwamba mwanaume hapaswi kugusa kitu chochote ndani ya nyumba, bali kutoa amri tu kumpa mkewe. Nyumba ya familia si makao makuu ya kutoa amri, isipokuwa hapo ni mahali pa upendo, wema na ushirikiano.
Bwana mpendwa! Usidhani kwamba wewe ukifanya kazi za nyumbani ni kushusha hadhi yako. Kinyume chake ni kwamba, mke wako atapendezwa sana na kitendo chake cha kumsaidia.
Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu ambaye ni mtu anaye heshimiwa sana katika historia, alikuwa na desturi ya kusaidia kazi za nyumbani.
Ayisha, mke wa Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wakati wowote Mtume
(s.a.w.w) anapokuwa hana kazi, alikuwa na desturi ya kushona nguo zake, kutengeneza viatu vyake na alikuwa anafanya kazi nyumbani kama wanaume wengine.”
Rudi Nyumbani Mapema
Mwanaume asiye na mke anao uhuru wa kutumia muda wake, lakini pindi anapooa, lazima abadilishe mpango wake. Hawezi kukaa nje kwa muda wowote anaotaka. Anatakiwa kumtaarifu mke wake mahali alipo na kadhalika. Lazima asisahau kwamba mke wake huwepo nyumbani siku nzima, husafisha nyumba, huosha vyombo na hupika. Humngoja arudi nyumbani mara tu anapomaliza kazi zake, ili amuone, azungumze naye na kufurahia kuwa naye.
Watoto pia huwa na matumaini ya kumuona baba yao. Si haki kwamba mwanaume aache familia yake nyumbani na yeye afuate starehe zake mahali pengine.
Ndoa si tu kulisha chakula na kuimvisha nguo familia yako. Mwanamke ni mwenza wa mume wake na si mtumishi. Mke hayupo pale kwa ajili ya kufanya kazi mchana kutwa na kulishwa chakula lakini hasa zaidi anayo matarajio ya kuwa na rafiki wa kudumu na mwenza.
Baadhi ya wanaume kwa kweli hawafanyi sawa, hawana haki na wapumbavu. Huwaacha wake zao na watoto wao nyumbani na kutumia muda wa usiku kucha mahali pengine. Fedha ambayo wangetumia na familia nyumbani, anaipoteza mahali pengine.
Wanaume wa aina hii bado hawajaelewa maana ya mapenzi na huba na huona starehe zao zisizo na thamani na chafu kama ndio njia ya maisha mazuri. Hawatilii manani ukweli kwamba vitendo kama hivyo huwadhalilisha. Wengine hutambua vitendo kama hivyo kuwa vya kipumbavu na kijeuri.
Wanaume wa aina hii ni sababu ya huzuni kwa wenyewe na familia zao. Matendo yao huwashawishi wake zao kudai talaka kutoka kwao.
Mwanaume ambaye alimtaliki mke wake, alisema mahakamani: “Mwanzoni mwa ndoa yangu, nilikuwa na marafiki fulani ambao nilikuwa nikitoka nao kwa matambezi, ambapo humwacha mke wangu nyumbani… na nilikuwa na desturi ya kurudi nyumbani kesho yake alfajiri. Mke wangu ambaye alichoshwa na hali hii, alipewa talaka.
Tulikuwa na watoto kumi, ambao nilitaka kukutana nao mara mbili kwa mwezi. Kipindi fulani kilipita tukitekeleza mpango huu. Lakini sasa ni muda mrefu tangu watoto wangu wajifiche na ninayo shauku kubwa kuwaona watoto wangu.”
Mwanamke alisema; “Nimekata tamaa kwa upweke. Mume wangu hajali kabisa kuhusu mimi. Kwa ajili ya starehe zake huwa nje hadi asubuhi sana.”
Bwana mpendwa! Sasa umeoa. Usiendekeze tabia ya kikapera. Wewe unawajibika kwa mke wako na watoto wako, acha kushirikiana na marafiki wasiofaa rudi nyumbani mara unapomaliza kazi yako. Furahia maisha ya familia na mke wako na watoto wako. Hata kama starehe zako za kila siku usiku si zenye uovu, hata hivyo, zinaweza kusababisha madhara kwako na maisha yako ya ndoa.
Comments
Post a Comment