Mpende Mkeo ; Soma hii ewe muislam uliye ndani ya ndoa itakusaidia
Mwanamke ni kituo cha wema na ni kiumbe chenye hisia kubwa sana. Kuwepo kwake hutegemea huruma na upendo. Huwa na shauku ya kupendwa na wengine na jinsi anavyopendwa zaidi ndivyo anavyofurahi zaidi. Hujitolea sana ili apendwe na wengi. Tabia hii ina nguvu sana ndani mwake hivyo kwamba akigundua kwamba hakuna mtu anaye mpenda, basi atajitambua kama ameshindwa. Atakasirika na atahisi kuvunjika moyo.
Kwa hiyo, kwa hakika mtu anaweza kudai kwamba siri ya mwanamume aliyefuzu katika maisha ya furaha ya ndoa ni jinsi anavyo onesha mapenzi kwa mke wake.
Bwana mpendwa! Mke wako kabla ya kuolewa na wewe, alikuwa anafaidi mapenzi ya wazazi wake na wema wa wazazi wake. Sasa ameingia kwenye mkataba wa ndoa na wewe na sasa amechagua kuishi na wewe katika maisha yake yote, anatarajia wewe umtimizie matakwa yake ya mapenzi na huba. Anatazamia wewe kuonyesha mapenzi zaidi kwake kuliko alivyopokea kutoka kwa wazazi wake na marafiki zake. Amekuamini wewe sana na ndio sababu amekupa udhamini wa maisha yake.
Siri ya ndoa yenye furaha hutegemea jinsi unavyodhihirisha mapenzi yako kwa mkeo.
Ukitaka kuuvutia moyo wake, ukitaka awe mtiifu kuhusu matakwa yako kama kuimarisha ndoa yenu, ukitaka mkeo akupende wewe, au adumishe uaminifu kuliko au… basi lazima kila mara uoneshe mapenzi na huba yako kwake.
Usipokuwa mwema kwa mke wako, basi anaweza kupoteza mvuto kwenye nyumba yake, halikadhalika na watoto pia. Na zaidi ya yote kwako wewe mwenyewe. Wakati wote nyumba yako itakuwa katika hali machafuko. Hatakuwa tayari kufanya juhudi kwa ajili ya mtu asiyempenda.
Nyumba ambayo ndani yake haina mapenzi, hufanana na jahanamu inayowaka moto, hata kama ni nadhifu sana na iliyojaa vitu vya anasa.
Mke wako anaweza kuugua au kupatwa na mfadhaiko. Anaweza kutafuta kupendwa na wengine kama hatoshelezwi na wewe. Anaweza asikuthamini wewe na nyumba yako pia, kiasi kwamba anaweza hata kuomba talaka!
Unawajibika kwa yote haya kwa sababu umeshindwa kumtosheleza mkeo. Kwa hakika ni kweli kwamba taratibu zingine za kutalikiana hutokea kwa sababu ya ukatili wa mume au kinyume chake.
Angalia takwimu zifuatazo. Mahitaji ya saikolojia ya mapenzi, uzembe wa waume kuhusu matakwa ya wake zao na kutokuzingatia umuhimu wa hadhi ya kiakili ya wanawake, ni vipengele ambavyo vimekuwa sababu ya kesi nyingi za kutalikiana.
Mnamo mwaka 1969 miongoni mwa kesi za kutengana 10372, katika kesi 1203 wanawake walionesha sababu ya kutaka kutalikiana kuwa ni kuvunjwa moyo kimaisha, kujihisi hathaminiwi na upungufu wa waume kutokujali matakwa na hisia kubwa za wake zao.” 146
Mwanamke alisema mahakamani; “Nipo tayari kuacha mahari yangu na hata kumlipa mume wangu fedha ili akubali kunipa talaka. Mume wangu anawapenda zaidi kasuku wake ndio sababu sitaki kuishi naye zaidi ya sasa.”
Mapenzi na urafiki wa familia ni thamani kubwa zaidi kuliko chochote na ndio sababu Mwenyezi Mungu ameiona hiyo kama mojawapo ya alama za uwezo na neema kubwa ambayo mwanadamu amepewa. Qurani Tukufu inasema:
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ {21}
“Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wenza kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri (Quran 30:21).”
Imamu Sadiq (a.s) alisema: Yeyote ambaye ni rafiki yetu huonesha wema zaidi kwa mke wake.”
Imamu Sadiq (a.s) alisema: Yeyote ambaye ni rafiki yetu huonesha wema zaidi kwa mke wake.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Jinsi mtu anavyozidi kuwa mwaminifu ndivyo anavyozidi kuonesha wema kwa mke wake.”
Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Mmojawapo ya sifa bainifu ya Mitume wa Mwenyezi Mungu ni kwamba wote ni wema kwa wake zao.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Maneno ya mwanaume anaye mwambia mke wake; ‘Ninakupenda kweli’ kamwe hayaondoki moyoni mwake.”
Kama mambo yalivyo, mapenzi na huba lazima yawe halisi na kuvutia kwenye moyo wa mwingine, lakini hata kupenda sana kwa mtu haitoshi, kwa kuwa ni muhimu kuonesha huba. Kwa kuonesha hisia zako kwa maneno na vitendo vyako, mapenzi unayoonesha, yatapata jibu zuri kutoka kwa mkeo na nyoyo zenu zitaimarisha muungano wa mapenzi.
Uwe wazi na udhihirishe mapenzi yako kwako bila kusita. Wakati yupo au hayupo, msifie. Mwandikie barua unapokuwa safarini na mtaarifu kwamba kutokuwa karibu naye unajihisi mpweke sana. Mara kwa mara mnunulie kitu kama zawadi. Mpigie simu unapokuwa ofisini au shughuli zako na umuulize hali yake.
Kitu kimoja cha muhimu sana kwenye akili ya mwanamke ni namna hizi za kuonesha mapenzi kwake.
Bibi fulani wakati analia kwa masikitiko alisema. “Niliolewa na mume wangu usiku mmoja wa majira ya kupukutika kwa majani. Tuliishi pamoja kwa amani kwa muda fulani. Nilihisi kuwa nilikuwa mwanamke mwenye bahati kubwa sana hapa duniani. Niliishi kwenye nyumba yake ndogo kwa miaka sita. Nilihisi ninayo furaha mara mia moja nilipogundua kwamba nilikuwa mja mzito.
Nilipomtaarifu mume wangu alidondokwa na chozi la furaha wakati amenikumbatia mikononi mwake. Alilia sana hivyo kwamba karibu angeshindwa kujizuia. Halafu akatoka nje na akaninunulia mkufu wa almasi kwa fedha yake ya akiba. Alinipa mkufu na akasema: ‘Ninatoa hii kwa mwanamke bora kuliko wote ambao ninewaona hapa duniani.’ Lakini baada ya muda mfupi alikufa kwenye ajali ya gari.”
Mheshimu Mke Wako
Mwanamke hujivunia utu wake kama ilivyo kwa mwanamume. Anapenda kuheshimiwa na watu wengine. Ataumia sana kimawazo kama akitukanwa au kudhalilishwa. Hufurahi anapo heshimiwa na huwachukia wale wanaojaribu kushusha hadhi yake.
Bwana mpendwa kwa hakika mke wako anatarajia kuheshimiwa na wewe zaidi kuliko watu wengine. Anayo haki kumtarajia mpenzi wake wa maisha na rafiki mzuri zaidi ya wote kumtunza yeye. Mke wako kufanya kazi kwa ajili ya faraja yako na watoto wenu na kwa hiyo anakutarajia wewe kumthamini yeye na juhudi zake.
Kumheshimu mkeo si jambo la kukushusha hadhi yako ila kwa kweli itakuwa ni uthibitisho wa mapenzi na huba yako kwake. Kwa hiyo, mheshimu mkeo zaidi ya wengine na sema naye kwa upole. Usiingilie kati au kumkemea anapozungumza.
Mwite kwa majina ya heshima na uadilifu. Onyesha heshima yako anapotaka kuketi chini.
Unapoingia nyumbani, akisahau kusema ‘Salaamu aleyk’ (yaani kukusalimia), basi anza wewe kumsalimia kwa kusema ‘salaamu aleyka.’
Sema ‘kwa heri’ unapoondoka nyumbani. Usiache kuwasiliana naye unaposafiri au unapokuwa haupo nyumbani. Mwandikie barua.
Dhihirisha heshima yako kwake unapokuwa kwenye mikusanyiko. Kwa dhati kabisa, epuka kumtusi kwa namna yoyote na kumfedhehesha. Usitumie lugha chafu au hata kumchokoza kwa kumtania. Usidhani ya kwamba kwa sababu upo karibu naye sana kwa hiyo hatojali ukimtania. Kinyume chake ni kwamba atachukia msimamo wa aina hiyo bila kukuonesha ishara yoyote. Mwanamke mwenye hadhi mwenye umri wa miaka 35, anasema kuhusu ombi lake la talaka; Ni miaka 12 tangu nimeolewa. Mume wangu ni mwanamume mwema na zipo tabia nyingi za mtu mwema na mpole ndani mwake.
Lakini kamwe hajataka kutambua kwamba mimi ni mke wake na mama wa watoto wake. Yeye ana dhani kwamba ni mtu anayeweza kuchanganyikana na kuzoeana na watu bila taabu, lakini maonesho yake hayo kuyafanya kwa kunitania na kunidhalilisha. Huwezi kuamini ni kiasi gani nimeumia katika hisia zangu. Neva zangu zimeathiriwa sana hivyo kwamba imenibidi niende kupata ushauri kutoka kwa bingwa wa maradhi ya akili ili nipate tiba. Nimezungumza na mume wangu kuhusu jambo hili mara nyingi. Nimemwomba asinifanyie hivyo.
Nimemkumbusha kuhusu nafasi yangu kama ‘mke wake’ na umri wangu na kwamba si stahili yake kunitania mimi mbele ya watu wengine hadi wanacheka au wanafurahia kitendo hicho. Nina hisi kuaibika mbele ya kila mtu na kwa sababu sijawahi hata wakati mmoja kuwa mcheshi, siwezi kushindana naye. Kwa kuwa matakwa yangu hayatekelezwi na mume wangu, ninataka kutengana naye. Ninajua sitakuwa na furaha nikibaki peke yangu, lakini siwezi kuishi na mwanaume ambaye hushusha hadhi yangu kila wakati ..”
Wanawake wote huwa na matamanio ya kuheshimiwa na waume zao na wote huchukia fedheha. Kama wanawake wengine kunyamaza wakati waume zao wanawadhalilisha huo si uthibitisho wa kuridhika kwao na tabia hiyo.
Ukimheshimu mke wako, na yeye atafanya hivyo kwako na uhusiano wenu utazidi kuimarika. Wewe pia utapata heshima zaidi kutoka kwa watu wengine. Kama ukimtendea vibaya mke wako na yeye alipe kisasi, hili tena si kosa lake ni kosa lako.
Bwana mpendwa! Kuoa si sawa na kupata mtumwa. Huwezi kumtendea mtu aliye huru kama mtumwa. Mke wako amekubali kuolewa na wewe ili aishi na wewe na kugawana maisha yake na mtu ambaye anampenda. Anatazamia mambo kama hayo kutoka kwako kama vile unavyotarajia kutoka kwake. Kwa hiyo, mtendee kwa namna ambayo wewe ungependa kutendewa.
Imamu Sadiq (a.s) akimnukuu baba yake, alisema: “Yeyote anayeoa, lazima amheshimu mke wake.”
Mtume (s.a.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Mtu yeyote anaye mheshimu Mwislamu, Mwenyezi Mungu atampa heshima yake mwenyewe.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) pia alisema: “Hapana yeyote ambaye angewaheshimu wanawake isipokuwa watu wakarimu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akaongeza kwa kusema: “Mtu yeyote anaye tukana familia yake, atapoteza furaha katika maisha yake.”
Uwe Na Tabia Njema
Dunia huchukua mkondo wake kufuatana na mpangilio linganifu. Matukio hutokea na kujidhihirisha moja baada ya lingine. Kuwepo kwetu katika ulimwengu huu mpana ni kama chembe ndogo ilioko kwenye mwendo na kuathiri chembe nyingine papo hapo.
Uendeshaji wa dunia huu haupo katika uwezo wetu na matukio ya dunia hii hayatokei kufuatana na utashi wetu. Tangu hapo ambapo mtu hutoka nyumbani kwake asubuhi hadi hapo anaporudi jioni, inawezekana hukabiliana na mamia ya mambo yasiyofurahisha.
Mtu hukutana na matatizo mengi sana katika uwanja wa maisha. Inawezekana mtu akakutukana, na mfanyakazi mwenzake asiye rafiki, utangojea basi kwa muda mrefu mno, umeshutumiwa kwa sababu ya kitu fulani ofisini, umepoteza fedha, au umekabiliwa na tukio lolote ambalo linaweza kumtokea mtu mwingine yeyote popote.
Inawezekana ukakasirishwa sana na matukio ya kawaida ya kila siku katika maisha yako hivyo kwamba unafanana na bomu lililotegwa na kulipuka wakati wowote.
Vema, inawezekana ukadhani kwamba huwezi kuwalaumu watu wengine au dunia kwa sababu ya bahati yako mbaya, hivyo kwamba unaporudi nyumbani, unajaribu kutoa nje hasira yako kwa mke wako na watoto wako.
Unaingia nyumbani kwako kama vile ‘Ziraili’ (malaika wa kifo) amewasili. Watoto hutawanyika kama panya wadogo mbele yako. Mungu na apishe mbali kwamba uone kitu fulani kilicho kosewa! Chakula, ama inawezekana kina chumvi nyingi au hakina chumvi, au kikombe chako cha chai hakijawa tayari, inaewezekana nyumba chafu, au watoto wanapiga kelele na kwa hiyo unapata kisingizio cha kulipuka kwa hasira ndani ya nyumba yako.
Halafu unamkasirikia na kumpigia kelele kila mtu, unawatukana unawapiga watoto na kadhalika. Wakati huo utakuwa umeigeuza nyumba ya huba na urafiki kuwa jahanamu iwakayo moto ambamo wewe na familia yako mtateseka.
Kama watoto wanaweza kukimbia kutoka nyumbani na kwenda mitaani, watafanya hivyo, na kama hawawezi kufanya hivyo, basi watahesabu sekunde hadi hapo utakapoondoka nyumbani.
Inaeleweka dhahiri ni mazingira ya kusikitisha na kutisha yalioje yanayotawala familia za aina hii. Kila mara upo ugomvi na mabishano. Nyumba yao kila mara imevurugika. Mke anachukia kuona uso wa mume wake.
Mwanamke anawezaje kuishi kwa furaha na mwanamume mkali na mwenye hasira?
Baya zaidi kuliko yote ni hatima ya watoto ambao watakulia kwenye mazingira hayo. Ugomvi wa wazazi wao kwa hakika utatia kovu kwenye roho na nyoyo zao zilizo nyepesi kuhisi. Watoto wanao wanaopata matatizo kama haya huendeleza tabia ya kuwa aina ya watu wenye hasira, wagomvi wenye huzuni na kuona kila jambo ni baya wakati watakapofika umri a utu uzima. Hukatishwa tamaa kwenye familia yao na hukengeuka. Inawezekana wakakutana na mitego ya watu waovu na kuanza kufanya uhalifu wa aina mbali mbali. Inawezekana wakawa na tabia ngumu sana kuelezeka na kuvurugikiwa akili hivyo kwamba wanaweza kuhatarisha maisha ya watu wengine kwa kuua au kujiua.
Msomaji anashauriwa kufanya utafiti wa historia ya maisha ya wahalifu. Takwimu na taarifa za kila siku za matukio ya uhalifu yote yanaonesha ukweli huu.
Yote haya yapo kwenye wajibu wa mlezi wa familia ambaye ameshindwa kudhibiti tabia yake na ameitendea vibaya familia yake. Mtu kama huyu kamwe hawezi kuwa na amani katika dunia hii na ataadhibiwa akhera.
Mpendwa bwana! Hatuna nafasi na hatuwezi kudhibiti mambo ya dunia hii. Mabalaa, shida, na matukio ya kusikitisha yote ni mambo yanayo ambatana na maisha haya. Kila mtu hupata matatizo wakati mbali mbali. Ni ukweli wa mambo kwamba, mtu hufika kwenye umri wa balekhe kwa kukabiliana na taabu. Mtu lazima apambane nayo kwa nguvu na lazima ajaribu kutafuta ufumbuzi wake. Binadamu wanao uwezo wa kukabiliana na mamia na matatizo madogo na makubwa na bila kukata tamaa chini ya mbinyo wa balaa.
Matukio ya dunia si ndio tu sababu ya kutibuliwa kwetu, isipokuwa hasa zaidi ni mpangilio wetu wa neva ambao huathirika na matukio kama haya na husababisha sisi tukose furaha. Kwa hiyo, kama mtu angeweza kudhibiti hali wakati anapokabiliwa na matukio ya maisha yasiyofurahisha, hangekasirika na kuchukia.
Tudhani ya kwamba umepatwa na tukio lisilofurahisha. Tukio hili ama ni matukio ya kila siku yalioambatana na hali ambayo hatuna uwezo wa kuingilia au hatuwezi kusaidia. Au inawezekana tukio hili ni lile ambalo sisi tunaweza kufanya uamuzi wetu.
Ni dhahiri kwamba katika mfano wa kwanza, hasira yetu hainge saidia kwa njia yoyote. Tutakuwa tunakosea kukasirika au kuhamaki. Lazima tukumbuke kwamba sisi hatukusababisha kutokea kwa tukio hilo na hata tujaribu kulikaribisha kwa uso wenye furaha.
Lakini kama tatizo letu ni la mfano wa pili, basi tunaweza kutafuta ufumbuzi unaofaa.
Kama hatutakata tamaa tunapokabiliwa na shida na kujaribu kujizuia, kwa kutumia busara, tunaweza kuyashinda matatizo yetu. Kwa njia hii hatuta kimbilia hasira ambayo inaweza kuwa tatizo juu ya tatizo.
Tunao uwezo wa kushinda matatizo yote kwa kutumia uvumilizu na hekima. Hivi si jambo la kusikitisha kwamba tunashindwa kudhibiti mambo yanayotokana na matukio yasioepukika maisha?
Zaidi ya haya kwa nini umlaumu mke na watoto wako kwa mabalaa yako? Mke wako anatekeleza mgawo wa wajibu wake. Anatakiwa kutunza nyumba na watoto. Anatakiwa kufua, kupika, kunyoosha pasi kufanya usafi na kadhalika. Unatakiwa kumtia moyo mke wako kama vile unavyomtendea.
Watoto wako pia wanafanya kazi yao. Wao pia wanamngojea baba yao wajifurahishe. Wafundishe mambo yaliyo sahihi na uwape hamasa wajifunze zaidi. Je, ni haki kwamba unakutana na familia yako ukiwa na uso wa kikatili na chuki?
Wanakutarajia wewe kuwatimizia matakwa ambayo ni haki yao. Wanatazamia wema kutoka kwako na wanataka uzungumze nao kwa upole na uoneshe furaha.
Watakuchukia sana kama ukidharau hisia zao na kama utaigeuza nyumba kuwa mahali pa giza ambamo hakuna furaha hata kidogo.
Unajua watateseka kiasi gani kutokana na tabia yako isiyopendeza na ya kikatili? Hata kama hutaichukulia familia yako kwa uzito uanostahili angalau ujihurumie wewe mwenyewe. Uwe na uhakika kwamba unaweza kuharibu afya yako kwa kuendeleza ukali.
Unawezaje kuendelea kufanya kazi na unawezaje kufuzu kupata mafanikio? Kwa nini uigeuze nyumba yako iwe jahannamu? Hivi si vizuri zaidi kwamba wewe uwe na furaha kila mara na uyakubali matatizo yako kwa busara na si hasira?
Hungetaka kuamini kwamba hasira haiwezekani kutatua matatizo yako, isipokuwa hasa zaidi matatizo yataongezeka? Hungekubali kwamba unapokuwa nyumbani unatakiwa kupumzika na kurudisha nguvu zako ili uweze kupata ufumbuzi unaofaa kwa matatizo yako akili yako ikiwa imetulia? Kutana na familia yako ukiwa na uso wenye tabasamu; taniana na watu wa familia yako kwa namna nzuri na jaribu kutengeneza mazingira ya furaha nyumbani kwako. Ule na kunywa pamoja nao na upumzike.
Kwa njia hii wewe na familia yako mtafurahia maisha na mtashinda matatizo yenu kwa urahisi. Ndio sababu dini tukufu ya Uislamu inaona tabia njema kuwa sehemu ya dini na ishara ya kiwango cha juu sana cha imani.
Mtume (s.a.w) alisema: “Mtu mwenye tabia njema amekamilika zaidi katika imani yake. Mtu mwema zaidi miongoni mwenu ni yule anayeitendea mema familia yake.”
Mtume (s.a.w) pia alisema: “Hakuna tendo jema zaidi kuliko tabia njema.”
Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Kuwatendea wema watu na kuwa na tabia inayostahili unapokuwa nao kufanya miji huwa na watu wengi zaidi na umri wa raia huongezeka.”
Imamu Sadiq (a.s) pia alisema: “mtu muovu hubakia kwenye mateso na uchungu.”
Luqman mwenye hekima alisema: “Mtu mwenye busara lazima afanye mambo kama mtoto mdogo wakati anapokuwa na familia yake, na kuendelea na tabia ya kiwanamume anapokuwa nje ya nyumba yake.”
Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: “Hakuna furaha iliyo nzuri zaidi kuliko tabia njema.”
Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Tabia njema ni nusu ya dini ya Uislamu.”
Imesimuliwa kwamba alipokufa Sad bin Maadh mmojawapo wa sahaba mashuhuri wa Mtukufu Mtume (s.a.w), Mtume (s.a.w) alishiriki kwenye maziko yake bila kuvaa viatu, kama vile alipoteza mmojawapo wa watu wa familia yake.
Mtume (s.a.w) aliweka maiti ya sahaba huyo karibuni kwa mikono yake iliyotakasika halafu akaufunika. Mama yake Sad ambaye alikuwa anaangalia heshima ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwa mwanae alimwambia Sad: “Ewe Sad! furahia Pepo” Mtume (s.a.w.w) alimwambia:
“Ewe mama wa Sad, usiseme hivyo, kwa sababu Sad sasa hivi amepata mateso kwa njia ya kugandamizwa kaburini na kadhalika. Baadaye, Mtume (s.a.w.w) alipoulizwa kuhusu sababu ya mateso ya Sad, Mtume (s.a.w.w) alijibu; “Ilikuwa kwa sababu alikuwa anaitendea mabaya familia yake.”

Comments
Post a Comment