Mji Uliokuwa Na Amani SOMA KISA HIKI
Maana
Wafasiri wametofautiana kuhusu mji uliotajwa kuwa, je, ni mji hasa au ni kiasi cha kukadiria tu kwa ajili ya kupigia mfano? Razi amenukuu kutoka kwa wafasiri wengi kuwa makusidio ya mji huo ni Makka.
Vyovyote iwavyo, sifa hizi zinafanana na Makka na watu wake. Kwa sababu watu walikuwa na amani ya nafsi na mali zao; hawakuwa na hofu ya vita wala ujambazi; kama ilivyokuwa kwa miji mingine ya waarabu.
Pia wakazi wa hapo hawakuwa na haja ya kuhemea chakula, kwa sababu riziki ilkuwa ikiwajia kutoka kila mahali, kutokana na kuitikiwa dua ya Ibrahim (a.s.):
رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُمْ مِنَ الثَّمَرَاتِ {37}
“Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda.” Juz. 13: (14:37).
Lakini watu wa Makka walizikufuru neema za Mwenyezi Mungu kwa kumkadhibisha Muhammad (s.a.w.) na wakaazimia kumuua mpaka akalazimika kuuhama mji wake.
Watu wa Makka walipatwa na njaa kwa dua ya Mtume (s.a.w.), pale aliposema: “Ewe Mola wangu! Wadhikishe kwa madhara na uajaalie miaka (ya shida) kama miaka ya Yusuf.” Basi Mwenyezi Mungu akaitikia maombi yake. Wakapatwa na shida mpaka wakawa wanakula mizoga, majibwa, mifupa iliyochomwa, manyani na ngozi iliyochanganywa na damu.
Mtu alikuwa akiangalia mbinguni na kuona moshi kutokana na njaa. Ama hofu iliyowapata ni pale nchi ilipowatingisha wakaanguka ni mateka wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.).
فَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاشْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ {114}
Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu.
إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنْزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّهِ بِهِ ۖ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {115}
Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwengi maghufira, Mwenye kurehemu.
وَلَا تَقُولُوا لِمَا تَصِفُ أَلْسِنَتُكُمُ الْكَذِبَ هَٰذَا حَلَالٌ وَهَٰذَا حَرَامٌ لِتَفْتَرُوا عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُونَ {116}
Wala msiseme uwongo kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali na hiki ni haramu, mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu.
مَتَاعٌ قَلِيلٌ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {117}
Ni starehe ndogo nao watapata adhabu chungu.
وَعَلَى الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا مَا قَصَصْنَا عَلَيْكَ مِنْ قَبْلُ ۖ وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَٰكِنْ كَانُوا أَنْفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ {118}
Na wale waliokuwa mayahudi tuliwaharamishia tuliyokusimulia kabla. Na hatukuwadhulumu, laikini walijidhulumu wenyewe.
ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ عَمِلُوا السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابُوا مِنْ بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا إِنَّ رَبَّكَ مِنْ بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَحِيمٌ {119}
Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga kisha wakatubu baada ya hayo na wakatengenea, hakika Mola wako ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Comments
Post a Comment