Kuweza Kuishi Na Ndugu Wa Mumeo
Kuweza Kuishi Na Ndugu Wa Mumeo
Mojawapo ya matatizo ya kifamilia husababishwa na ndugu wa mume na mke wake.
Baadhi ya wanawake hawana uhusiano mzuri na mama wa mumewe, dada au kaka zake mumewe.
Kwa upande moja mke anaweza kujaribu kumtawala mume wake ili asiweze kumsikiliza hata mama yake au ndugu yake yeyote na anaweza kujaribu kuwafitinisha ili wasielewane wao kwa wao. Kwa upande mwingine, mama wa mume anajiona kuwa yeye ni mmiliki wa mwanae na mke wa mwanae.
Mama hujaribu sana kuwa karibu sana na mwanae na kutahadhari kwamba mke wa mwanae asiweze kummiliki mumewe kwa ukamilifu. Anaweza kusingizia uwongo kuhusu mke wa mwanae au kumuona anayo makosa.
Msimamo wa aina hii unaweza kufuatwa na mabishano mengi na hata chuki ya mara kwa mara. Hali inakuwa mbaya zaidi endapo watu hawa huishi kwenye nyumba moja. Hata kama ugomvi unaweza kutokea baina ya wanawake wawili, uchungu wa kiakili na dhiki hasa zaidi humpata mume aliyoko kati yao.
Mume ananaswa katikati ya mabishano ambapo hawezi kuegemea upande wowote. Kwa upande moja yupo mke wake ambaye angependa kuendesha maisha ya kujitegemea bila kuingiliwa na mtu yeyote. Kwa kawaida mume huhisi lazima amsaidie mke wake na amfurahishe. Lakini kwa upande mwingine, anafikiria wazazi wake ambao wamemsaidia kuingia katika maisha, wamemsomesha na wametumia muda mwingi wa maisha yao kumlea.
Anahisi kwamba wazazi wake wanatarajia awasaidie wakati wanahitaji msaada na kwamba haitakuwa busara kuwasahau. Zaidi ya hayo, kama yeye mwenyewe anayo haja ya kupata kitu fulani, hatakwenda kwingineko isipokuwa kwa wazazi wake, ambao watamsaidia yeye na familia yake. Matokeo yake ni kwamba anatambua kwamba marafiki zake wakuaminika ni wazazi wake na ndugu zake. Kwa hiyo, mtanziko kwa mtu mwenye busara ni ama kuwa upande wa mke na kuwaacha wazazi au kinyume chake, lakini hapana lolote kati ya haya mambo mawili yanawezekana.
Matokeo yake, atalazimika kwenda na pande zote mbili na kuziweza pande hizi katika hali ya kuridhika ambayo ni kazi ngumu. Njia moja tu inayoweza kurahisisha hali ni kwamba mwanamke lazima awe mwaminifu na mwenye hekima. Katika hali kama hii, mume anatarajia mkewe amsaidie katika kutatua tatizo.
Kama mke anamheshimu mama mkwe wake, humtaka ampe ushauri wake, na anakuwa mtiifu na kufanya urafiki naye basi, mama mkwe wake atakuwa msaidizi wake mkubwa sana.
Je, si jambo la kusikitisha kuona mtu ambaye anaweza kuwavutia watu wengi kwa sababu ya wema wake na tabia zake, halafu awafukuze kwa ajili ya ukaidi na ubinafsi wake? Hutambui kwamba katika mazuri na mabaya ya maisha, mtu anaweza akahitaji msada wa wengine, na hususan ule wa ndugu ambao wanaweza kukusaidia ambapo kila mtu akiwa amekukimbia? Je, si ni jambo zuri zaidi kufurahia uhusiano mzuri na ndugu wa mtu kwa kutumia busara na tabia njema? Je, hivi kweli ni busara na haki kufanya urafiki na watu wengine ambapo unavunja uhusiano na ndugu zako?
Uzoefu unaonesha kwamba mtu anapotaka msaada kutoka kwa wengine, marafiki humkimbia lakini ndugu aliwo watupa huja kumsaidia. Hii ni kwa sababu mshikamano wa kifamilia unao asili na hauwezi kuvunjika kwa urahisi. Kuna methali isemayo: “Hata kama nyama ya mtu ingeliwa na ndugu zake, wasingeitupa mifupa yake”
Imam Ali (a.s) alisema: “Mtu hawezi kamwe kuishi bila kuwa na ndugu zake, hata kama ni tayari na anao watoto.”
Mtu atataka heshima na wema wa ndugu zake. Ni wao ndio watakao msaidia kimwili na kiakili. Ni ndugu ndio wanasaidia mara nyingi. Wakati wa shida ndugu huweza kusaidia haraka zaidi kuliko wengine. Yeyote anaye watupa ndugu zake hupoteza mikono mingi, ya kumsaidia.
Mpendwa Bibi! Kwa ajili ya mume wako na faraja yako mwenyewe na pia kutafuta marafiki wengi na wanao kuunga mkono, vumilia kuwa nao ndugu wa mumeo. Usiwe mbinafsi na mjinga; uwe na busara na usisababishe usumbufu wowote kwa mumeo. Uwe mke mzuri na mwenye kujitolea ili uweze kukubalika kwa Mwenyezi Mungu na watu.
Kuvumilia Kazi Ya Mume Wako
Kila mtu anayo kazi na kazi hutofautiana; mathalan, dereva ambaye muda mwingi zaidi yupo barabarani na anashindwa kurudi nyumbani kila siku usiku; polisi ambaye anatakiwa kuwa kwenye zamu baadhi ya muda wa usiku; daktari wa tiba ambaye ana muda mfupi wa kuwa na familia yake, mkufunzi au mwanasayansi ambaye husoma sana muda wa usiku; makanika ambaye nguo zake ni chafu na hunuka mafuta, mfanyakazi kiwandani ambaye hufanya kazi usiku. Kwa hiyo ni mara chache sana mtu kuwa na kazi ambazo hazisumbui kwa namna moja au nyingine na kusababisha kero kwa familia.
Hakuna njia nyingine yeyote ya kupata riziki kihalali isipokuwa kufanya kazi. Ni muhimu kwa wanaume kuvumulia matatizo ya kazi zao. Hata hivyo, kuna tatizo lingine ambalo ni malalamiko ya familia.
Kwa kawaida wanawake hupenda waume zao kuwa karibu nao na hupendelea wawepo nyumbani giza liingiapo. Wanawake hutaka waume zao kuwa na kazi nzuri yenye mshahara mnono. Wanapenda kuwa na muda wa kutosha wa kwenda matembezi ya jioni. Lakini bahati mbaya kazi za waume walio wengi, hazikidhi matamanio ya wake zao, na hii kwa baadhi ya familia ni chanzo cha ugomvi na mabishano.
Dereva ambaye amekuwa kazini kwa mausiku kadhaa, ambaye hajalala usingizi wa kutosha na amekuwa hapati chakula kwa wakati unaostahili, anaingia nyumbani kwake apumzike na apate amani na faraja akiwa na familia yake. Halafu mke wake, bila kumpa nafasi ya kupumzika hata kidogo, anaanza kupiga kite na kugumia: “maisha gani haya? Kwa nini unaniacha mimi na watoto hawa na ulikuwa wapi? Ninafanya kazi zote kwa sababu wewe haupo ambapo ungenisaidia. Nimechoshwa na hawa watoto watundu! Na kwa kweli udereva si kazi nzuri. Ama lazima ubadili kazi au tulizana na mimi hapa nyumbani. Siwezi kuishi namna hii zaidi ya hapa!”
Masikini dereva huyu ambaye anaye mke wa aina hii hawezi kutegemewa kufanya vizuri kazi yake na anaweza kuhatarisha maisha yake; na maisha ya hao anao wasafirisha.
Daktari ambaye tangu asubuhi hadi usiku, huwatembelea wagonjwa makumi kadhaa hawezi kuvumilia malalamiko ya mke wake. Daktari huyu ataweza kuendelea na kazi yake? Mfanya kazi ambaye hufanya kazi ya zamu ya usiku hawezi kufuatilia kazi yake kwa hamasa endapo mke wake ni mwanamke mjanja.
Mwanasayansi ataweza kufuzu katika eneo la taaluma yake ya utafiti endapo mke wake anamsumbua kila wakati?
Hii ni mitihani inayo wabainisha wanawake wenye busara na wale walio wajinga.
Mpendwa Bibi! Hatuwezi kuitengeneza dunia iwe vile tunavyotaka sisi, na mazingira yaliyopo. Mume wako anahitaji kazi ili aweze kupata riziki halali kwa ajili ya familia yake. Kazi yake inayo masharti ambayo yatakufanya ubadilike ili uendane nayo. Lazima upange utaratibu wa maisha ya familia yako kufuatana na kazi yake. Kwa nini ulalamike na umuone anayo makosa kwa sababu ya kazi yake? Mkaribishe nyumbani kwa uso wenye furaha na uwe mwema kwake. Uwe na hekima na uivumilie kazi yake.
Kama mume wako ni dereva ambaye muda mwingi yupo barabarani, basi, tambua kwamba anajaribu kuleta fedha nyumbani kwa ajili yako na watoto. Kazi yake si tatizo. Yeye ni sehemu ya jamii na anaihudumia kwa namna nzuri kadiri awezavyo. Ingekuwa bora kama angekuwa mvivu au kama angekuwa anafanya kazi isiyoendana na masharti ya dini? Kwa hiyo, yeye hana ubaya wowote. Kasoro ipo kwako, unatarajia awepo nyumbani kila siku usiku na wewe unashindwa au hutaki kubadilika kufuatana na hali iliyipo sasa.
Hivi si busara kuzoea hali ya wakati uliopo na kuishi kwa raha zaidi? Si ingekuwa bora zaidi kumkaribisha mumeo kwa uso wenye tabasamu na kumshawishi aendelee na kazi yake kwa kumpa ‘kwa heri’ ya kuchangamsha anapoondoka nyumbani kwenda kwenye kazi yake? Kama ukimfanyia wema, atazidi kuvutiwa na familia yake na anaweza kuzidisha bidii kwenye kazi yake.
Hata farakana na wewe; atarudi nyumbani mapema kadiri iwezekanavyo; atajitahidi asifanye ajali na atakuwa imara kushikilia maadili mema.
Kama mume wako anafanya kazi ya zamu ya usiku, anakosa usingizi mzuri wa usiku ili aweze kumudu matumizi ya familia yake. Jaribu kuzoea hali hii na usioneshe kutokuridhika kwako. Kama unachoshwa na upweke, unaweza kufanya baadhi ya kazi za nyumbani, kushona na kusoma wakati wa usiku. Asubuhi tayarisha kifungua kinywa, mume wako anaporudi kutoka kwenye kazi, halafu tandika kitanda mahali penye kimya. Wanyamazishe watoto wawe kimya na uwafundishe wasimsumbue baba yao wakati anapumzika. Unaweza hata kulala nusu usingizi ili uweze kupumzika na mume wako wakati wa mchana. Lakini usisahau kwamba amekuwa macho usiku kucha na usingizi wake wa mchana ni sawa na usingizi wako wa usiku. Wanawake waliopo kwenye hali kama hii wanatakiwa kuwa na mipango ya aina mbili, moja wa kwao na mwingine wa waume zao.
Kama mume wako ni dereva, dakitari, mfanya kazi au bingwa wa sayansi na kadhalika, basi lazima ujivune na sababu ya kuwa naye. Mume wako si mvivu, mzururaji au hafanyi kazi isiyo afikiana na mafundisho ya dini. Kwa hiyo, umthamini na kumshukuru.
Usimtarajie yeye au kumuambia aache kazi yake, lakini jaribu kuafikiana na kazi aliyonayo. Kama anasoma au anatafiti katika eneo fulani, basi usimsumbue. Wewe unaweza kufanya kazi ya nyumbani soma kitabu au kwa ruhusa yake, nenda uwatembelee marafiki au ndugu.
Lakini, wakati anapumzika, jaribu kuwepo nyumbani. Tayarisha chakula chake na mahitaji mengine. Mpokee mume wako kwa tabasamu na tabia njema. Kwa kuonesha wema wako na kwa kumfurahisha, unaweza kumfanya asahau uchovu wake. Kama wewe ni mke mzuri, basi si tu kwamba utaharakisha kupandishwa kwake cheo, lakini unatoa mchango kwa huduma zake kwa jamii.
Si wanawake wote wanastahiki wanamume wenye bidii kama hao. Kwa hiyo, kwa kuwa na tabia njema na mwenye kujitolea, thibitisha kwamba na wewe unastahiki kuwa naye.
Kama kazi ya mume wako inamtaka avae nguo rasmi ambazo huchafuka, basi zifue nguo hizo mara kwa mara.
Usilalamike na usimwambie mambo yasiyofaa kwa sababu ya kazi yake. Usimwambie abadili kazi. Kuna ubaya gani kuwa makenika? Kwa vyovyote vile, hili si jambo la umuhimu na familia zisivunjike kwa sababu hii.
“Mwanamke alimwambia jaji mahakamani kwamba kazi ya mume wake, ilikuwa kuuza mafuta ya taa na kwa hiyo kila mara alikuwa ananuka vibaya na kwa hiyo alichoshwa na hali hiyo.”

Comments
Post a Comment