Kikwazo Kikubwa Katika Kusuluhisha Tofauti
Kikwazo kikubwa sana katika kusuluhisha ugomvi wa kifamilia ni ubinafsi na kiburi. Kwa bahati mbaya, watu wengi huathiriwa na tabia hizi. Watu kama hawa hupungukiwa na sehemu fulani ya akili ambapo hukubali tabia zao tu na kukataa za wengine na hawataki kukubali makosa yao. Hususan ni hatari sana ambapo ghasia ya tabia inafanikishwa na mtu mwingine yaani, kuwakosoa wengine kwa makosa yao. Wakati mwingine mume na mke wote husumbuliwa na tatizo hili kwa maana hiyo, watagombana kila siku. Kila mmoja atamlaumu mwenzake na wakati huo huo kila mmoja wao atakataa kuhusika kabisa na makosa yote.
Wakati mwingine kama upande moja tu utaumia kutokana na dosari hii ya kukoseana, kila mmoja atamwona mwenzake analo kosa na kwa kufanya hivyo watakuwa wanajikomboa kabisa kutokana na kulaumiana.
Pale ambapo mume na mke wote wanakumbwa na usumbufu wa vurugu hii, ni vigumu sana kuwasuluhisha, kwa sababu hawatakuwa tayari kuzingatia ushauri wa mtu yeyote. Wakati ambapo kila mmojawao anasikiliza redio au anaangalia vipindi vya runinga vinavyohusu mambo ya familia, wataona dosari fulani ya tabia ambayo inaendekezwa na mwenza wake na kwa hiyo ataanzisha lawama zake hapo hapo. Lakini dosari yoyote ikizungumziwa inayogusa udhaifu wao watajifanya hawasikii na wataelekeza fikira zao kwenye mambo mengine. Wanaweza kununua kitabu kinachohusu maadili ya familia na kumpa mwenza wake, bila wao kuwa na hisia zozote za kuwa na hamu ya kusoma yaliyomo humo.
Ubinafsi unaweza kuwa mkali sana hivyo kwamba muathirika hataweza hata kutambua tatizo hilo. Katika hali kama hiyo, uhusiano baina ya wanandoa unaharibika na hata usiwezekane kuendelea. Matokeo yake ni, ama maisha yataendelea katika hali ya ugomvi, huzuni, kutokuwa na furaha au hata kutalikiana.
Kwa hiyo, inashauriwa kwamba wanandoa wote waache tabia ya ubinafsi na kiburi. Wanandoa ambao wanatatizwa na hali hii, wanatakiwa wapate muda wakae pamoja, na wawe kama majaji wawili waaminifu wazungumzie matatizo yao. Kila mmoja amsikilize mwenzake kwa umakini na bila upendeleo wowote. Kila mmoja wao anatakiwa kufahamu dosari zake bila kusahau hata iliyo ndogo sana pamoja na nia ya kuzirekebisha. Halafu wote wawili wanatakiwa waamue kujisahihisha wao wenyewe; lakini ni hapo tu ambapo wanahisi umuhimu wa uelewano wa kina na ambapo wote wanatamaani kufufua mapenzi yao na utulivu ambao ulikuwapo baina yao.
Hata hivyo, inapokuwa hakuna uwezekano wa kupatikana suluhu, wanandoa wanatakiwa kuwasilisha matatizo yao kwa mtu mwenye uzoefu, mwaminifu, mtambuzi wa kutegemewa na mwema. Kama mtu kama huyo ni rafiki au ndugu, hiyo itakuwa nafuu yao kwa sababu wanaweza kumwambia kila kitu na kungoja hukumu yao. Lazima wamsikilize na kuupokea ushauri wake na kutia nia ya kuutekeleza kwa vitendo.
Kama ilivyo, kuamini ushauri wa jaji si rahisi, lakini mtu ambaye anajali familia yake na uimara wake, amani kudumu kwake anatakiwa kuvumilia na baadaye afurahie matokeo yake yenye manufaa.
Wazazi wa wanandoa wa aina hiyo, kama wanatambua matatizo ya kifamilia ya watoto wao, wanatakiwa kuwashauri wamuone Kadhi mwenye uzoefu, mwaminifu na nia njema. Wazazi hawatakiwi kuonesha upendeleo kwa mume au mke., Kwa njia hii, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, matatizo yao yanaweza kutatuliwa.
Mwenyezi Mungu anasema kwenye Qurani Tukufu:
وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِنْ أَهْلِهَا إِنْ يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّهَ كَانَ
عَلِيمًا خَبِيرًا
{35}
“Na mkichelea kutakuwepo mfarakano baina ya mume na mke basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke, wakitaka mapatano mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye Khabari.”(Quran 4:35)

Comments
Post a Comment