Hifadhi Siri Za Familia

Wanawake mara nyingi kupenda kujua siri za waume zao, kipato chao, maamuzi yao kuhusu maisha ya siku zijazo, na kazi zao. Wanatarajia wanamume hawataficha chochote kutoka kwao.
Kinyume chake, wanaume hawapo tayari kuwaambia wake zao kila kitu. Matokeo yake ni kwamba waume wengine na wake wengine wakati wote huwa wanabishana kuhusu suala hili.
Baadhi ya wanawake wanasema kwamba waume zao hawana imani nao, hawataki wasome barua zao; hawataki wajue idadi ya kipato chao; wanaficha mambo mengi, hawajibu maswali yao inavyo stahili; na mara nyingine husema uwongo.
Katika hali ya kawaida, wanaume wanaweza kuwaambia wake zao siri zao.
Lakini wanaume wanamini kwamba wake zao hawafichi siri; kwamba huwaambia watu kila kitu wanacho jua na wanaweza hata kusababisha matatizo kwa waume zao.
Kama mtu anataka kujua siri za watu wengine inatosha kwenda kwa wake zao. Baadhi ya wake za watu, baada ya kujua siri za waume zao, huwasaliti na kwa hiyo hutumia vibaya imani ya waume zao kwao.
Ni dhahiri kwamba wanaume kwa kiasi fulani wanayo hoja. Wanawake, wakilinganishwa na wanaume, wanazidiwa zaidi na nguvu za mvuto wa hisia. Wanawake wanapo kasirika, hushindwa kujidhibiti, na kwa kuwa wanajua siri za waume zao, huwaingiza kwenye matatizo kwa kutoa siri zao.
Kwa hiyo, kama mwanamke anataka kujua siri za mume wake, lazima awe mwangalifu sana kwamba asiwaambie watu isipokuwa kwa idhini yake. Hatakiwi kuwaambia hata marafiki zake wa karibu sana au ndugu zake. Huko si kuweka siri kama ukimwambia mtu kuhusu siri hiyo, na kumwambia asiseme kwa mtu yeyote, vinginevyo kila mtu atajua siri hiyo.
Kwa hiyo mtu mwenye busara ni yule ambaye hasemi siri yake kwa mtu yeyote.
Imamu Ali (a.s) pia alisema: “Kifua cha mtu mwenye hekima ni kasiki ya siri zake.”
Imamu Ali (a.s) pia alisema: “Wema wa ulimwengu huu na ule ujayo umo katika mambo mawili; Kuwa msiri, na kufanya urafiki na watu wazuri; na maovu yote yamo kwenye mambo mawili kushindwa kuwa msiri na kufanya urafiki na watu wabaya.”

Kubali Uongozi Wake

Kila taasisi, kiwanda na shirika huhitaji meneja muajibikaji. Kwenye kila kitengo cha jamii na shirika, ushirikiano baina ya wafanyakazi ni muhimu. Hata hivyo, kuendesha mambo ya kitengo cha aina hiyo huhitaji meneja ambaye anaweza kuratibu kazi.
Mojawapo ya kitengo muhimu sana cha jamii ni familia; Kuendesha mambo ya kitengo hiki ni jambo la lazima na gumu.
Bila shaka, lazima pawepo na uelewano wa kina sana, na ushirikiano baina ya watu wa familia, lakini pia lazima pawepo kiongozi ambaye anaweza kuwajibika kwa ukamilifu kuhusu mambo ya familia. Ni wazi kwamba, kama familia haimfurahikii mtu anayeweza kuwapanga wengine, itapata usumbufu wa vurugu na ghasia.
Hivyo ama mume lazima awe kama mkurugenzi na mke awe chini yake au kinyume chake.
Hata hivyo, kwa kuwa kipengele cha mantiki ya wanaume kinatawala kipengele cha hisia za wanawake, wanaume wanaweza kuwa viongozi bora zaidi.
Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anasema kwenye Qurani Tukufu:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّهُ

ۚ

{34

}
“Wanamume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayotoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii ….” (Quran 4:34).
Hivyo, ni kwa manufaa ya jamaa wa familia kumheshimu mwanaume kama mlinzi wao na mkuu wao, na kutaka usimamizi wao katika matendo yao.
Hata hivyo, mtu asihitimishe kwamba hadhi ya mwanamke ndani ya nyumba inadunishwa, lakini ni kweli kwamba kudumisha utaratibu na nidhamu ndani ya nyumba ni majukumu yanayohitaji utendaji wa mume. Wanawake wanaoweza kufikiri bila upendeleo, wanaweza kuthibitisha tendo hili.
Mwanamke alisema: “Tulikuwa na desturi nzuri Iran ambayo kwa bahati mbaya imefifia pole pole. Kwenye mila hii mwanaume alikuwa ndiye mkuu wa mambo ya familia. Alikuwa ndiye msimamizi. Siku hizi hata hivyo hali imebadilika na familia haziwezi kufanya uamuzi kuhusu nani awe mkuu.
Ninaamini kwamba mwanamke wa leo, ambaye kwa namna moja au nyingine anayo hadhi sawa na ya mwanaume katika jamii, anaweza kukubali mume wake kama mkuu wa kaya…Desturi hii ya zamani inatakiwa ipendekezwe kwa mwanamke kijana wa leo, ambaye anayo nia ya kuolewa.
Anatakiwa kuingia nyumbani kwa mumewe akiwa amevaa vazi la harusi na kutoka ndani ya nyumba hiyo akiwa amevaa sanda.”
Ni kweli kwamba shughuli za maisha ya kila siku hazimruhusu mwanaume kushiriki katika mambo yote ya familia na kwamba kwa kawaida mke ndiye anaye endesha familia kufuatana na atakavyo, lakini hata hivyo haki ya kuamuru hubaki kwa mwanaume, na kwa hali hiyo lazima ahishimiwe.
Kwa hiyo, inapotokea mwanaume kutoa maoni yake kuhusu jambo lolote la familia au anashauri kitu chochote, mke hatakiwi kumpinga au kumnyima mume wake haki yake kuamuru kwa namna yoyote ile. Vinginevyo, mwanaume atajifikiria yeye hana mamlaka na kumuona mke wake kama mwanamke asiye na adabu na shukrani. Mwanaume anaweza kujenga kinyongo dhidi yake na katika hatua ya baadaye, anaweza hata kukataa matakwa ya halali ya mkewe.
Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu alisema: “Mwanamke mzuri atajali matakwa ya mumewe, na atafanya kwa mujibu wa apendavyo mumewe.”
Mwanamke alimuuliza Mtume (s.a.w): “Mwanamke anawajibu gani kwa mume wake?” Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke lazima amtii mume wake na asikiuke amri zake.”
Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Mwanamke mbaya sana miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mkaidi na sugu.”
Mtume (s.a.w.w) pia alismema: “Mwanamke mbaya zaidi miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mgumba, mchafu, sugu na asiye mtiifu.”
Bibi mpendwa! Kubali mamlaka ya mume wako. Taka usimamizi wake kuhusu mambo yenu ya familia. Usikiuke amri zake. Usikatae au kuweka pingamizi, yeye hushiriki katika mambo ya nyumbani na familia. Usikatae kushiriki kwake hata kwenye yale mambo ambayo wewe una utaalamu nayo. Usifanye vitendo vya kuonesha kwamba yeye hana mamlaka.
Mruhusu ashiriki katika kazi zako mara chache. Wafundishe watoto wenu kuhishimu mamlaka yake na waambie lazima waombe ruhusa kutoka kwa baba yao kuhusu mambo yao. Watoto wenu lazima watambue kwamba hawatakiwi kukiuka amri zake tangu utoto wao.
Kwa njia hii watoto wenu watakuwa na malezi ya kuwatii wazazi wao.

Uwe Muelekevu Wakati Wa Hali Ngumu

Maisha yamejaa hali ya kupanda na kushuka kuhusu kipato. Magurudumu ya bahati njema hayazunguki mara zote kufuatana na vile tunavyotaka. Mtu kupita kwenye hali ngumu mara nyingi. Kila mtu huugua maradhi. Hupoteza kazi zao na wengine wanaweza kupoteza utajiri wao wote. Mambo mengi yasiyo furahisha hutokea katika maisha ya kila mtu.
Mwanaume na mwanamke ambao wametoa kiapo cha kuaminiana wao wawili na kusaini makubaliano ya ndoa, wanatakiwa kupita kwenye njia ya maisha kwa kuelewana. Makubaliano yanatakiwa kuwa imara sana hivyo kwamba yanaweza kuwawoka pamoja katika hali ya maradhi na afya njema, katika hali ya neema na shida ya kipato na wakati wa raha na shida.
Bibi mpendwa! Kama mume wako anafilisikia na kuwa fukara, hivi ni lazima uongeze kwenye matatizo yake kwa kuwa na tabia isiyo kubalika.
Kama anaugua, na kulala kitandani, ama nyumbani au hospitalini, ni hatua ya kupendeza wewe ukizidisha wema kwake. Lazima umuuguze, shughulikia mahitaji yake, na tumia fedha kwa ajili yake. Kama unazo fedha za kwako mwenyewe, lazima ulipie matibabu yake. Kumbuka kama wewe ungekuwa mgonjwa, angelipa fedha yake kwa ajili ya afya yako. Je, ni haki wewe uzuiye mali yako kwa kuipendelea zaidi kuliko afya njema ya mume wako? Kama ukishindwa kumridhisha katika wakati mgumu kama huu, basi utamkasirisha, na anaweza hata kupendelea kukutaliki.
Hapa kuna kesi ifaayo kusoma: “Mtu alikuja mahakamani kumwacha mke wake. Alisema: ‘Siku chache zilizopita niliugua na daktari wangu aliniambia kwamba nilitakiwa kufanyiwa upasuaji. Nilimwomba mke wangu anikopeshe fedha alizokuwa nazo kwenye akiba yake. Alikataa na aliondoka nyumbani kwangu. Matokeo yake nilifanyiwa upasuaji kwenye Hospitali ya taifa. Sasa nimepona na afya yangu ni njema sitaki kuishi na mwanamke ambaye anapenda zaidi fedha yake kuliko mume wake. Mtu atamwitaje mwanamke huyu, mke?”
Kila mtu aliye makini katika mambo yake atakubali kwamba kwenye mfano uliotajwa hapo juu, mwanaume ndiye aliyekuwa na haki. Mwanamke kama huyo ambaye hataki kutumia fedha yake kwa ajili ya tiba ya mume wake, hastahili kuwa kwenye nafasi inayo heshimiwa ya ‘mke wa mtu.’
Bibi mpendwa! Uwe mwangalifu, usiwe katili wakati mume wako akiumwa maradhi ya kudumu; hivi ni lazima umwache yeye na watoto wenu kwa sababu hii? Unawezaje kumkimbia mwanamume ambaye umekuwa naye mchana na usiku wa starehe ya siku nyingi? Unajuaje kwamba labda hatima ya aina hii inakungojea wewe? Unawezaje kuwa na uhakika kwamba mwanamume mwingine atakuwa bora zaidi kuliko huyu? Usiwe sugu na mbinafsi. Ujitolee mhanga na uwe na moyo wa kumuabudu Mwenyezi Mungu, uilinde heshima yako na watoto wako.
Uwe mvumilivu na uwafundishe watoto wako somo la moyo wa upendo, mapenzi na ustahamilivu.
Unaweza kuwa na uhakika kwamba, katika dunia hii na ile ijayo, utapata thawabu nyingi sana. Moyo wako wa kujitolea ni njia bora sana ya kuonesha unamjali mume wako tabia ambayo inawekwa kwenye kiwango sawa na Jihadi.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Jihadi ya mwanamke ipo katika kumtunza mume wake.”

Usikatae Kusema Na Usinune

Ni kawaida ya wanawake wengine kwamba, wanapo tibuliwa na waume zao, hununa, hukataa kusema, hukataa kushughulikia kazi za nyumbani, hawataki kula, huwapiga watoto, au hulalamika. Wanaamini kwamba kuacha kusema au kuanzisha ugomvi ndizo njia nzuri sana kulipiza kisasi kwa waume zao. Msimamo huu si tu unashindwa kumwadhibu mwanaume, lakini unaweza kusababisha naye kulipiza kisasi. Maisha huanza kuwa magumu kwani hugeuka kuwa na mfululizo wa ugomvi. Mwanamke hupiga kite, halafu mwanamume naye hufanya hivyo. Mwanamke hukataa kusema na mwanamume hulipa kisasi. Mwanamke hufanya kitu kingine, na mwanamume hufanya hivyo hivyo hadi wanachoka na kupitia upatanishi wa ndugu au marafiki, huelewana. Lakini hii si mara ya kwanza wao kugombana. Watagombana tena na tena na patakuwepo na siku chache za machungu.
Kwa hiyo, kuishi maisha yenye ugomvi wa familia litakuwa si jambo la kufurahisha kwa ama wazazi au watoto. Vijana wengi waliozikimbia familia zao wanatoka kwenye familia za aina hii ambao baadaye huingia kwenye uhalifu na uovu.
Kijana ambaye alikamatwa kwa tuhuma ya wizi, aliwalaumu wazazi wake kwa uhalifu wake na alisema: “Wazazi wangu walikuwa wakibishana kila siku na baadaye kwenda kwa ndugu zao na mimi nilikwenda kuzurura mitaani. Halafu nikadanganywa na vijana wengine na hatimaye nikafanya uhalifu wa wizi.”
Msichana mwenye umri wa miaka kumi aliwaambia wafanya kazi wa usitawi wa jamii: “Sina uhakika lakini nakumbuka kwamba siku moja wakati wa usiku wazazi wangu walibishana kuhusu kitu fulani. Kesho yake, mama yangu aliondoka na baada ya siku chache, baba alinipeleka kwa shangazi yangu. Baada ya kipindi fulani mwanamke mkongwe alinichukua kutoka kwa shangazi na akanileta Tehran. Ni miaka michache iliyopita hadi sasa, ambapo nimekuwa ninaishi naye na niliteseka sana hivyo kwamba sitaki kurudi kwake.”
Mwalimu wa msichana huyo alisema; Huyu msichana ni mmojawapo wa wanafunzi wangu. Hana maendeleo mazuri katika masomo yake na inaonesha kama vile anaumizwa na jambo fulani. Wakati wote anafikiri. Amekuwa hata anakaa kwenye ua wa shule na kuonekana hayuko tayari kurudi nyumbani. Siku mbili zilizopita nilimuuliza kwa nini hataki kwenda nyumbani? Akajibu kwamba alikuwa anaishi na mwanamke mzee ambaye alikuwa mbaya sana kwake na kwamba hakutaka kurudi nyumbani kwa bi kizee huyo. Nilimuliza kuhusu wazazi wake na akasema walitengana.”
Bibi mpendwa! Lazima ukumbuke kwamba kama mume wako anakuwa mkali sana kwako na hataki kusema na wewe, halafu anaweza hata kuchukua hatua kali zaidi kama vile kukupiga.
Inawezekana labda utaondoka kwenda kwa wazazi wako kwa sababu ya ukali wake. Kitakachofuatia ni kwamba wazazi wako wanaweza wakaingilia kati, na ugomvi wako na mume wako utazidi kupanuka. Hatimaye labda unaweza kuachika ambapo wewe utapata hasara zaidi kuliko mume wako. Inawezekana ukaendelea kuishi peke yako katika uhai wako wote. Kwa hakika utajuta kutalikiwa.
Mwanamke alisema: “Kipindi fulani kilichopita niliolewa. Sikuwa na uelewa mzuri kuhusu kumtunza mume wangu na yeye hakuwa na ujuzi wa kutosha kunitunza mimi. Ilikuwa tabia yetu kugombana kila siku. Wiki moja nilikiwa sisemi naye na wiki moja baadaye alikuwa hataki kusema na mimi.
Mnamo siku za Ijumaa tu, tulikuwa tunaelewana, kupitia kwa upatanishi wa marafiki na ndugu. Pole pole mume wangu alikasirishwa na mimi na alifikiria kunitaliki na kuoa mke mwingine. Kwa kuwa nilikuwa na umri mdogo, sikuwa tayari kubadilika na sikukataa kutalikiwa. Tuliachana na mimi nilipanga nyumba ya kwangu mwenyewe. Baada ya muda mfupi nikatambua hatari. Watu wengi niliokutana nao lengo lao kubwa lilikuwa kunidanganya. Niliamua kupatana na mtaliki wangu na nilikwenda nyumbani kwake. Huko nilimkuta mwanamke ambaye alijijulisha kwangu kama mke wa mtalaka wangu. Nililia njia yote nilipokuwa narudi kwangu. Nilijuta kwa nini nilikubali kuachika, lakini nilichelewa sana.”
Mwanamke mwenye miaka ishirini na mbili, alimpeleka mtoto wake kwa wazazi wake, baada ya kuachika, alijaribu kujiua muda wa usiku, siku ya harusi ya dada yake.
Mama mpendwa! Lazima kwa kweli uepuke kumnunia na kukataa kusema na mumeo. Kama mumeo amekutibua uwe mvumilivu. Ukisha tulia na kuwa makini, ongea naye kwa upole kuhusu kukasirika kwako. Mathalan, unaweza kumwambia: “Ulinifedhehesha jana, au ulikataa kusikiliza matakwa yangu… Hivi ni haki kwamba unaweza kunitendea hivyo?”
Njia kama hivyo, si tu inakupumzisha kwenye hisia zako, bali pia itampa onyo. Kwa hiyo, mumeo atajaribu kurekebisha tabia yake na atakuheshimu kwa tabia yako njema. Matokeo yake atapitia upya tabia yake, na atajaribu kuwa na nidhamu.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wakati Waislamu wawili wakikataa kusemeshana na wasipopatana kwa muda wa siku tatu, wote wawili watakuwa wamevua joho la Uislamu, na hapatakuwepo na urafiki wowote baina yao. Halafu yeyote miongoni mwao ambaye ataanza kupatana na mwenzake, siku ya ufufuo ataishia Peponi (haraka kuliko mwenzake.)”

Comments

Popular posts from this blog

NAMNA YA KUSWALI HATUA KWA HATUA

UTUKUFU WA MJI WA MAKKA NA MSIKITI MTUKUFU

Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1