Heshima Ya Mume

Hamu ya kuheshimiwa ni jambo la asili, lakini si kila mtu yupo tayari kuitoa. Mumeo hukutana na watu wengi katika shughuli zake wakati hayupo nyumbani. Baadhi ya watu hao wanaweza kuwa hawana staha na kumfedhehesha hali ambayo hatimaye humtibua mtu.
Wewe kama mke wake, anakutarajia wewe kuonesha heshima na ari akiwa nyumbani na kwa hali hiyo unaipandisha hadhi ya nafsi yake iliyokanyagwa.
Kumstahi na kumheshimu mume wako hakukudhalilishi wewe, lakini huongeza nguvu na mwelekeo kwenye harakati za kuyafanya maisha kuwa bora. Kila mara unatakiwa umsalimie na kwa hayo maamkizi yako mfanye ahisi unamjali. Usiingilie kati mazungumzo yake. Uwe na adabu na mpole unapozungumza naye na usimpigie makelele. Inapotokea wote wawili mnakwenda kwenye mkutano ngoja mumeo aingie kwanza. Msifie mbele ya watu wengine. Waambie watoto wenu kumheshimu baba yao na uwakaripie kama hawaoneshi adabu kwake. Mheshimu mbele ya wageni na uwe makini kwa mahitaji yake, na yale ya wageni.
Anapogonga mlango jaribu kufungua mlango huku ukitabasamu na kuonesha uso wenye furaha. Tendo hili dogo la kuonesha furaha, athari yake ni kwamba huburudisha moyo na kumwondolea uchovu mumeo. Baadhi ya wanawake wanaweza kudhani kwamba tabia ya aina hiyo si ya kawaida. Fikiria unapomwamkia mumeo kama mgeni. Hii si tabia nzuri kwa sababu mumeo amekuwa kwenye harakati siku nzima kwa ajili ya ustawi wa familia yake na anastahiki kufikiriwa na kuheshimiwa anaporudi nyumbani. Maamkuzi hayo ya kwanza huleta picha nzuri sana, na lililo zuri kwa mgeni ni zuri pia kwa jamaa wa familia.
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wajibu wa mwanamke ni kujibu hodi ya mlangoni na kumkaribisha mume wake.”
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwanamke anayemheshimu mume wake na hamsumbui, atapata bahati na mafanikio.”
Mtukufu Mtume (s.a.w) alisema: “Mke anawajibika kutayarisha beseni na taulo ili mumewe anawe mikono.”
Uwe mwangalifu usije ukamfedhehesha mumeo, usizungumze naye kwa ukali, usimtukane, uwe msikivu kwake na usimuite kwa majina machafu. Ukimkosea na yeye atakufedhehesha wewe. Hatimaye, moyo wa mapenzi na kuaminiana utamomonyoka. Kwa hiyo, mtagombana mara kwa mara na kubishana, hali ambayo itasababisha mtalikiane.
Hata kama mtaendelea kuishi pamoja, maisha yenu kwa hakika yatajaa fujo. Hisia za uadui na usumbufu wa kisaikolojia unaweza kuanza kujengeka hadi kufikia kiwango cha kuhatarisha maisha ya wanandoa na hali hiyo inaweza kusababisha uhalifu. visa vifuatavyo vinaonesha baadhi ya mambo haya:
“Mtu mmoja mwenye umri wa miaka ishirini alimchoma kisu mkewe mwenye umri wa miaka kumi na tisa hadi akafa kwa sababu mke alimtukana mume. Mahakamani mume alisema; ‘nilimuoa mwanamke huyu mwaka moja uliopita. Mwanzoni mke wangu alinipenda sana. Lakini baada ya kipindi kifupi mke wangu alibadilika na kuanza kunidhalilisha.
Alianza kutumia lugha ya matusi kwangu kila ilipowezekana na kwa sababu ndogo sana, alianza kunikebehi. Kwa sababu jicho langu la kushoto ni kengeza, akawa na desturi ya kuniita mimi ‘punda kipofu.’ Siku moja, akaniita ‘punda kipofu’ nilikasirika sana hivyo kwamba nilimchoma kisu mara kumi na tano.’ ”
“Mtu mwenye umri wa miaka sabini na moja (71) ambaye alimuua mkewe, alitoa maelezo yafuatayo: ‘Ghafla tabia ilibadilika kwangu na akaanza kutonijali mimi. Wakati mmoja akaniita ‘mtu nisiyevumilika.’ nikagundua kwamba alikuwa hanipendi tena, nikamshuku na nilimuua kwa kumkata shoka mara mbili.”

Malalamiko Na Manung’uniko

Hakuna mtu yeyote asiyekuwa na matatizo na manung’uniko kuhusiana na maisha ya kila siku. Kila mtu hupenda kuwa na mtu wa kumhurumia ambaye anaweza kuwa mwandani wake na kumsikiliza matatizo yake. Lakini jambo la kukumbuka ni kwamba “upo wakati na mahali kwa kila jambo.” Mtu lazima aelewe wakati muafaka na mahali pa kulalamikia. Baadhi ya wanawake wajinga na wabinafsi hawatambui kwamba waume zao wanachoka sana na fadhaa baada ya kazi ya siku nzima. Badala ya kungoja kwa muda wa saa moja au mbili ili apumzike na kupata nguvu, huanza kumshambulia kwa mfululizo wa malalamiko. Mathalani mke anaweza kusema:
“uliniacha mimi na watoto hawa maluuni na ukaenda zako. Ahmad amevunja kioo cha mlango wa chumba cha mbele. Watoto wetu wa kike walipigana. Makelele ya watoto wa majirani zetu yananiudhi kweli. Hasan hajifunzi hata kidogo na amepata maksi za chini sana. Nimefanya kazi sana leo najisikia nimechoka. Hakuna hata mtu wa kusikiliza kilio changu!
“Watoto hawa hawanisaidii hata kidogo kwa kazi za hapa ndani. Afadhali nisingezaa watoto kabisa! Unayo habari dada yako alikuwa hapa leo? Sijui tatizo lake nini; alikuwa anafanya mambo kama vile nimemeza urithi wa baba yake.
“Mungu na aninusuru kutoka na mama yako! Amekuwa ananisengenya. Nimechoshwa na wote hao. Pia nimejikata kidole leo kwa kisu na kuumia sana.
“Ingekuwa vema kama nisingekwenda kwenye harusi ya Muhamedi jana. Ungemuona mke wa Rashid! Alivyopendeza, ungeshangaa! Mwenyezi Mungu angenipa na mimi bahati kama hiyo! Wanaume wengine wanawapenda wake zao na huwanunulia vitu vizuri. Hao ndio waoaji wa kweli.
“Rashid alipoingia kila mtu alimpa heshima. Ni kweli kwamba watu hupendelea kuona tu vazi ulilovaa. Anacho nini ambacho mimi sina? Kwa nini ajioneshe mbele yangu? Ndio, anayo bahati kuolewa na mume ambaye anampenda, yeye si kama wewe!
“Siwezi kuvumilia kuendelea kuishi kwenye nyumba iliyolaaniwa, kukutunza wewe na watoto. Kwa hiyo fanya utakalo!”
Msimamo wa namna hi si sahihi. Wanawake wa aina hii hudhani kwamba waume zao huondoka kwenda kwenye pikiniki au burudani kila asubuhi. Wanaume hukutana na mamia ya matatizo kila siku. Bibi mpenzi! Hujui mumeo amepita kwenye mambo gani anapokuwa katika kazi yake. Hujui ni watu fidhuli na wenye karaha kiwango gani mumeo ameshughulika nao siku nzima. Kwa hiyo, anapokuja nyumbani usiwasilishe malalamiko yako yote kwa wakati moja. Usimfanye ajihisi kuwa imekuwa hatia kuwa mwanamume.
Uwe na wastani na umfikirie. Endapo kwa kunung’unika kwako na kumsumbua, kutamuongezea wasi wasi na machungu, basi, ama anaweza akaanza ugomvi au akaondoka hapo nyumbani na kwenda kwenye mgahawa au filamu au hata kutembea tu mitaani.
Kwa hiyo, ewe Bibi mpenzi! Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, acha mazoea haya ya kulalamika hata wakati usio muafaka. Tafuta muda unaofaa na halafu mpe matatizo yako ambayo ni ya kweli, si kwa kulalamika, lakini fanya hivyo, kwa namna ya kushauriana. Kwa njia hii, hutasababisha yeye kuanza kujenga hisia za uadui na mapatano ya familia yanabaki kuwa salama.
Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema:
“Sala za mwanamke anayemchokoza mume wake kwa ulimi wake, hazikubaliwi na Mwenyezi Mungu hata kama akifunga saumu kila siku, anaamka kila siku usiku kufanya ibada, anawaachia huru watumwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mwanamke mwenye ulimi mbaya ambaye humuumiza mumewe kwa njia hii, ni mtu wa kwanza kuingia Jahanamu!”
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Wanawake wa Peponi huwaambia wanawake wanaowatukana waume zao kwa njia hii: ‘Mwenyezi Mungu na akuuweni. Msiwe watovu wa adabu kwa waume zenu. Mtu huyu (mume) si kiumbe wako, na wewe hustahiki kuwa naye. Muda mfupi ujao atakuacha na atakuja kwetu.’ ”
Sijui wanawake wa aina hii wanataka kujipatia nini kwa hayo manung’uniko yao. Kama wanataka kusikilizwa na waume zao au kujionesha, basi, hakika wanajipatia kitu kinyume chake kabisa na kumkasirisha. Kama wanakusudia mateso kwa mume, kumsababishia madhara ya kisaikolojia na kumuingiza kwenye mazoea bandia ya kuangamiza, basi wapo kwenye njia potofu.
Bibi mpendwa! Kama unamjali mumeo na familia yako, basi ni lazima uache msimamo huu usio na mantiki. Je, umewahi hata kufikiria kwamba mwenendo wako mbaya unaweza ukasababisha kuvunjika kwa maisha ya familia yako?
“Daktari mmoja alitoa ushahidi mahakamani: ‘Sijapata kumuona mke wangu akifanya mambo kama mke sahihi wa nyumbani wakati wote wa ndoa yetu. Nyumba yetu mara nyingi imekuwa katika machafuko.Wakati wote mke wangu anapiga makelele na kutukana. Nimechoshwa naye.’ Baada ya kumlipa mke wake fedha nyingi tu, akapata talaka. Akasema kwa furaha: ‘Kama angetaka na angeomba utajiri wangu wote na hata shahada yangu ya taaluma ya tiba, ningempa ili niachane naye haraka sana.’ ”

Tabia Za Kupendeza

Mtu yeyote mwenye tabia njema na inayopendeza pia angepata dhiki na matatizo ya maisha kwa njia ile ile. Hawa ni aina ya watu ambao watu huvutiwa nao na wanawatafuta wakati wote. Tabia inayopendeza na msimamo wa mtu utakuwa na kinga dhidi ya maradhi ya kisaikolojia kwa kuwa kuonekana kwao katika maisha ni kushinda matatizo yao kwa njia nzuri iwezekanayo.
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Hakuna maisha yanayo kubalika zaidi kuliko yale ambayo yanatokana na tabia njema.”
Lakini mtu mwenye tabia mbaya naye pia angeyaona maisha hayafurahishi kwani uhusiano wa watu hao kuendeleza wasiwasi na fadhaa.
Mtu kama huyu hupenda kulalamika na kupigia kelele maisha. Msimamo wa namna hii huepukwa na watu wengi ambapo mtu huyo hapati marafiki wengi. Hii ndio hali ambayo huathirika kwa urahisi na matatizo mbali mbali ya kisaikolojia na maradhi mengineyo kwa sababu ya wasi wasi na utupu ambao mtu mwenye msimamo mbaya anavyoyaona maisha.
Mtukufu Mtume (s.a.s) alisema: “Mtu mwenye tabia na msimamo mbaya atakuwa kwenye masumbuko na mateso wakati wote.”
Msimamo mzuri na unaopendeza ni muhimu kwa watu wote kwa ujumla na hususan baina ya wanandoa kwani wanandoa lazima wawe pamoja.
Mpendwa Bibi! Kama unataka kufurahia maisha ya furaha na mumeo na watoto wako, ufanye msimamo wako na tabia ya kupendeza vikubalike. Uwe na tabia njema na si mgomvi. Unao uwezo wa kuifanya nyumba yako kuwa Pepo ya hali ya juu au Jahanamu iwakayo moto. Unaweza kuwa malaika wa huruma ambapo mumeo na watoto wanaweza kupata amani kupitia kwako.
Unajua utaacha mvuto wa kupendeza kiasi kwenye roho zao kwa huo msimamo wako wa kutabasamu na lugha nzuri.
Mvuto wa kupendeza ni mbichi katika akili zao wanapoondoka kwenda shuleni au kwenye shughuli za kazi na unawasaidia wao kuwa na mwanzo mzuri wa siku.
Kwa hiyo, kama unajali kuhusu sifa nzuri ya maisha yako na uhusiano ulio nao na mumeo, usiwe kinyume na tabia njema. Uwe dhahiri katika msimamo wako na tabia inayopendeza kwani nguzo bora zaidi ya kutegemea kwa usalama wa ndoa ni maadili mazuri ambayo yanaelekeza kwenye tabia inayopendeza.
Namna nyingi za talaka ni kwa sababu ya tabia zisizolingana za mume na mke. Takwimu juu ya talaka kwa uthibitisho zinaonesha kwamba msimamo wa kupatana, maadili mema na tabia ya kupendeza, hazikuwepo kwa wanandoa husika. Chanzo kikubwa cha ugomvi na kutokuelewana kwa wanandoa ni kwa sababu yakutolingana kwa tabia na kanuni za maadili za wanandoa. Takwimu zifuatazo zinavutia:
“Mwaka 1968 kesi za malalamiko ya ndoa zilizowasilishwa mahakamani zilikuwa 16,039, kesi 12,760 miongoni mwa hizo, misingi ya malalamiko yao ilikuwa kutokulingana kwa kanuni za maadili. Mwaka 1969 kesi za malalamiko ya aina hiyo hiyo 16,058 liziwasilishwa mahakamani, kesi 11,246 miongoni mwa kesi hizo, misingi ya malalamiko ilifanana na ile ya kesi za mwaka wa nyuma. Kwa hiyo, inathibitika kwamba zaidi ya asilimia sabini ya ugomvi wa kifamilia ulisababishwa na kipengele hiki.”
Mwanamke alilalamika kwenye Baraza kwamba mume wake kila siku alikuwa na desturi ya kula chakula chake cha mchana na jioni nje.
Halafu mwanaume akaeleza kwamba sababu iliyomfanya ale nje ni kwamba mke wake hakuwa mbunifu hata kidogo na alikuwa mwenye tabia isiyopendeza kuliko wanawake wote wenye tabia kama hiyo hapa duniani. Haraka sana mwanamke alinyanyuka na kuanza kumpiga mume wake mbele ya majaji.”
Mwanamke huyu mpumbavu alidhani kwamba angebadilisha tabia ya mume wake ya kula chakula chake nje badala ya nyumbani kwa kulalamika, kutukana na kumpiga.
Lakini mwanamke huyu hakutumia mbinu rahisi na ya kiakili ambapo alitakiwa kuwa na busara zaidi na kuzingatia mwenendo unaostahili.
Mwanamke mwingine alipeleka taarifa mahakamani kwamba mume wake aliacha kusema naye kwa muda wa miezi 15 na kwamba alikuwa anatoa matumizi yake kupitia kwa mama yake (mume). Mume alijibu kwamba alikwisha kinai na msimamo usiopendeza wa mke wake ambao ulimfanya yeye asizungumze naye kwa miezi.”15
Migongano mingi ya kifamilia inaweza kusuluhishwa kwa wema, huruma na tabia inayopendeza. Kama mume wako si mwema, kama anatoka kwenda kula chakula cha jioni peke yake, kama anapenda kutumia lugha ya matusi, anatumia utajiri wake wote vibaya, hupenda kusema suala la kutalikiana na kutengana au sababu kadhaa katika ugomvi wa kifamilia, ipo njia moja tu ya kusuluhisha. Njia hii ni kuwa mwema na tabia njema. Matokeo ya mazoea ya tabia kama hii ni ya kimiujiza.
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwenyezi Mungu Mweza wa yote atampa mtu mwenye tabia ya kupendeza thawabu zinazolingana na zile za Jihadi. Atamneemesha kwa wingi mtu huyo usiku na mchana.”
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwanamke yeyote anaye msumbua na kumtesa mumewe yu mbali na neema za Mwenyezi Mungu na mwanamke yeyote anayemheshimu, anaye mtii na hamhuzunishi mumewe, ameneemeka na kufanikiwa.”
Ipo hadith inayosema kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alipewa taarifa ya mwanamke mwema ambaye alifunga saumu kila siku na alikuwa anafanya ibada kila siku usiku akimuabudu Mwenyezi Mungu, lakini alikuwa na tabia isiyo pendeza ya kuwaudhi majirani zake kwa maneno yake makali. Mtukufu Mtume alisema: “Hapana jema kwake huyo na yeye ni mkazi wa Jahanamu.”

Matarajio Mabaya

Mpendwa Bibi! Wewe ni mwanamke mkuu wa familia yako. Uwe na hekima na uweledi. Panga vizuri matumizi yako. Panga bajeti ya matumizi yako kwa njia ambayo haitasababisha hasara kwa utajiri na hekima yako.
Usishindane na wengine na uwaonee wivu. Kama unaona nguo nzuri imevaliwa na mwanamke, au kama unavutiwa na fanicha na vyombo ambavyo umeviona kwenye nyumba ya rafiki, usimlazimishe mumeo kununua vitu kama hivyo ambavyo vinazidi uwezo wake wa kifedha na pengine atalazimika kukopa. Je, si vema zaidi kungoja hadi hapo ambapo hali ya kipato itaruhusu au itakapopatikana akiba ya ziada ya kuwezesha kununua vitu visivyo vya muhimu?
Mara nyingi ni wale wanawake wajinga na wanaojipendelea ambao hushindwa, na kuwa wabadhirifu na kutaka kushindana. Wanawake wa aina hii huwalazimisha waume zao kuingia kwenye madeni na huchoshwa na kukasirishwa na kujaribu kuridhisha matakwa yao yasiyo weza kutoshelezwa. Wakati mwingine, ufumbuzi wa aina moja tu uliopo kwa wanaume wa kutatua matatizo haya ni uamuzi wa kumtaliki mke au kujiua.
Wanawake ambao hawatambui madhumuni ya kweli na maana ya ndoa na badala yake wanaifikiria kama utumwa ambapo mwanamume anapatikana kwa lengo la kutimiza matamanio yao ya kitoto na mahitaji ya kiulimwengu.
Wanawake wa namna hii wanataka mume ambaye atawahudumia kama mtumwa na hawatapinga njia zao za matumizi. Wanawake wa aina hii mara nyingine huenda mbali zaidi. Wanawafanya waume zao watumie zaidi ya uwezo wao hali ambayo inaweza kuwafilisi, wanaweza kufanya mauaji au matokeo yoyote ya msiba.
Wanawake wa aina hii ni aibu kwa wanawake wenzao. Endapo matarajio yake makubwa yanasababishwa kutalikiana, mwanamke atanyang’anywa mapenzi ya watoto wake na ataishi maisha ya upweke.
Kwa wanawake wa aina hii si rahisi kuolewa tena kwa urahisi. Hata kama inatokea, hakuna uhakika wa ndoa ya pili kama itadumu, kwani binadamu wengi hawapendi kuwekwa katika utumwa. Na mume mpya inawezekana naye asiwe na uwezo wa kutimiza mahitaji yao kabisa kuliko hata wa mwanzo.
Mpendwa Bibi! Badala ya kuwa mwenye tamaa sana, jaribu kuwa mwenye busara. Tumia muda mwingi na juhudi kwa ajili ya ustawi wa familia yako na mumeo badala ya kujaribu kuiga mambo ya kila mtu. Kama mumeo anaumia kupita kiasi, mzuie na udhibiti matumizi yake yasiyo ya muhimu. Badala ya kununua bidhaa zisizo za muhimu, ni vema kuweka kiasi fulani cha akiba kwa ajili ya matatizo ya siku za usoni.
Katika hadith Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke yeyote ambaye halingani na mume wake na humshawishi afanye mambo zaidi ya uwezo wake, basi matendo yake hayatakubaliwa na Mwenyezi Mungu, ataonja ghadhabu ya Mwenyezi Mungu mnamo Siku ya Ufufuo.”
Katika hadith nyingine, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke yeyote asiyelingana na mumewe, haridhiki na kile ambacho Mwenyezi Mungu amewajaalia na humtendea mume wake ubaya kwa kudai ampe zaidi ya uwezo wake, basi matendo yake (au ibada ya mke) hayakubaliki kwa Mwenyezi Mungu na Atamkasirikia mwanamke huyo.”
Katika hadith nyingine, Mtume (s.a.w.w) alisema: “Baada ya kumwamini Mwenyezi Mungu, hapana neema iliyo kubwa zaidi ya kuwa na mume au mke mnayeelewana naye.”

Uwe Faraja Kwa Mumeo

Uzito wa mzigo wa maisha huchukuliwa na wanaume kwa sababu wao wanao wajibu wa kutunza na kusaidia familia zao. Katika kutimiza wajibu huu, mwamaume wa familia lazima akabiliane na matatizo mengi na vikwazo vingi nje ya familia yake. Baadhi ya matatizo haya yanaweza kuwa ukubwa wa kazi, mizozo kwenye msongamano wa magari na usumbufu wa kungoja na kupanda mabasi kutoka nyumbani kwenda ofisini na kurudi nyumbani, wasiwasi kuhusiana na masuala ya marafiki nawafanyakazi wenzake na wasiwasi wa kiuchumi na kisiasa ya siku hiyo, wasi wasi wa marafiki na wafanya kazi wenzake, na wasiwasi wa kujaribu kuboresha hali ya maisha ya familia yake. Kiasi cha mishughuliko na wasiwasi wa mtu mwenye kuwajibika ni mikubwa na yenye sehemu nyingi. Si jambo la kushangaza kwamba wastani wa umri wa mwanaume ni mdogo zaidi ya ule wa mwanamke.
Ili mwanadamu aweze kwenda sambamba na mizigo ya maisha ni muhimu kuwa na mtu ambaye atakusikiliza na kukuhurumia. Mumeo ni mmoja wapo wa watu hao. Anaweza akahisi yu mpweke na akahitaji kupata kimbilio na faraja akiwa katikati ya misukumo hii. Ni kawaida kwamba mwanaume hutarajia kupata faraja na utulivu kutoka kwa mke wake na familia yake. Kwa hiyo, tazamia matarajio na mahitaji yake.
Uwe mkunjufu na mchangamfu wakati ambapo kwanza ndio anarudi nyumbani kutoka katika kazi zake, na apate viburudisho au umfanye ahisi kwamba wewe upo tayari kusikiliza mahitaji yake. Jaribu kutokumwingiza kwenye shari kwa kuanza kumlaumu mara tu umuonapo.
Ngoja apumzike na apate nguvu upya kabla ya kumweleza madai binafsi ya watu wa familia.
Mumeo anapokuja nyumbani, jaribu kutabasamu na kumsalimia kwa uchangamfu. Mtimizie mahitaji yake ya kimwili ya uchovu, njaa na kiu. Halafu muulize kuhusu matatizo yake. Kama hayupo tayari kusema uwe msikilizaji mzuri na umhurumie. Jaribu kuonesha kuhusika kwako kwa dhati na halafu umsaidie kutambua kwamba matatizo si kwamba hayawezekani, na makubwa kama anavyodhani. Mpe moyo wa kumuunga mkono na kumsaidia aweze kukabiliana na masuala ipasavyo. Unaweza kusema kitu kama: “Matatizo haya yanawapata watu wengi. Kwa utashi na uvumilivu, inawezekana kuyatatua matatizo almuradi mtu asiruhusu yamshinde. Matatizo haya, kwa kweli ni mitihani na pia hujenga tabia ya kweli ya mtu. Usikate tamaa. Unaweza kuyatatua kwa kuazimia na ustahamilivu.
Kama unayo mawazo fulani kuhusu jinsi ya kuyashughulikia, mwaambie mumeo. Kama huna, labda unaweza kumshauri amuone rafiki mzuri ambaye anao ujuzi na sifa zaidi.
Mpendwa Bibi! Wakati wa matatizo, mumeo anahitaji sana umjali na mapenzi yako. Unatakiwa umsaidie na umtunze kama mtaalamu wa maradhi ya akili na mke mwenye huruma. Kiwango gani cha matunzo mtaalamu wa maradhi ya akili angempa ambacho na wewe ungempa? Usikadirie pungufu uwezo wako wa kumtuliza na kumpa nguvu. Hakuna mtu muaminifu na mwenye kuhusika zaidi kuhusu ustawi wa mumeo isipokuwa wewe. Ataweza kupata nguvu kutokana na mapenzi yako kwake na aweze kukabiliana na matatizo yake kwa hali ambayo itapunguza mhemuko wake na wasiwasi wa akili. Hatimaye, mapatano ya kuheshimiana na upendo utakuwa mkubwa zaidi.
Katika hadith, Imam Sadiq (a.s) alisema: “Hakuna kitu bora zaidi duniani kuliko kuwa na mke mwema. Na mke mwema ndiye huyo ambaye mume wake hufurahi pindi amuonapo.”
Kwenye hadith, Imam Rida (a,s) alisema: “Lipo kundi la wanawake ambalo huzaa watoto wengi. Ni wanawake wema na wana huruma. Huwasaidia waume zao wakati wa matatizo na katika mambo ya dunia hii na ile ijayo. Wanawake hawa hawafanyi matendo yoyote ambayo yangewapa hasara waume zao kuongeza matatizo yao.”

Comments

Popular posts from this blog

NAMNA YA KUSWALI HATUA KWA HATUA

UTUKUFU WA MJI WA MAKKA NA MSIKITI MTUKUFU

Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1