Haki Za Kinidhamu Za Mume

Ingawaje mume na mke ambao hutengeneza maisha ya pamoja ya familia, hugawana na kushirikiana katika kuendesha mambo ya nyumba yao, wanaweza kuwa na maoni tofauti kuhusu mambo fulani. Mwanaume anaweza kuhisi kwamba ni yeye ndiye anayetakiwa kuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu mambo ya familia, bila kupata upinzani kutoka kwa mke wake.
Wakati huo huo mke wake anaweza akakataa kazi yake kama upande uliomtiifu. Ubishi na ugomvi unaweza ukaanza kwa sababu kila upande unajaribu kuanzisha mamlaka juu ya upande mwingine. Suluhu nzuri zaidi ya tatizo kama hili ni kwamba pande zote zinatakiwa kuacha kujionesha kama unao mamlaka makubwa zaidi kuzidi upande mwingine, na kujaribu kupata ufumbuzi wa matatizo yao kwa njia ya mazungumzo na uelewano wa kina. Hii inawezekana tu kufanikiwa kama pande zote zinaacha ukaidi.
Baadhi ya wanamume huwaamuru wake zao kufanya mambo mengi na kama wakikabiliwa na upinzani, wanadhani ni sahihi kuwashika, kuwaadhibu au hata kuwapiga wake zao. Msimamo huu si sahihi kabisa. Mwanaume wa kipindi cha ujahiliya ambaye alipungukiwa ubinadamu, alifanya mazoea ya kuwapiga na kuwaumiza wake zao.
Mtukufu Mtume (s.a.w) alipiga marufuku kuwapiga wanawake, isipokuwa katika hali isiyozuilika ambapo adhabu huwa wajibu.”
Mtume (s.a.w) pia alisema Nina shangazwa na mwanaume anaye mpiga mke wake, ambapo ni yeye mwenyewe, zaidi ya mke wake ambaye anastahili kupigwa. Enyi watu, msiwapige wanawake zenu kwa kutumia fimbo kwa sababu tendo la namna hiyo lina ulipizaji kisasi.”
Kumuonea mwanamke ambaye kwa utashi wake amekubali kuolewa na mwanamume, ambaye anataka kupata faraja na utulivu na yeye, na ambaye anamtarajia mume wake kushirikiana wote katika matatizo, si sahihi. Kwa kweli Mwenyezi Mungu anamdhamini mwanamke kwa mume wake kwa njia ya ndoa na maonevi ya mwanaume kwa mke wake ni kutokuwa mwaminifu kwa dhamana ya Mwenyezi Mungu.
Imam Ali (a.s) alisema; Wanawake wamedhaminiwa kwa wanamume na kwa hiyo, wao si wamiliki wa bahati zao au mabalaa yao. Wao wapo na nyinyi kama dhamana ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo msiwaumize na msifanye maisha yao kuwa magumu.”
Mwanaume ambaye humpiga mke wake, hulazimisha uharibifu kwenye roho hivyo kwamba anaweza akapata mateso yasiyo elezeka na upendo wa familia na uchangamfu unaweza ukatoweka kabisa. Mwanamume mwenye ghadhabu anaweza kudunisha uhusiano mzuri wa ndoa na mke wake na kushushiwa hadhi? Hii kwa kweli ni aibu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Enyi wanaume! Inawezekanaje yeyote miongoni mwenu ampige mke wake na baadaye amkumbatie?”
Mwanaume, isipokuwa awe na haki ya pekee kwa mke wake, inayofanana na zile ambazo zitatajwa kwenye sura hii haruhusiwi kisheria kumlazimisha mke wake kufanya jambo lolote au kukimbilia matumizi ya kipigo kuhusu utovu wa utiifu. Mathalani mwanamke kisheria hawajibiki kufanya kazi za nyumbani kama kufagia, kupika, kufua, kutunza watoto, kushona na kadhalika. Licha ya kuwa wanawake walio wengi hufanya kazi hizi za mama wa nyumbani kwa kutaka wao wala si za lazima.
Wanaume wanatakiwa kuwashukuru wake zao kwa kazi zao za ndani ya nyumba. Kwa hiyo, hapana mwanamume mwenye haki ya kuhoji au kumwadhibu mke wake anapokabiliwa na kukataa kwake kutekeleza kazi za nyumbani.
Uislamu unapendekeza adhabu ya kipigo kwenye mifano miwili tu ambapo hali zake hukiukwa:
Mfano wa kwanza; Mwanaume ameruhusiwa kisheria katika Uislamu kupata na kutoshelezwa na tendo la Ndoa na kupata starehe ya kila aina kutokana na uhusiano huu na mke wake. Mke anawajibika kisheria kukubali matamanio ya ngono kutoka kwa mume wake. Kama mwanamke anakataa kumtosheleza mume wake, mume katika hatua ya kwanza anatakiwa amshawishi katika njia na mpangilio unaostahili. Hata hivyo, kama mwanaume anahisi kwamba mke wake anataka kuleta hali hiyo, basi kwa kuchunguza hatua zilizo bainishwa anaweza kumwadhibu.
Mwenyezi Mungu anasema:

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنْفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّهُ ۚ


{34}
“Wanaume ni wasimamizi wa wanawake kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanao jitihada hata katika siri kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde.”
(Quran 4:34).
Kwa hiyo, Qura’ni inamruhusu mume kumpiga mke wake kama hatua ya mwisho ya kutoa adhabu, kama inatokea mke anaonesha tabia mbaya kwa mume wake kuhusu matakwa yake ya ngono.
Hatua ya kwanza ni kutoa ushauri. hatua ya pili; Mwanaume aache kulala kitanda kimoja na mkewe au amgeuzie mgongo na kwa njia hii anatakiwa kuonesha hasira yake. Kama hakuna jibu linalotarajiwa hadi mwishoni mwa hatua ya pili na bado mwanamke anaendelea kukataa, mume anaruhusiwa kumpiga mke wake kidogo.
Mume, hata hivyo, haruhusiwi kuvuka mpaka uliowekwa na kukimbilia kumuonea. Wanaume wanakumbushwa kuhusu yafuatayo: Lengo la adhabu ya kipigo kwa mke wa mtu linatakiwa kuwa njia ya kumuelimisha na si kulipiza kisasi.
Kipigo kinatakiwa kufanywa kwa kutumia mkono au mti mwembamba na mwepezi.
Kipigo kikali cha kuweza kubadilisha rangi ya ngozi kuwa buluu au nyekundu hakiruhusiwi na mhusika lazima apigwe faini (dia).
Kupiga sehemu nyororo na nyeti za mwili kama vile macho, kichwa tumbo na kadhalika, hakiruhusiwi.
Adhabu ya kipigo haitakiwi kuwa kubwa mno hivyo kwamba haitasaidia kuanzisha hasira na fikra mbaya miongoni mwa wanandoa kumwelekeza mke kwenda kwenye kiasi cha kutotii zaidi.
Mwanaume (anaye nuia kumwadhibu mke wake kwa kutumia njia hii) anatakiwa kukumbuka kwamba ataendelea kuishi na mke wake na kwamba upendo wa familia usiharibiwe.
Mwanaume haruhusiwi kumpiga mke wake kama zipo sababu halali zilizomfanya asikubali matakwa yake.
Mathalani kama mke yupo kwenye siku zake za hedhi, saumu ya mwezi wa Ramadhani, awe amevaa vazi la Hija (Ihram) au mgonjwa. Sababu hizi zinakubalika na mwanamume hawezi kumwadhibu mke wake kwa kukataa matamanio yake kwa sababu hizo zilizotajwa.
Mfano wa pili; Mwanamke anaweza kutoka nje hapo tu ambapo ameruhusiwa na mume wake. Akitoka nje bila ruhusa hairuhusiwi kisheria na kufanya hivyo ni dhambi.
Hadith imesimuliwa kwamba Mtume (s.a.w.w) hakumruhusu mwanamke yeyote kutoka nje ya nyumba yake bila ruhusa ya mume wake. Alisema; Mwanamke yeyote ambaye hutoka nje ya nyumba yake bila ruhusa ya mume wake, atapata laana kutoka kwa malaika wote walioko mbinguni na wote wale wanao muona, wawe majini au wanadamu, hadi anaporudi nyumbani kwake.”
Hii ni hali ya mume yeyote ambayo lazima iangaliwe na wake zao.
Lakini wanaume hawatakiwi kuwa wakali sana kwa wake zao. Ni bora zaidi wao kuwaruhusu wake zao kutoka nje kila inapowezekana.
Hali hii ya wanaume haimaanishi kuonesha nguvu au kujaribu kuwashinikiza wake zao, lakini ni njia ya kuwazuia wanawake wasiende kwenye sehemu zisizo pendeza na zisizofaa.
Kuwa mkali sana si tu kwamba ni jinsi isiyofaa, lakini inaweza kuathiri uhusiano wa familia au hata kumsukuma mwanamke kuelekea kwenye utovu wa nidhamu na uovu.
Mwanaume lazima amzuie mke wake asiende kwenye sehemu za mikusanyiko zenye uovu na zisizofaa. Huu ni wajibu wa kidini kwa wanawake kuwatii waume zao. Mwanamke asiye mtiifu anaweza kuadhibiwa na mume wake. Hapa tena adhabu inatakiwa kutekelezwa hatua kwa hatua.
Hata hivyo, mwanamke anaweza kutoka nje ya nyumba yake kwa sababu maalum bila ya ruhusa ya mume wake na wanamume hawaruhusiwi kuwaumiza wake zao katika mifano kama hiyo: Kutoka nje kwa ajili ya kujifunza amri muhimu za dini.
Kutoka nje kwa ajili ya Hija pale ambapo anao uwezo muhimu wa kifedha na kutekeleza Hija.
Kutoka nje ya nyumba kwa ajili ya kulipa deni almuradi deni hilo haliwezi kulipwa bila kutoka nje.

Wanamume Wa Kutuhumu

Ni haki ya wanaume kuchunguza wake zao lakini si kwenye kiwango cha tuhuma na kutokuaminiana. Wanaume wengine hutuhumu na kutilia shaka uaminifu wa wake zao. Hii ni hatari na kufanya maisha kuwa magumu kwa familia yote.
Mwanaume anayesumbuliwa na tabia hii, wakati wote hutafuta dosari na kukusoa. Humfuatilia mke wake kwa karibu sana kwa humfuata kila aendako. Hupata ushahidi wa kusaidia sababu yake ya kutuhumu kutoka kwenye kila kitu. Kama akimuona au akiona picha ya mwanaume kwenye vitu vyake au akiona barua aliyoandikiwa na mwanaume au akimwona mwanaume anamtazama, atapata uhakika kuhusu kutokuaminika kwa mke wake. Kama mke wake akificha barua kutoka kwake, atadhani ni barua ya mapenzi. Asipoonesha mapenzi yake kama ilivyokuwa zamani atatilia shaka uaminifu wake.
Anaweza hata kufikiria kwamba kwa kuwa binti yake hafa nani na yeye, mke wake lazima alizini.
Mifano yote ya aina hii inaweza kuonekana kama uthibitisho imara wa udanganyifu wa mwanamke wa mume anayemtuhumu mke wake. hali huwa mbaya sana kama ndugu au rafiki akikubaliana na tuhuma yake.
Familia nyingi ambazo zimeathiriwa na maradhi haya, huteseka sana. Mwanaume anaweza kujishughulisha kama mpelelezi ndani ya nyumba. Na mke wake anaweza kuhisi kama vile alikuwa amefungiwa jela. Wote wawili wanaweza kupata maradhi ya kiakili na ndoa yake kuwa hatarini. Wanaweza hata kukimbilia kutalikiana au mauaji.
Ipo mifano mingi ya kuua na kujiua ambayo imetokea kutokana na tuhuma. Katika hali hii mwanaume na mke wake lazima watahadhari kuhusu uwezekano wa matokeo mabaya sana na kwa kutumia busara na utambuzi, huondoa hatari yoyote, ambayo ingetisghia ndoa yao au hata uhai wao. Wanatakiwa tu kuwa na tahadhari ya uwezekano wa hatari na kuweza kufikiri bila wasi wasi ili waweze kushinda matatizo yao.
Mwanaume anatakiwa kuacha ushabiki wake na wivu wa kupindukia. Lazima atumie mantiki. Lazima atambue kwamba kumtia hatiani mke wake kwamba ni mgoni si jambo dogo na kwamba madai ya aina hii huhitaji uthibitisho uliokamili.
Mwenyezi Mungu amesema kwenye Qurani Tukufu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ

ۖ

{12}
“Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi . . .”
(Quran 49:12).
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) alisema: “Yeyote awaye, ambaye atamshitaki kwa kumsingizia mke wake kwa kuzini atapoteza thawabu zake zote za matendo mema kama vile ambavyo nyoka huvua ngozi yake ya zamani. Na kwa kila unywele kwenye mwili wake, dhambi elfu moja zitaandikwa kwenye rekodi yake (kwa ajili ya siku ya hukumu).”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) pia alisema:
“Mtu yeyote ambaye atamshitaki mwanaume au mwanamke muumini kwa kumsingizia, Mwenyezi Mungu atamning’iniza kwenye lundo la moto ili apate adhabu ya dhambi yake siku ya Hukumu.” 201.
Alimuradi kutokuaminika kwa mwanamke hakujathibitishwa kwa ushahidi ulio thabiti, mwanaume hana haki yoyote ya kumshitaki, vinginevyo atakuwa anafanya dhambi ambayo, kufuatana na Uislamu ataadhibiwa kwa kuchapwa viboko themanini.
Ushahidi utokanao na dhana hauoneshi lolote. Barua za zamani, picha na kadhalika hazithibitishi lolote.
Kutunza vitu kama hivyo si sahihi, lakini hili ni kosa ambalo hufanywa na vijana wengi na si jambo la kujihusisha nalo kabisa.
Kama mwanamke anaonekana anazungumza na mwanaume mgeni, licha ya kwamba si sahihi yeye kufanya hivyo, jambo hili haliwezi kuaminika kuwa uthibitisho wa kutokuaminika kwake.
Hii ni kwa sababu inawezekana alifikiria ingekuwa ni jeuri kutokuzungumza na mwanaume huyo, au inawezekana mwanamume huyo hakuwa mgeni lakini alikuwa rafiki yake baba yake au kaka.
Kama mwanamke anampongeza mwanaume, ingawa asingefanya hivyo, inawezekana kuwa hiyo ilikuwa kurahisisha na kwa hiyo haiwezekani liwe tendo la kuonesha kutokuaminika kwake.
Kama mwanamke anasema uongo kuhusu uhusiano fulani au akificha barua zake, inawezekana iwe kwamba ipo sababu nzuri ya kufanya hivyo au anaweza kuogopa mashtaka ya mume wake yasio na maana.
Kama mwanamke amekuwa hamchangamkii mume wake, inawezekana ametibuliwa naye, inawezekana ni mgonjwa au anaweza kuwa na matatizo mengine.
Kwa ufupi, katika mazingira yote ambayo yanaweza kuonesha dalili za kutokuwa mwamnifu anaweza kupata sababu nyingi na nzuri zinazotengeneza uwezekano wa makosa yeyote kuwa bure.
Bwana mpendwa! Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu acha tabia ya kutuhumu. Jione wewe mwenyewe kuwa mwamuzi wa haki na ulione tatizo kimantiki. Pima kiwango cha uwezekano wa mkeo kutokuwa mwaminifu na uelewe kama ndivyo, ni tuhuma tu au hata la kuaminika?
Sisemi kwamba wewe usijali na uwe mzembe lakini unatakiwa kuchukua hatua kufuatana na ushahidi ulio nao na si zaidi ya hapo. Kwa nini ukuze tatizo kwa kufuata tuhuma isiyo na msingi na uyafanye maisha kuwa magumu kwako na familia yako. Wewe ungejisikiaje kama mtu yeyote angekushitaki kwa jinsi isiyo ya haki? Kwa nini ujifedheheshe mwenyewe na mke wako? Kwa nini usimhurumie mke wako? Imepata kukujia fikira kwamba hatimaye mke wako anaweza akukengeuka kwa sababu ya wewe kutokumwamini na mashitaka ya kumsingizia?
Imamu Ali (a.s) alimsimulia mwanae Imamu Hasan (a.s): “Uwe mwangalifu usifanye mambo kama mtawala ambapo haupo hivyo kwa sababu hii inawezekana kuwaelekeza watu wanaofaa kwenye dhambi”
Kama unamtuhumu mke wako, usimwambie mtu yeyote unayemuona, kwa sababu wanaweza kuthibitisha tuhuma yako kwa vile ni maadui zako, wepesi kuamini au uzembe. Wanaweza hata kuimarisha hutuma yako na kukusababishia ukosefu wa furaha katika dunia hii na akhera. Hususan, usimwambie mama yako au dada yako kwa sababu ni kawaida watakubaliana na wewe na kwa hiyo kuongezea tuhuma yako.
Lazima utafute ushauri kutoka kwa watu wenye busara na marafiki na ndugu wenye uzoefu.
Msimamo mzuri zaidi, hata hivyo, ni wewe mume kuzungumza na mke wako na mwambie akueleze. Lakini usitake kuthibitisha uhalifu wake. Sikiliza yale ambayo wanakuambia na uamue kama mwamuzi mwenye haki ambaye hana upendeleo.
Angalau ujaribu kumuamini na uchukulie kana kwamba shemeji yako wa kiume anakuletea ushahidi juu ya dada yako wewe kutokuwa muaminifu. Kwa nini ulishughulikie jambo hili bila huruma na kumuona mhusika kuwa mhalifu aliye thibitishwa?
Uwe na busara na uvumilivu, vinginevyo utamwacha bila sababu ya maana. Kama unavumili mateso ya kuwa mtalaka lakini unao uhakika gani kuhusu mke wa ndoa ijayo?
Bado utaendelea kuwa unatuhumu. Kosa lao ni nini kama ni wewe ambaye unasumbuliwa na maradhi haya? Uwe na busara na jaribu kuelewa tatizo lako mwenyewe.
Uwe na tahadhari usije ukajiua au kumua mke wako. Kwa sababu, utaharibu maisha yako hapa duniani na Mwenyezi Mungu Mweza atakuwadhibu huko Akhera.
Lazima uelewe kwamba kumwaga damu siku moja kitendo hicho kitajulikana halafu ama utanyongwa au utafungwa kifungo cha maisha.
Kama hutakubaliana na jambo hili basi tazama takwimu za waliotiwa hatiani.
Wake za wanaume wenye ugonjwa wa kutuhumu pia wanao wajibu mkubwa kuhusu familia zao. Wanawake hawa lazima wajitolee muhanga na kuthibitisha uwezo wao katika hali ngumu kama hiyo.
Mama mpendwa kwanza kabisa mume wako ameambukizwa ugonjwa wa hatari ambapo yeye, kwa kutaka yeye mwenyewe, huchukua hatua zisizo sahihi ambazo zingehatarisha familia yenu.
Lazima uoneshe mapenzi yako kwake kadiri uwezavyo. Lazima awe na uhakika kwamba ni yeye tu katika maisha yako. Uwe mvumilivu kuhusu tabia yake, usimpigie kelele, usikatae kusema naye na usiwe kaidi kwake.
Ukihisi kwamba anafuatilia barua zako au anadhibiti kurudi na kutoka kwako nyumbani, usifanye upinzani. Mwambie kila kitu, mwambie ukweli. Epuka kusema uwongo au kukanusha matukio ambayo yametokea.
Kama akigundua kwamba umemdanganya kuhusu suala lolote, ataona hilo kama uthabitisho kuhusu udanganyifu wako, ambapo haitakuwa rahisi kurekebisha uharibifu wake.
Kama mume wako mwenye maradhi ya kituhuma akikuzuia ushirikiane na mtu fulani au anataka ufanye kazi fulani, basi kubali neno lake vinginevyo sababu ya wasi wasi wake kwako itaimarika. Kwa ufupi epuka matendo yote ambayo yanaweza kumfanya akutuhumu.
Imamu Ali (a.s) alisema: “Yeyote anayejiweka wazi kwa shutuma, asiwalaumu wale wanao mtuhumu.”
Kama mume wako anaonesha chuki kwa mtu yeyote, lazima uache mawasiliano na mtu huyo kabisa.
Bibi mpendwa! Ni bora zaidi wewe kuiweka familia yako pamoja kwa lengo la kudumisha urafiki na watu wengine. Usidhani kwamba wewe ni mtumwa kwenye minyororo ya mume wako, lakini tambua kwamba bado wewe ni mke wa mwanaume.
Kumbuka ulipofanya mapatano ya ndoa na mume wako, ulikubali mgawo wote wa nyakati za furaha na huzuni katika maisha. Hivi itakuwa haki wewe kumtendea mabaya mume wako ambaye anaumwa maradhi ya kutuhumu? Weka pembeni mawazo yasiyo pevuka na uwe na busara. Kwa jina la Mwenyezi Mungu kujitolea kwako kwa kiwango chochote kwa ajili ya familia yako ni kitendo cha manufaa. Mwanamke mzuri ni yule anaye weza kuvumilia hali ngumu.
Imamu Ali (a.s) alisema: “Jihadi ya mwanamke ipo kwenye kuvumilia matendo ya kashifa na hamasa ya mume wake.”
Usifanye jambo lolote ambalo lingemfanya mume wako akutuhumu. Usiwatazame wanaume wengine.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: Mwenyezi Mungu atamkasirikia sana mwanamke aliyeolewa anayependa kuwatazama wageni.”
Usishirikiane na wanaume wageni. Usiondoke nyumbani bila ruhusa ya mume wako. Usipande magari ya wageni. Usafi wako tu peke yake hautoshi, lakini ungeepuka kitu chochote ambacho kingeamsha tuhuma ya mume wako. Inawezekana akutuhumu kwa mambo madogo sana kutokana na tabia yako.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 27 alisema mahakamani; Ilikuwa wakati wa baridi ya mwaka 1963, ambapo ilikuwa siku ya barafu niliingia kwenye gari la mjomba wa rafiki yangu. Aliniambia kwamba mjomba wake angenipeleka hadi nyumbani kwangu kwa gari lake. Nilikubali nikaingia kwenye gari lake. Tulipofika nyumbani mume wangu alikuwa amesimama karibu na mlango wa nyumba na kwa vile sikutaka mume wangu kuniona ndani ya gari la mtu mwingine nilimwomba mjomba wa rafiki yangu aendelee na safari na alifanya hivyo. Baadaye mume wangu ambaye alikwisha niona ndani ya gari hilo, aliniuliza kuhusu suala hili, lakini nilikanusha kila kitu. Akawa ananituhumu zaidi na ilifika kiwango ambapo hakuamini hata ushahidi wa rafiki yangu. Sasa ni miaka minane wala haishi na mimi ama kunipa talaka. Sijui hata la kufanya.”
Unadhani ni nani wa kulaumiwa katika hadith hii? Ningesema kwamba mwanamke ana hatia zaidi kuliko mume wake. Ni mwanamke ambaye kwa uzembe wake na wepesi wa fikira, alijiweka yeye na mume wake katika hali hii.
Kwanza, kabisa mwanamke hangekubali msaada wa lifti ya gari la mgeni kwani hilo si jambo sahihi kufanywa na mwanamke yeyote. Haistahili na ingeweza kuwa hatari.
Pili, hangefanya alivyofanya baada ya kumuoana mume wake. Angesimamisha gari na kumpa mume wake maelezo ya kina.
Tatu, mojawapo ya makosa ya mwanamke ilikuwa kumwambia dereva kuendelea na safari.
Nne, hangekataa baada ya kuulizwa. Angeeleza kila kitu katika hatua hii ya kuchelewa na ingesaidia kupata ufumbuzi wa tatizo.
Kama mambo yalivyo, pia mwanaume alikosea. Si lazima aone tukio hili kama ndio ushahidi wa kutoa uamuzi kuhusu hatia ya mke wake. Lazima afikirie uwezekano kwamba mke wake inawezekana alipanda gari la mgeni kwa uzembe na halafu labda kwa sababu ya woga alimwambia dereva asisimamishe gari na kama ilivyo kawaida akakanusha jambo lote.

Lazima apeleleze jambo hili mara atakapo hakikisha kwamba hana hatia, lazima awe msamehevu.

Comments

Popular posts from this blog

NAMNA YA KUSWALI HATUA KWA HATUA

UTUKUFU WA MJI WA MAKKA NA MSIKITI MTUKUFU

Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 1