Hadithi ni nini? Je utafafanua tofauti kati ya aya (ayah) na hadithi?
Aya maana yake ni sentensi ambayo mwanzo wake na mwisho uko wazi katika Quran. Kila aya ya Quran ni muujiza. Kila aya ni ushahidi kwa ajili ya uaminifu wa mtume aliyefikisha aya hiyo na somo la kupigiwa mfano kwa ajili ya wenye kufikiri, kutafakari na kuzingatia; kila aya ni ‘kitu cha ajabu’ kwa sababu ni muujiza na ina thamani.
Hadithi ni maneno, amali, idhinisho na sunnah za Mtume zinazojumuisha maadili yake na ubora wa kiutu ulioelezwa kwa maneno au maandishi. Kwa namna hii, hadithi ni kisawe cha sunnah.
Neno hadithi limeanza kutumiwa kuwa ni jina la jumla kwa ajili ya habari zilizoripotiwa kutoka kwa Mtume kwa mujibu wa muda.
Mjumbe wa Allah (s.a.w.) sio tu aliwapelekea watu ufunuo alioupokea kutoka kwa Allah bali pia aliwafafanulia ufunuo huo na kuutekeleza katika maisha yake yeye mwenyewe, kuwa ni mfano madhubuti kwao. Kwa hivyo, pia alikuwa akiitwa Quran hai.
Wanazuoni wa Kiisilamu kwa ujumla wanazizingatia hadithi zinazohusiana na masuala ya kidini kuwa zimefunuliwa na Allah kwa mtume na kuonesha aya ifuatayo kuwa ni ushahidi wa hilo:
“Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa; “(an-Najm, 53/3-4).
Kwa kuongezea, wanasema neno hikmah (hekima) lililotajwa katika aya ifuatayo linamaanisha sunnah:
“Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi.” (Aal-i lmran, 3/164)
Kwa hakika, baadhi ya masimulizi yaliyoripotiwa kutoka kwa Mtume na Maswahaba zake yameutanguliza ukweli huu. Yafuatayo yanaripotiwa kutoka kwa Mjumbe wa Allah:
“Nimepewa Kitabu kitukufu na mfano wake (sunnah)” (Abu Dawud, Sunan, II, 505).
Hassan Ibn Atiyya amefafanua yafuatayo kuhusiana na suala hili: “Jibril (Jibrilu) ameleta na kufundisha sunnah kwa Mjumbe wa Allah kama vile alivyoileta na kuifundisha Quran.” (Ibn Abdilbarr, Jamiu'l Bayani'l-ilm, II, 191).
Kama inavyofahamika kutoka kwenye aya na taarifa za hapo juu, Quran na hadithi (au sunnah kwa ufahamu mpana zaidi) ni sawasawa kwa upande wa kuwa ni ufunuo ulioteremshwa kwa Mjumbe wa Allah (s.a.w.) na Allah. Hata hivyo, Quran inatofautiana na hadithi kwa sababu ni jambo lisilowezekana kutoa kitu kama Quran kwa upande wa maana na maneno, inathibitishwa kwa maandishi katika ubao uliohifadhiwa (Lawh al-MafuzMahfudh), na sio Jibril wala Mtume (s.a.w.) anayeweza kubadilisha kitu ndani yake. Hadithi hazikuwa ufunuo kama maneno; na sio miujiza kama maneno ya Quran; inaruhusiwa kuiripoti kwa maana yake tu maadamu maana haibadiliki.
Kama ilivyo fiqh ni chanzo kinachotegemea ufunuo, hali ya hadithi kwa kulinganisha na Quran na kwa upande wa hukumu inayoileta ni kama ifuatavyo:
1. Baadhi ya hadithi zinathibitisha na kusisitiza hukumu ambazo Quran imezileta; kwa mfano, hadithi zinazokataza kuwaasi wazazi wawili, kubeba ushahidi wa uongo na kufanya mauaji.
2. Baadhi ya hadithi zinafafanua na kuzijalizia hukumu ambazo zimeletwa na Quran. Kusimamisha sala, kutekeleza hajj na kutoa zakah yote yameamrishwa katika Quran lakini haikuelezewa namna ya kutekelezwa. Tunajifunza namna gani ya kuyatimiza hayo kutoka katika hadithi.
3. Baadhi ya hadithi zimetoa hukumu kuhusu masuala ambayo Quran haikuyataja kabisa. Hadithi zilizokataza kula nyama ya punda na ndege wanaowinda na hadithi zinazothibitisha hukumu mbalimbali kuhusu diyah, n.k. ni mifano ya hadithi inayoonesha kuwa hadithi zinaweza kuwa ni chanzo cha sheria za kutegemewa.
Tulichokieleza hadi sasa kinaonesha nafasi ya hadithi (sunnah) katika dini ya Uisilamu. Ukweli kuwa ni lazima kuzipa umuhimu hadithi kama ni chanzo kinachokuja mara tu baada ya Quran kutoka katika nukta ya mtazamo wa dini ya Uisilamu na kutenda kwa mujibu wa sunnah za Mtume kumeamrishwa kwa hotuba za dhahiri na wote wawili Allah na mjumbe Wake Bwana Muhammad (s.a.w.). Aya zifuatazo zinazohusiana na suala hilo zimo ndani ya Quran.
“Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu.” (Aal-i Imran, 3/31);
“Sema: Mt’iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka basi Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.” (Aal-i Imran, 3/32);
“Na mt’iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa. (Aal-i Imran, 3/132);
“Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho. (al-Hashr, 59/7).
Kama inavyoonekana, katika aya kama hizo hapo juu, kumtii Mjumbe wa Allah (s.a.w.) kumeamrishwa pamoja na kumtii Allah; hata pia imeelezwa wazi kuwa kumtii Mtume (s.a.w.) kunamaanisha ni kumtii Allah.
Katika hadithi fulani, Mjumbe wa Allah (s.a.w.) amesema, “Jueni ya kwamba nimepewa Quran na mfano wake (sunnah). Utafika wakati mtu ameshiba juu ya kochi lake atasema: Ihifadhini Quran; mkikuta jambo la halali ndani yake lihalalisheni, na mkikuta linalokatazwa likatazeni. Bila ya shaka yoyote, lile ambalo Mjumbe wa Allah ameliharamisha ni kama vile Allah ameliharamisha.” (Abu Daawd Sunnah, 5; Ibn Majah, Muqaddima, 2; Ahmad b. Hanbal, Musnad, IV,131), akiwaonya Waisilamu dhidi ya wale wote wanaodharau sunnah na wanaotaka kuitenganisha kutokana na dini na kutilia mkazo kuwa dini haiwezi kuzingatiwa bila ya sunnah.

Comments
Post a Comment