Aya 90 – 93: Mwenyezi Mungu Anaamrisha Uadilifu Na Hisani
Lugha
Kwa kawaida kila analojilazimisha nalo mtu kwa hiyari yake ni Ahadi. Ahadi inakuwa ni wajib kuitekeleza ikiwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuambatanishwa na jina lake; mfano kusema: ‘Nimemwahidi Mwenyezi Mungu kufanya jambo fulani’ au ‘Nimejilazimisha ahadi ya Mwenyezi Mungu kufanya jambo fualani’ Kuvunja ahadi hii ni kama kuvunja kiapo, inabidi kutoa kafara; kama ilivyoelezwa katika vitabu vya Fiqh.
Maana
Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na hisani na kuwapa jamaa na anakataza uchafu na uovu na dhulma.
Aya imeamrisha mambo matatu mazuri na kukataza matatu maovu. Ama matatu mazuri ni haya yafuatayo:
1. Uadilifu: Mtu mwadilifu ni yule anayewafanyia insafu watu yeye mwenyewe na kuwafanyia yale yaliyo wajibu kuwafanyia.
2. Hisani: Inakusanya kila jambo la kheri. Watu wanafahamu kuwa hisani ni kujitolea mtu kwa mali yake au juhudi yake katika njia ya kheri.
3. Kuwapa jamaa: Huko pia ni kufanya hisani. Mwenyezi Mungu amekuhusisha kukutaja peke yake kwa kukukweza kutokana na ubora wake.
Ama matatu mabaya ni:
1. Uchafu; kama zinaa, ulawiti, pombe, kamari, uwongo na uzushi. Uchafu ulio dhahiri zaidi ni zinaa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَا ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا {32}
“Wala msiikurubie zinaa; hakika hiyo ni uchafu na njia mbaya.” (17:32).
2. Uovu: Ni kila linalopingana na akili na sharia.
3. Dhulma: Ni kuwafanyia uadui watu kwa kauli au vitendo. Hukumu yake kesho mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na shirki, bali dhulma ni zaidi. Kwa sababu shrki ni kuifanyia uadui haki ya Mwenyezi Mungu ambaye anaweza kuisamehe. Lakini dhulma ni kuifanyia uadui haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya watu.
Mara nyingine uchafu unaitwa uovu na uovu unaitwa uchafu. Yote hayo mawili ni dhulma.
Anawapa mawaidha ili mpate kukumbuka.
Makusudio ya mawaidha yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni kuamrisha kwake mambo mazuri na kukataza kwake mambo mabaya. Lengo la mawaidha ni kuwa tuwe waumini wenye takua, wema na wasafi. Wapokezi wa Hadith wamepokea kutoka kwa Ibn Mas’ud kwamba Aya hii ndiyo iliyokusanya zaidi mambo ya kheri na ya shari katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Amesema Uthman Bin Madh’un: “Nilisilimu kwa kumstahi Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na haukuingia Uisalmu moyoni mwangu mpaka iliposhuka Aya hii. Kwa hiyo nikamwamini Muhammad (s.a.w.) na nikamwendea ami yake, Abu Twalib, nikampa habari ya jambo langu hilo, akasema: ‘Enyi maquraish! Mfuateni Muhammad mtaongoka. Kwa sababu yeye hawaamuru isipokuwa tabia nejema.”
Na tekelezeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapoahidi.
Kumwahidi Mwenyezi Mungu kunaweza kuwa kwa mambo mawili: Kwanza, kukata mtu katika nafsi yake kumwahidi Mwenyezi Mungu kufanya jambo fulani au kuliacha; kama kusema: ‘Namwahidi Mwenyezi Mungu kuwa nitafanya jambo kadhaa au kuacha jambo kadhaa’
Aina ya pili ni kumwamini Mwenyezi Mungu. Kwa sababu mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu anakuwa amempa ahadi Mwenyezi Mungu kufuata amri yake na kukatazika na makatazo yake.
Ahadi zote hizi mbili ni wajibu kuzitekeleza. Makusudio ya ahadi kwenye Aya hii ni aina ya kwanza ya ahadi tuliyoieleza.
Wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha.
Makusudio ya kuvidhibitisha hapa ni kuvifunga hivyo viapo, yaani kuapa. Kwa sababu kiapo kinafungika ikiwa si kwa kumwasi Mwenyezi Mungu na wala hakifungiki, kivyovyote, ikiwa ni kwa jili ya kumwasi.
Imesemekana kuwa makusudio ya kuvithibisha hapa ni kuvitilia mkazo na kuvisisitiza. Lakini maelezo haya ni kutatizika. Ambapo maana yake yatakuwa viapo visivyosisitizwa havina wajibu wa kuvitekeleza na inajulikana kuwa kiapo kikitimia basi ni wajibu kukitekeleza, kiwe kimesisitizwa au la.
Ilhali mmekwishamfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu.
Kila aliyeapa kwa jina la Mwenyezi Mungu amemfanya Mwenyezi Mungu ni mdhamini kiutekelezaji. Akivunja kiapo basi atakuwa amemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu hasa, na atastahiki adhabu.
Hakika Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya.
Mwenye kutekeleza ahadi yake na kiapo chake, Mwenyezi Mungu atamlipa thawabu za watiifu na mwenye kuvunja na akafanya hiyana atamwadhibu adhabu ya waasi.
Kwa hakika ilivyo ni kwamba ahadi na kiapo vinafunguka ikiwa kuacha ni bora kuliko kutekeleza. Kwa mfano, mtu akiapa au kumwahidi Mungu kuwa hatakula nyama na ikawa kuacha kula nyama kuna manufaa ya afya yake, basi kiapo au ahadi itafungika.
Na kama baadae, ukimtokea ulazima wa kula nyama, atakula na kiapo au ahadi itafunguka na hatakuwa na chochote. Kuna hadith isemayo: “Ukiona heri yoyote katika kiapo chako basi kiache”
Wala msiwe kama mwanamke ambaye ameufumua uzi wake baada ya kuusokota na kuwa mgumu.
Kila kitu kinachovunjwa baada ya kufungwa basi kimefumuka, kiwe uzi, kamba au kitu chochote.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amepiga mfano wa kuvunja ahadi na uzi uliofumuliwa baada ya kusokotwa.
Inasemekana kuwa huko Makka kulikuwa na mwanamke mmoja mpum- bavu aliyekuwa akisokota sufu yake asubuhi na ikifika jioni anaifumua, na Mwenyezi Mungu akamfananisha na mvunja ahadi.
Vyovyote iwavyo ni kuwa Aya inatilia mkazo kauli yake Mwenyezi Mungu: ”Wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha.”
Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa kundi moja lina nguvu zaidi kuliko jengine.
Yaani msijaalie viapo vyenu kuwa ni nyenzo ya kudanganya na hiyana; kwa kuapa mbele ya wale walio wengi na wenyenguvu zaidi kuliko nyinyi ili wawaamini, wakati nyinyi mnadhamiria kuvunja viapo hivyo na muwaache wale ambao mliapa mbele yao pale mtakapojiona nyinyi mna nguvu zaidi kuliko wao.
Hakika Mwenyezi Mungu anawajaribu kwayo
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawakalifisha waja ili atii mtiifu kwa hiyari yake na aasi muasi kwa hiyari yake; kisha kila mmoja amlipe malipo yake anayostahiki. Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 7 (5:94)
Na hakika atawabainishia siku ya Kiyama yale mliyokuwa mkihitali- fiana.
Mwenyezi Mungu atawarudisha waja siku ya kiyama ili ajulikane mtiifu na mbatilifu na amlipe kila mmoja stahiki yake.
Na Mwenyezi Mungu angelitaka bila shaka angeliwafanya umma mmoja.
Yaani kama Mwenyezi Mungu angelitaka kumlazimisha mtu kuamini watu wote wangelikuwa umma mmoja, lakini amemwachia mtu na hiyari yake. Kwani lau angelimnyang’anya uhuru huu na hiyari, angelikuwa sawa na mnyama Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 7 (6: 35) na katika Juz. 12 (11:118).
Lakini humpoteza anayemtaka na humwongoa anayemtaka.
Hakuna shaka kwa mwenye akili kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi wala kumwongoza yeyote kwa lazima. Lau ingelikuwa hivyo isingelikuwa sawa kumuuliza na kumchukulia hisabu. Naye amesema mara tu baada ya maneno hayo:
Hakika mtaulizwa kuhusu yale mliyokuwa mkiyafanya.
Maana ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamzingatia mtu kuwa ni mpotevu baada ya yeye mwenyewe kufuata njia ya upotevu, na anamzingatia ni mwongofu baada ya kufuata njia ya uwongofu; sawa na anavyomuua anayeamua kujinyonga.
Yametangulia maelezo kuhusu uongofu na upotevu katika Juz. 1 (2:26), Juz. 3 (2: 272) na Juz. 5 (4:88).
Yametangulia maelezo kuhusu uongofu na upotevu katika Juz. 1 (2:26), Juz. 3 (2: 272) na Juz. 5 (4:88).
وَلَا تَتَّخِذُوا أَيْمَانَكُمْ دَخَلًا بَيْنَكُمْ فَتَزِلَّ قَدَمٌ بَعْدَ ثُبُوتِهَا وَتَذُوقُوا السُّوءَ بِمَا صَدَدْتُمْ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۖ وَلَكُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ {94}
Wala msivifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu. Na mkaonja maovu kwa sababu ya kuzuilia kwenu njia ya Mwenyezi Mungu na mkapata adhabu kubwa.
وَلَا تَشْتَرُوا بِعَهْدِ اللَّهِ ثَمَنًا قَلِيلًا ۚ إِنَّمَا عِنْدَ اللَّهِ هُوَ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ {95}
Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hakika kilicho kwa Mwenyezi Mungu ndio bora kwenu ikiwa mnajua.
مَا عِنْدَكُمْ يَنْفَدُ ۖ وَمَا عِنْدَ اللَّهِ بَاقٍ ۗ وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُوا أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {96}
Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobaki. Na kwa hakika tutawalipa waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {97}
Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ {98}
Unaposoma Qur’an muombe Mwenyezi Mungu akulinde na shetani mwenye kufukuzwa.
إِنَّهُ لَيْسَ لَهُ سُلْطَانٌ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ {99}
Hakika yeye hana madaraka juu ya walioamnini na wakamtegemea Mola wao.
إِنَّمَا سُلْطَانُهُ عَلَى الَّذِينَ يَتَوَلَّوْنَهُ وَالَّذِينَ هُمْ بِهِ مُشْرِكُونَ {100}
Hakika madaraka yake yako juu ya wale tu wanaomtawalisha na wale ambao kwaye wanashirikisha.

Comments
Post a Comment