Aya 106 – 111: Moyo Wake Umetua Juu Ya Imani
Aya 106 – 111: Moyo Wake Umetua Juu Ya Imani
Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake.
Tabari ametaja njia nne za irab ya jumla hii. Razi ametaja njia nne na akachagua moja kuwa iko mahali pa maf ’ul; kwa maana ya kukadiriwa kuwa, ninamkusudia kumtaja anayemkufuru...
Ama sisi tumechagua kuwa iko mahali pa mubdata (jumla ya kuanzia maneno) na Khabar yake (ukamailisho wake) ni jumla inayokadirwa kuwa, anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yake. Jumla hii inafahamika kutokana na jumla iliyo mwishoni mwa Aya hiyo hiyo: ‘Basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao.’
Isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya imani.
Hii inafahamisha kuwa iko ruhusa ya kutamka neno la kufuru kwa ajili ya kujiokoa na kuuuliwa ikiwa mwenye kutamka ni muumini wa kweli.
Imeelezwa katika tafsiri ya Razi: “Watu walilazimishwa neno la kufuru. Miongoni mwao ni Ammar na wazazi wake Yasir na Summayya. Vilevile Suhayb, Bilal, Khabbab na Salim. Wote hao waliaadhibiwa.
Summayya alifungwa baina ya ngamia wawili na akachomwa mkuki moyoni mwake na Yasir naye pia akauawa, lakini Ammar aliwapatia kile walichotaka kwa ulimi wake, akiwa amelazimika kufanya hivyo. Baadhi ya watu wakasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika Ammar amekufuru..”
Mtume (s.a.w.) akasema: “Hapana! Hakika Ammar imani imemmjaa kuanzia utosini mwake hadi nyayoni mwake.”
Ammar akamajia Mtume huku akilia. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) akawa anampangusa machozi na kumwambia: “Kwani una nini? Wakikurudia, rudia uliyosema.” Yametangulia maelezo ya Taqiya katika Juz. 3 (3:28).
Lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao na watapata adhabu kubwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu kumtaja muumini halisi aliyedhihirisha kufu- ru, kuwa yeye anakubaliwa udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu; sasa anamtaja yule kafiri wa kweli asiyekuwa na jengine zaidi ya kupendelea ukafiri. Hakuna malipo kwa huyu isipokuwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake kali.
Hiyo ni kwa sababu wao wamestahabu maisha ya dunia kuliko ya Akhera.
Hiyo ni ishara ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Wamestahabu, yaani wameathirika zaidi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawaondolea makafiri rehema yake na atawaadhibu kwa moto wake, kwa sababu wao wameathirika zaidi na maisha ya dunia na starehe zake.
Maana ya yote haya ni kuwa kila mwenye kuathirika na matamanio kuliko haki na mambo ya sasa kuliko yajayo, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama kafiri na mshirikina katika kustahiki ghadhabu na adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na kwamba Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu hawazingatii kuwa ni wenye kuongoka baada ya kustahabu ukafiri kuliko imani. Vilevile hawaongozi kwa maana ya kuwa hawalipi thawabu. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu amewaongoa kwa maana ya kuwa amewawekea dalili za kutosha juu ya kuweko kwake Mwenyezi Mungu na utume wa mitume yake. Mwenyezi Mungu anasema:
وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ{17}
“Na ama Thamud tuliwaongoa, wakastahabu upofu kuliko uongofu” (41:17).
Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga chapa juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na hao ndio wenye kughafilika.
Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz. 1 (2:2).
Hapana shaka kwamba wao ndio wenye kuhasirika Akhera.
Wala hapana hasara kubwa zaidi kuliko ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Kisha hakika Mola wako kwa wale waliohajiri baada ya kusumbuliwa kisha wakafanya jihadi na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja waumini halisi na makafiri dhahiri, hapa sasa anataja wale waliokuwa wamemwamini Mtume, lakini wakabakia Makka na wasihame naye kwenye Hijra. Wakawapa washirikina baadhi ya waliyoyataka. Kisha wakatubia, wakahama kwa Mtume na wakasubiri kwa kupigania jihadi dhidi ya washirikina na wafisadi. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha hukumu ya ya hawa kwa kusema: “Bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.”
Makusudio ya baada ya hayo ni hayo waliyoyatenda; kama unavyofahamisha mfumo wa maneno. Inawezekana pia ni kwa maana ya baada ya kutubia kwao pamoja na kuhama, jihadi na subira.
Katika tafsiri nyingi imeeelezwa kuwa Aya hii ilishuka kwa sababu ya jamaa fulani katika maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) waliokuwa wamebaki nyuma Makka na wasihame pamoja na Mtume. Washirikina wakawapa shida sana mpaka baadhi yao wakafitinishwa na dini yao; kisha wakajuta, lakini wakahofia kuwa toba yao haitatakabaliwa; ndipo ikashuka Aya hii.
Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea.
Yaani kila mtu siku ya Kiyama atajitetea mwenyewe, wala hatajishuguhulisha na mwingine:
لِكُلِّ امْرِئٍ مِنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ {37}
“Kila mtu siku hiyo atakuwa na jambo linalomshughulisha” (80:37).
Na kila nafsi italipwa sawa na yale iliyoyafanya, nao hawatadhulumi- wa.
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {22}
“Na ili ilipwe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa” (45:22)
na pia kauli yake:
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا تَسْعَىٰ {15}
“Ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyahangaikia” (20:15).
Yamekaririka maana ya Aya hii katika Aya nyingi.
وَضَرَبَ اللَّهُ مَثَلًا قَرْيَةً كَانَتْ آمِنَةً مُطْمَئِنَّةً يَأْتِيهَا رِزْقُهَا رَغَدًا مِنْ كُلِّ مَكَانٍ فَكَفَرَتْ بِأَنْعُمِ اللَّهِ فَأَذَاقَهَا اللَّهُ لِبَاسَ الْجُوعِ وَالْخَوْفِ بِمَا كَانُوا يَصْنَعُونَ {112}
Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hiyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na hofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
وَلَقَدْ جَاءَهُمْ رَسُولٌ مِنْهُمْ فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ وَهُمْ ظَالِمُونَ {113}
Na alikwishawajia Mtume kutoka miongoni mwao, lakini wakamkadhibisha, basi ikawafikia adhabu hali ya kuwa wamedhulumu.

Comments
Post a Comment