Aya 1-5: Hiyo Ni Aya Za Kitabu
Alif laam Raa.
Umetangulia mfano wake na maelezo yake katika Juz. 1, mwanzo wa Sura ya Baqara
Hiyo ni Aya za Kitabu na Qur’an inayobainisha.
Hiyo, ni ishara ya hiyo Sura yenyewe tunayoifasiri. Makusudio ni kueleza kuwa hiyo ni miongoni mwa Aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu na ni Qur’an inayopambanua baina ya haki na batili.
Huenda waliokufuru wakatamani wangekuwa Waislamu.
Neno ‘Huenda’ hapa lina maana ya maana ya wingi; yaani kila mmoja kati ya wenye makosa, kesho atafunukiwa na pazia na atatamani lau angelikuwa hapa duniani ni miongoni mwa wenye takua ambao wameisalimisha haki na wakaitumia. Angalia kifungu cha maneno ‘Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu’ katika Juz. 3. (3:19).
Waache wale (chakula), na wastarehe na iwazuge tamaa; watakuja jua.
Waliathirika na starehe za duniani, Mwenyezi Mungu akawahadharisha na yatakayowapata kesho miongoni mwa adhabu kali.
Na hatukuangamiza mji wowote ule ila una Kitabu maalum.
Kana kwamba muulizaji ameuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu haharakishi adhabu ya wale waliomuasi Yeye na mitume yake? Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa kila adhabu ina muda wake na kwamba Yeye, ambaye imetukuka hekima yake, hakuangamiza umma wowote hapo nyuma ila baada ya kufikia muda wake. Mjinga ni yule anayedanganyika na muda.
Hauwezi umma wowote kuitangulia ajali yake wala kuchelewa.
Angalia kifungu cha ‘Ajali haina kinga’ Juz. 4. (3:145).
وَقَالُوا يَا أَيُّهَا الَّذِي نُزِّلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ {6}
Na walisema: “Ewe uliyeteremshiwa ukumbusho! Wewe ni mwendawazimu.
لَوْ مَا تَأْتِينَا بِالْمَلَائِكَةِ إِنْ كُنْتَ مِنَ الصَّادِقِينَ {7}
Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?”
مَا نُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ إِلَّا بِالْحَقِّ وَمَا كَانُوا إِذًا مُنْظَرِينَ {8}
Hatuteremshi Malaika ila kwa haki na hapo hawatapewa muda.
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ {9}
Hakika sisi tumeuteremsha ukumbusho huu na hakika sisi ndio tuulindao.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِكَ فِي شِيَعِ الْأَوَّلِينَ {10}
Na hakika tulikwishawatuma Mitume kabla yako katika mataifa ya mwanzo.
وَمَا يَأْتِيهِمْ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ {11}
Na hakuwajia Mtume ila walikuwa wakimfanyia stihzai.
كَذَٰلِكَ نَسْلُكُهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ {12}
Hivyo ndivyo tunavyouingiza katika nyoyo za wakosefu.
لَا يُؤْمِنُونَ بِهِ ۖ وَقَدْ خَلَتْ سُنَّةُ الْأَوَّلِينَ {13}
Hawauamini na hali umewapitia mfano wa wa kwanza.
وَلَوْ فَتَحْنَا عَلَيْهِمْ بَابًا مِنَ السَّمَاءِ فَظَلُّوا فِيهِ يَعْرُجُونَ {14}
Na lau tungeliwafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda.
لَقَالُوا إِنَّمَا سُكِّرَتْ أَبْصَارُنَا بَلْ نَحْنُ قَوْمٌ مَسْحُورُونَ {15}
Basi wangelisema: Macho yetu yamelevywa; bali sisi ni watu waliorogwa.
وَلَقَدْ جَعَلْنَا فِي السَّمَاءِ بُرُوجًا وَزَيَّنَّاهَا لِلنَّاظِرِينَ {16}
Hakika tumeweka katika mbingu buruji na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
وَحَفِظْنَاهَا مِنْ كُلِّ شَيْطَانٍ رَجِيمٍ {17}
Na tukazilinda na kila shetani afukuzwaye.
إِلَّا مَنِ اسْتَرَقَ السَّمْعَ فَأَتْبَعَهُ شِهَابٌ مُبِينٌ {18}
Isipokuwa asikilizaye kwa kuiba, naye hufuatwa na kijinga kinachoonekana.

Comments
Post a Comment