NAMNA YA KUHIJI
- Mwenye kuhiji atahirimia (atanuia kuingia katika ibada ya hija) siku ya nane ya mwezi wa Dulhijja akiwa Makka. Atatia nia moyoni mwake; kwa maana ya kuingia katika ibada ya hija. Atatamka kwa ulimi wake: «Labbaika llaahumma hajjan». Maana yake ni kwamba: (Ewe Mola wangu, nimeitikia kuja katika hija). Baada ya kunuia huko ataleta Talbiya akitangaza utumishi, ufuasi na kuitikia wito wa Muumba pekee kwa kusema: «Labbaika-llaahumma labbaiik. Labbaika laa shariika laka labbaiik. Innalhamda, wanniimata, laka walmulk. Laa shariika laka labbaiik». Maana yakeni kwamba: Nimekuitikia Mola wangu, nimekuitikia. Nimekuitiki ewe usiye na mshirika nimekuitikia. Hakika, sifa njema na neema na ufalme ni vyako wewe tu. Huna mshirikia. Nimekuitikia
Atavaa nguo za Ihramu, na atajizuia asifanye mambo yote yaliyokatazwa na ambayo mwenye kuingia katika ibada ya hija anakatazwa kuyafanya mpaka akomboke na kumaliza, kama inavyo oneshwa katika jedwali ya pembeni:
- Sheria inamtaka kwamba baada ya kuhirimia siku ya nane ya mwezi wa Dhul-hijja aende Mina wakati wa Dhuhaa, alale hapo, aswali hapo swala ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Ishaa na Alfajiri. Kila swala aiswali kwa wakati wake bila ya kujumuisha, pamoja na kupunguza swala za rakaa nne na kuziswali kwa rakaa mbili mbili.
- Katika siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-hijja atakwenda Arafa baada ya kuchomoza kwa jua. Ataswali Adhuhuri na Alasiri kwa kuzijumuisha na kupunguza rakaa kwa Adhana moja na Iqama mbili. Halafu watu wataomba dua na kujinyongesha mbele ya Allah. Arafa ndio tukio kubwa sana miongoni mwa matukio ya hija mpaka Mtume,swallalahu alayhi wasalam, ameeleza kwamba Allah hujivuna mbele ya Mailaika wake kupitia watu walioko Arafa kutokana na hali waliyo nayo ya kuomba dua, unyenyekevu na kumlilia Allah. Mtume swallalahu alayhi wasalam anasema kwamba: «Hawa ni waja wangu wamenijia wakiwa nywele kitimtim, wamejaa vumbi. Ninakushuhudizeni kwamba nimewasemehe». (Ahmad, Hadithi Na. 7089).
- Ataondoka Arafa kwa utulivu baada ya kuzama kwa jua akielekea Muzdalifa. Ataswali Magharibi na Isha kwa kuzijumuisha. Atalala Muzdalifa na kuswali Alfajiri hapo. Ni sunna kwake kumtaja Allah na kumuomba mpaka kupambazuke na kabla ya kuchomoza kwa jua. Inafaa kwa wanawake, watu wenye udhaifu na wazee pamoja na wanaofuatana nao kuondoka Muzdalifa baada ya usiku kugawanyika nusu.
- Ataondoka Muzdalifa kabla ya kuchomoza kwa jua kwenda Mina. Hii ni siku ya Eid. Sheria inamtaka aliyemo katika ibada ya hija kufanya mambo kadhaa katika siku ya Eid, na amabayo ni haya:
- Kuurushia vijiwe saba mnara mkubwa huku akileta Takbira katika kila kijiwe anacho rusha. Minara (Jamaraat) ni sehemu ambazo shetani alimuwekea pingamizi baba wa Mitume Ibrahimu, Allah amfikishie amani, kwa kumshawishi asitekeleze amri ya Allah. Mtume Ibrahimu alimrushia vijiwe saba shetani huyo. Allah amelifanya tukio hilo kuwa sheria kwetu. Kwa hiyo, tunalifanya hilo kwa ajili ya kumtii Allah Mtukufu, kufuata vile alivyotuamrisha, kumuiga Mtume wa Allah ambaye pia amefanya hivyo, na pia tunafanya hivyo ili tuzipe nafsi zetu msukumo wa kupambana na shetani na udhaifu uliopo katika nafsi zetu na uchaguzi wetu wa mambo ya kufanya.
- Atachinja mnyama wake hapo Mina au Makka siku ya Eid. Muda wa kuchinja unaendelea siku tatu baada yake. Atakula, atatoa zawadi na atatoa sadaka. Kama hana uwezo wa kununua mnyama wa kuchinja, atafunga siku tatu akiwa hija na siku saba atakapo rejea nyumbani kwake. Inawezekana kwa mwenye kuhiji kuipa uwakala taasisi inayoaminika kwa ajili ya kuchinja mnyama wake na kugawa nyama yake kwa wenye shida.
- Atanyoa nywele zake au atapunguza. Kwa hatua hii, atakuwa amekomboka (Uhuru wa kwanza). Kwa maana hiyo, ataruhusiwa kufanya yote aliyokatakazwa kufanya kwa sababu ya kuingia katika ibada ya hija isipokuwa tu kukutana kimwili na mkewe
- Ataelekea Makka ili kutufu Tawafu Ifadha(twawaf ya hijja), mara saba kuzunguka Kaba Tukufu. Tawafu Ifadha ni moja ya nguzo za hija. Halafu baada yake atakwenda kufanya Saayi ya hija. Kwa kufanya Tawafu, atakuwa amehalalishiwa yote aliyokatazwa kufanya kwa kuingia katika ibada ya hija. Kila kitu kilichokuwa haramu kwa sababu ya Ihramu kitakuwa halali kwake, hata kukutana na mkewe. Inawezekeana kwake kuahirisha kufanya Tawafu siku ya Eid iwapo itakuwa uzito kwake.
- Kisha atarejea Mina na kulala hapo siku mbili kwa mwenye kufanya haraka kuondoka na siku tatu kwa watakao chelewa kuondoka. Sheria inamtaka kuirushia vijiwe minara mitatu kila siku baada ya jua kupinduka kutoka usawa wa kati (muda wa swala ya Adhuhuri): Mnara mdogo (ambao uko mbali na Makka), kisha Mnara wa kati, kisha Mnara mkubwa ambao aliurushia vijiwe siku ya Eid.
- Atakapo taka kuondoka Makka itamlazimu, kabla ya kuondoka, atufu Tawafu ya kuaga, ili uhusiano wake wa mwisho na Kaaba Tukufu uwe kuitufu.
Mambo ya haramu kufanya ukiwa umehirimia.
- Kunyoa nywele au kuzipunguza. Na ni mfano wake kukata kucha.
- Kutumia manukato, sawa iwe kwenye nguo yake au mwilini mwake
- Kukutana kimwili mke na mume. Pia kugusa na kukumbatia iwapo kutafanyika kwa matamanio.
- Kufunga ndoa; ni sawa aliyeingia katika ibada ya hija ni mwanaume au mwanamke.
- Mwenye kuingia katika ibada ya hija anakatazwa kuwinda mnyama. Haifai kwake kuwinda ndege na wanyama pori.
- Makatazo yanayowahusu wanaume tu ni haya:
- Kuvaa nguo inayo onesha mchanganuo wa maungo kwa namna kwamba kila kiungo kinabainisha nguo iliyovaa na kujitenga, kama vile shati, kanzu, nguo ya ndani, suruali na mfano wake.
- Kufunika kichwa kwa kitu kinacho gusana na kichwa. Ama mapaa ya majengo, vyombo vya usafiri na myamvuli inayofunika kichwa haina ubaya.
- Makatazo yanayomhusu mwanamke tu ni haya:
- Kuvaa barakoa (nikabu) na kufunika uso. Jambo linalotakiwa na sheria ni mwanamke kufunua uso wake, isipokuwa tu watakapo pita mbele yake wanamume ambao sio maharimu zake. Hapo anaweza kufunika uso wake na haitamdhuru iwapo hiki anachotumia kufunikia uso wake kitaugusa uso.
- Kuvaa glovu(soksi za mikononi).
Mwenye kufanya lolote kati ya haya yaliyokatazwa kwa kusahau au kwa kutojua au kwa kulazimishwa, hana kosa, kwa mujibu wa kauli ya Allah isemayo kwamba: «Na hakuna ubaya kwenu katika yale ambayo mmeyafanya kwa kukosea, na lakini ubaya upo katika yale ambayo nyoyo zenu zimekusudia kuyafanya». (Sua Al-ahzaab, aya 5). Lakini iwapo atakumbuka au akapata kujua kuwa haifai kuyafanya, basi aliache haraka hilo alilokatazwa.
Msikiti wa Khaif na mahema ya mahujaji yanaonekana huko Mina.
Umra
Ni kumuabudu Allah kwa kuhirimia (kunuia kuingia katika ibada ya Umra = Ihraam), kuzunguka Kaaba mara saba, kufanya Saayi kati ya Swafaa na Mar`wa mara saba, kisha kunyoa au kupunguza nywele.
Hukumu yake: Ni wajibu kwa watu mwenye uwezo, mara moja tu katka umri. Ni jambo linalo pendekezwa kurudia rudia kufanya Umra.
Wakati wake: Inafaa kufanya Umra muda wotewote wa mwaka, lakini kuifanya katika mwezi wa Ramadhani kuna malipo mengi zaidi, kama Mtume,swallalahu alayhi wasalam, alivyosema kuwa: «Umra ndani ya Ramadhani inahukumika kuwa ni kuhiji pamoja na mim». (Bukhari, Hadithi Na. 1863).
Comments
Post a Comment